Guardiola aongeza presha CAF sakata la AFCON 2025
Muktasari:
- Sakata la AFCON 2025 limeendelea kuchukua sura mpya baada ya Meneja wa Manchester City, Pep Guardiola kushangaa uamuzi wa CAF kuipa Morocco ubingwa wa mezani.
Dar es Salaam. Meneja wa Manchester City, Pep Guardiola ameibua mjadala mpya kimataifa baada ya kuhoji uamuzi wa Shirikisho la Mpira wa (CAF) kubadili matokeo ya fainali ya AFCON 2025 na kuipa Morocco ubingwa, akisisitiza umuhimu wa uwazi katika maamuzi ya soka.
Guardiola amesema hajapata maelezo ya kina yanayofafanua msingi wa uamuzi huo, akionya kuwa hatua ya kubadilisha mshindi wa mashindano makubwa bila ufafanuzi wa wazi inaweza kuathiri taswira na uaminifu wa mchezo huo duniani.
“Maamuzi kama haya yanapaswa kueleweka kwa kila mdau. Lazima kuwe na ushahidi wa kutosha na mawasiliano rasmi ili kulinda heshima ya soka,” amesema.
Kauli hiyo imekuja wakati mjadala mkali ukiendelea barani Afrika na kimataifa, huku wadau wakitaka CAF kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu sababu zilizopelekea kubadilishwa kwa matokeo ya mechi hiyo.
Rais wa Senegal aibuka kwa kauli nzito
Wakati huo huo, Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, ametoa tamko kali akipinga uamuzi huo, akiuona kuwa umeibua maswali mazito kuhusu uadilifu wa uendeshaji wa soka la Afrika.
Katika kauli iliyosambaa kwa kasi, Faye amesema Senegal haitasita kujiondoa katika mashindano ya CAF iwapo hakutakuwa na mabadiliko ya msingi ndani ya shirikisho hilo.
Amesisitiza kuwa taifa lake haliko tayari kuvumilia kile alichokiita mfumo usio wa haki, akiongeza kuwa Senegal si taifa la kuogopa linapodai haki yake.
Tamko hilo limeongeza uzito wa kisiasa katika sakata hilo, huku likionyesha namna mgogoro huo ulivyovuka mipaka ya michezo na kugusa heshima ya taifa.
Weah aomba CAS iingilie kati
Naye Rais wa zamani wa Liberia na mshindi wa Ballon d’Or, George Weah, ameitaka mahakama ya usuluhishi wa masuala ya michezo kuingilia kati haraka, akisisitiza kuwa sheria za soka zinatambua mamlaka ya mwisho ya mwamuzi uwanjani.
Weah ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya tano ya mchezo, matokeo yaliyopatikana baada ya filimbi ya mwisho hayawezi kubadilishwa mezani, isipokuwa kwa misingi iliyo wazi na inayokubalika kisheria.
“Mpira unapaswa kuamuliwa uwanjani, siyo katika vyumba vya vikao baada ya mechi kumalizika,” amesisitiza.
CAF yamtetea Motsepe
Katika upande mwingine, msemaji wa CAF, Luxolo September, amemtetea vikali Rais wa CAF, Patrice Motsepe, dhidi ya tuhuma za rushwa na upendeleo.
Luxolo amesema Motsepe hawezi kushawishiwa kifedha, akieleza kuwa kiongozi huyo amekuwa akijitolea kwa rasilimali zake binafsi kuendesha shughuli za CAF bila kulipwa mshahara.
Amesema ni makosa kwa baadhi ya watu kudhani kuwa viongozi wa Afrika hawawezi kuwa waadilifu, akisisitiza kuwa hakuna ushahidi unaounga mkono tuhuma zinazotolewa.
Senegal yalinda kombe jeshini
Wakati sintofahamu ikiendelea, taarifa kutoka Senegal zinaeleza kuwa kocha Pape Thiaw amelipeleka kombe la AFCON katika kambi ya kijeshi kwa ajili ya ulinzi.
Hatua hiyo imetafsiriwa kama msimamo mkali wa taifa hilo, likisisitiza kuwa haliko tayari kukabidhi taji hilo hadi haki itakapopatikana.
Inaelezwa kuwa kombe hilo linalindwa saa 24 na wanajeshi, ikiwa ni ishara ya kulinda heshima ya taifa dhidi ya kile kinachoonekana kama uamuzi wa mezani usio wa haki.
Wataalamu: Mwamuzi ndiye mamlaka ya mwisho
Akichangia sakata hilo, aliyewahi kuwa mwamuzi wa CAS, Raymond Hack, amesema kisheria matokeo ya mechi hayawezi kubatilishwa baada ya kumalizika ikiwa mwamuzi aliruhusu mchezo kuendelea hadi mwisho.
“Baada ya filimbi ya mwisho, mshindi hutambulika rasmi. Hapo hakuna mjadala,” amesema.
Mustakabali wa soka la Afrika
Sakata hilo limeendelea kuongeza presha kwa CAF, huku wadau wengi wakisubiri uamuzi wa mwisho kutoka CAS ambao unaweza kuwa na athari kubwa kwa uendeshaji wa mashindano ya soka barani Afrika.
Kwa sasa, macho ya dunia yanaelekezwa kuona kama mgogoro huo utatatuliwa kwa misingi ya sheria na haki, au utaacha doa katika taswira ya soka la Afrika.