Gamondi: Nitapangua kikosi Yanga

Muktasari:
- Kauli hiyo inakuja muda mfupi baada ya Yanga kucheza mechi mbili ndani ya siku nne, moja ugenini dhidi ya Kagera na nyumbani ilipovaana na Dodoma Jiji.
Dar es Salaam: Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema kuwa kubana kwa ratiba ya Ligi Kuu kunamlazimisha kutoa nafasi kwa kundi kubwa la wachezaji kama njia ya kuepuka uchovu wa kikosi ambao unaweza kuchangia wasifanye vizuri.
Kauli hiyo ya Gamondi imekuja muda mfupi baada ya Yanga kucheza mechi mbili ndani ya siku nne moja ikiwa ya ugenini dhidi ya Kagera Sugar na kisha nyumbani dhidi ya Dodoma jiji na kuanzia kesho Februari 8 hadi Februari 25 italazimika kucheza mchi tano ndani ya siku 18 ikiwa na maana ya kuwa na siku tatu tu za kujiandaa kutoka mechi moja hadi nyingine.
Mrundikano huo wa mechi kwenye ratiba umetokana na viporo ambavyo Yanga na Simba wamekuwa navyo kutokana na kusogezwa mbele kwa baadhi ya mechi zao ili kuzipa nafasi timu hizo kujiandaa na kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumzia ugumu huo wa ratiba ulio mbele yake na ule ambao tayari timu yake imshakutana nao, Gamondi alisema kuwa namna pekee ya kukabiliana nao ni kufanya mabadiliko ya mara kwa mara ya vikosi ili kutochosha wachezaji.
"Kutokana na ugumu wa ratiba natarajia kufanya mabadiliko makubwa ya mara kwa mara kwenye kikosi ili kutoa nafasi ya wachezaji wengine kukusanya nguvu mpya huku wengine wakipambania timu kufikia malengo.
"Tumecheza leo, siku mbili mbele tuna mchezo mwingine wachezaji wanakosa muda wa kurudisha utimamu wa mwili, hilo linaweza kuwasababishia majeraha madogo madogo, ili kuepuka hayo nitafanya mabadiliko ya mara kwa mara na wala mtu asishangae.
"Nina imani kubwa na wachezaji waliopo kikosini naamini kila mmoja atafanya kazi yake kwa usahihi akipata nafasi ya kucheza, lengo ni moja kukusanya pointi zitakazotufanya tuweze kutetea ubingwa msimu huu," alisema kocha huyo raia wa Argentina.
Akizungumzia matokeo waliyoyapata ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex, alisema yatawasaidia kupunguza presha kwa wachezaji na anaamini mechi zijazo watacheza kwa kujiamini zaidi na kutumia nafasi.
"Timu ilikuwa inacheza kwa presha kila mchezaji alikuwa anatamani kufunga lakini haikuwa rahisi hivyo naamini ushindi wa bao moja dhidi ya Dodoma Jiji utaamsha hali ya ushindani na mwendelezo mzuri wa kufunga.
"Wachezaji wangu wamecheza vizuri, kukosa nafasi ni sehemu ya mchezo jambo zuri ni kwa kuwa hawajakata tamaa, wamepambana na kunipa pointi tatu, hilo limeongeza morali na naamini katika michezo ijazo watacheza kwa kujiachia bila presha," alisema Gamondi.
MECHI ZA YANGA
Yanga vs Mashujaa-Februari 8
Tanzania Prisons vs Yanga-Februari 11
KMC vs Yanga-Februari 17
Yanga vs CR Belouizdad- Februari 24
JKT Tanzania vs Yanga-Februari 26