Arsenal yasitisha mazungumzo, Sporting ikigomea bei ya Gyokeres

Muktasari:
- Mbali na Gyokeres, Arsenal wamehusishwa na nia ya kumsajili winga wa Chelsea, Noni Madueke, pamoja na nyota wa Crystal Palace, Eberechi Eze, kama mbadala endapo dili la mshambuliaji huyo litashindikana.
Lisbon, Ureno. Hatma ya mshambuliaji wa Kimataifa wa Sweden, Viktor Gyokeres kujiunga na Arsenal imeingia dosari, baada ya mazungumzo kati ya The Gunners na Sporting CP kugonga mwamba kutokana na sintofahamu ya thamani ya uhamisho.

Arsenal, ambao tayari wameshakamilisha usajili wa nyota kadhaa akiwemo Martin Zubimendi kutoka Real Sociedad kwa dau la Sh198 bilioni, Kepa Arrizabalaga kutoka Chelsea Sh16.5 bilioni, na Christian Norgaard wa Brentford Sh39.6 bilioni, walitarajiwa kumaliza dili la Gyokeres wiki hii, lakini mambo sasa yamegeuka.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Ureno, hakuna maendeleo yoyote tangu mwishoni mwa wiki huku mazungumzo yakidaiwa kukwama kwenye suala la ada ya uhamisho. Sporting wanataka dau la moja kwa moja la €70 milioni (Sh196 bilioni), wakati Arsenal wameshatuma ofa ya €65 milioni (Sh182 bilioni) pamoja na nyongeza ya Sh42 bilioni ikiwa ni jumla ya Sh224 bilioni.

Taarifa zinaeleza kuwa Arsenal walidhani kuna makubaliano ya awali baina ya Gyokeres na Sporting kwamba angetolewa kwa kiasi cha €60 milioni (Sh168 bilioni) pamoja na nyongeza ya €10 milioni (Sh28 bilioni). Hata hivyo, klabu hiyo ya Ureno inaonekana kugeuka msimamo na kushikilia bei ya juu zaidi.
Kutokana na hali hiyo, jarida la Record la Ureno limeripoti kuwa wawakilishi wa Arsenal waliokuwa Lisbon kwa mazungumzo tayari wamerejea London bila makubaliano yoyote, hali inayoashiria huenda klabu hiyo ikaachana kabisa na dili hilo endapo hakutakuwa na mabadiliko kutoka upande wa Sporting.

Gyokeres mwenyewe anaripotiwa kuwa tayari kujiunga na Arsenal na ameonesha kujitolea kwa kiwango kikubwa, akidaiwa kufikia hatua ya kukubali kupunguza mshahara wake kwa kiasi cha €2 milioni (Sh4.6 bilioni) ili kurahisisha dili hilo.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa zamani wa Coventry City na Brighton hajahudhuria mazoezi ya Sporting na ameeleza wazi kutotaka tena kuichezea timu hiyo, akihisi amevunjwa moyo na uongozi wa klabu kwa kukiuka makubaliano ya awali kuhusu bei yake ya kuuzwa.
Gyokeres, mwenye umri wa miaka 27, amebakiza miaka mitatu kwenye mkataba wake na Sporting lakini ni wazi kwamba hatamaliza mkataba huo, hasa baada ya kufunga mabao 54 msimu uliopita katika michuano yote akiwa na klabu hiyo.

Arsenal sasa wanasubiri maamuzi ya Sporting, huku taarifa zikidai kuwa mshambuliaji huyo anaweza pia kupelekwa kwa mkopo Fenerbahce ya Uturuki endapo dili na Arsenal litashindikana. Licha ya hali hiyo, Gyokeres anaripotiwa kuwa na nia ya dhati ya kurejea Ligi Kuu ya England.
Mbali na Gyokeres, Arsenal pia wamehusishwa na nia ya kumsajili winga wa Chelsea, Noni Madueke, pamoja na nyota wa Crystal Palace, Eberechi Eze, kama mpango mbadala endapo dili la mshambuliaji huyo litashindikana.