Geay, Simbu watua Paris kwenye Olimpiki 2024

Muktasari:
- Kwa upande wa Sakilu na Shauri wamepangwa kukimbia Agosti 11, 2024 kwa umbali wa kilomtea 42 kuanzia saa 3:00 asubuhi. Siku hiyo ndiyo itakuwa ya mwisho ya michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.
Wanariadha wanne wa Tanzania watakaoshiriki michezo ya Olimpiki 2024, wamewasili salama jijini Paris nchini Ufaransa wakiwa na tumaini la kulibeba taifa.
Wawakilishi hao wa Tanzania upande wa riadha ni nahodha wa timu ya taifa ya mchezo huo, Alphonce Felix Simbu, Gabriel Gerald Geay, Jackline Juma Sakilu na Magdalena Crispin Shauri ambapo waliwasili usiku wa kuamkia Agosti 8, 2024 wakiwa na kocha wao Anthony Njiku Mwingereza aliyekuwa akiwanoa kambini Arusha.
Baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Charles de Gaulle uliopo Paris, wanariadha hao walipokelewa na Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau.
Simbu na Geay watashiriki mbio za kilometa 42 wanaume Jumamosi Agosti 10, 2024 ambapo mashindano hayo yanatarajiwa kuanza saa 3:00 asubuhi.
Kwa upande wa Sakilu na Shauri wamepangwa kukimbia Agosti 11, 2024 kwa umbali wa kilomtea 42 kuanzia saa 3:00 asubuhi. Siku hiyo ndiyo itakuwa ya mwisho ya michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.
Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 ilianza Julai 26, 2024 na inatarajiwa kufikia tamati Agosti 11, 2024 ambapo Tanzania imekuwa na wawakilishi saba katika michezo tofauti.
Alianza mchezo judo Andrew Mlugu, kisha muogeleaji upande wa wanaume Collins Saliboko akifuatiwa na muogeleaji mwanamke Sophia Anisa Latiff ambao wote hao hakuna aliyeshinda medali yoyote.
Tumaini lililobaki kwa Watanzania ni kuona wanariadha hao wanne Simbu, Geay, Sakilu na Shauri wakilitoa kimasomaso taifa.