Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gyökeres akaribia kutua Arsenal

Muktasari:

  • Gyokeres aliwahi kueleza kiu yake ya kurudi Ligi Kuu England baada ya kushindwa kuonyesha makali yake alipokuwa Brighton.

London, England. Hatimaye Arsenal wako karibu kumalizana na Sporting Lisbon kuhusu usajili wa mshambuliaji hatari wa Sweden, Viktor Gyokeres, kwa ada ya pauni milioni 63.4, (Sh222 bilioni) huku ripoti zikieleza kuwa makubaliano ya pande zote mbili yako katika hatua za mwisho.

Kwa mujibu wa The Athletic, dili hilo limegawanywa katika malipo ya awali ya pauni milioni 54.8 (Sh192 bilioni) na nyongeza ya pauni milioni 8.4 kutegemea mafanikio ya mchezaji huyo Emirates.

Mkataba wa miaka mitano uko tayari, huku pande zote zikimalizia taratibu ndogo kabla ya kuthibitisha rasmi usajili huo ambao umekuwa miongoni mwa tetesi kubwa zaidi za usajili kiangazi hiki.

Dili hilo limekumbwa na mvutano wa miezi kadhaa, hasa kuhusu kiasi gani kilipaswa kulipwa mapema na namna ya kugawanya malipo. Iliripotiwa kuwa wakala wa Gyokeres alikubali kuachana na malipo yake ya kamisheni ili kufanikisha usajili huo, hatua iliyosaidia kuvuka kizingiti kilichobakia.

Taarifa kutoka gazeti la A Bola la Ureno zinaeleza kuwa hali ya mvutano huo ilimtoa machozi baba mzazi wa Gyokeres, huku kukiwa na hofu kuwa usajili unaweza kuvurugika dakika za mwisho.

Safari ya Asia na mustakabali wa Gyokeres

Arsenal tayari wapo kwenye ziara ya maandalizi ya msimu mpya barani Asia ambapo wanakabiliwa na mechi dhidi ya AC Milan na Newcastle huko Singapore, kabla ya kukipiga na wapinzani wao wa jadi Tottenham Hotspur huko Hong Kong.

Hata hivyo, Gyokeres anatarajiwa kujiunga nao baadaye, pengine kabla ya mechi ya maandalizi dhidi ya Villarreal Agosti 6 pale Emirates. Arsenal watamaliza maandalizi yao kwa mechi dhidi ya Athletic Club kabla ya kuanza rasmi kampeni ya Ligi Kuu Uingereza kwa mechi dhidi ya Manchester United ugenini.

Rekodi ya Gyokeres

Gyokeres amekuwa moto wa kuotea mbali nchini Ureno amefunga mabao 97 katika mechi 102 tangu ajiunge Sporting mwaka 2023 akitokea Coventry City kwa ada ya pauni milioni 20. Msimu uliopita pekee, alitikisa nyavu mara 54 kwenye michuano yote takwimu zilizomfanya kuwa mmoja wa washambuliaji tishio zaidi barani Ulaya.

Akiwa na umri wa miaka 27, anatarajiwa kuwa suluhisho la muda mrefu kwa Arsenal katika eneo la ushambuliaji, eneo ambalo limekuwa changamoto kubwa kwa Mikel Arteta kwa misimu kadhaa. Ikiwa usajili huu utakamilika, Gyokeres atakuwa msaada mkubwa Arsenal kwenye harakati zao za kutafuta taji la kwanza la EPL tangu 2004.

Malengo na kisasi dhidi ya Brighton

Katika mahojiano ya awali, Gyokeres aliwahi kueleza kiu yake ya kurudi Ligi Kuu England baada ya kushindwa kuonyesha makali yake alipokuwa Brighton:

“Ni moja ya ligi kubwa zaidi barani Ulaya. Nilitumia miaka kadhaa huko bila kucheza hata mechi moja. Basi bila shaka, ni jambo ambalo ningependa kufanya tena. Ingekuwa kisasi kikubwa sana.”