Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fei Toto bosi mpya Azam

Muktasari:

  • Fei Toto amemaliza akiwa kinara wa kupiga pasi za mwisho katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/2025 ambapo alikuwa nazo 13.

Dar es Salaam. Mkataba mpya wa mwaka mmoja ambao Azam FC imempatia kiungo Feisal Salum hapana shaka unamfanya awe mchezaji ghali zaidi ndani ya kikosi cha Azam FC na pia mzawa mwenye mkataba wa thamani kubwa zaidi.

Kiungo huyo anayechezea timu ya Taifa ya Tanzania amekubaliana na Azam FC kuongeza mkataba wa mwaka mmoja utakaomfanya asalie klabuni hapo hadi 2027.

Mkataba wa awali wa Fei Toto na Azam FC ulikuwa ufikie tamati baada ya kumalizika kwa msimu wa 2025/2026 lakini kiungo huyo ataendelea kuwepo kwa mwaka mmoja zaidi.

Habari za uhakika ambazo Mwananchi Digital inazo ni kuwa katika mkataba huo mpya, Azam FC imepanga kumlipa Fei Toto kiasi cha Dola 200,000 (Sh520 milioni) kama ada ya mchezaji huyo kusaini mkataba mpya.

Azam FC pia imempa ongezeko la mshahara Fei Toto ambapo sasa itamlipa kiasi cha Sh80 milioni kwa mwezi ambacho kinamfanya kwa mwaka apokee kitita cha Sh960 milioni.

Hata hivyo mshahara huo ni kabla ya kukatwa kodi lakini fungu atakalobaki nalo mkononi kila mwezi baada ya kodi na makato mengine ni Sh50 milioni na kwa mwaka atapata kiasi cha Sh600 milioni.

Kiujumla kwa mwaka mmoja alioongeza, Feisal atavuna kitita cha Sh1.1 bilioni) baada ya makato ya kodi.

Inaripotiwa pia Fei Toto atapewa udhamini wa matangazo wa miongoni mwa kampuni zilizo chini ya Azam.

Hapana shaka kuongeza mkataba kwa Fei Toto kunazikata rasmi maini Yanga na Simba ambazo zilikuwa zikimuwania kwa udi na uvumba katika dirisha hili kubwa la usajili linaloendelea.

Kiwango bora ambacho Fei Toto amekionyesha akiwa na jezi ya Azam katika misimu miwili iliyopita kimemfanya awe miongoni mwa nyota lulu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Msimu wa 2023/2024, kiungo huyo alimaliza akiwa nafasi ya pili katika chati ya kufumania nyavu katika Ligi Kuu akipachika mabao 19 huku akipiga pasi za mwisho saba.

Katika msimu uliomalizika wa 2024/2025, Fei Toto alimaliza akiwa kinara wa kupiga pasi za mwisho kwenye Ligi akiwa nazo 13 na kufunga mabao manne.

Makali ya Fei Toto hayajaishia katika ngazi ya klabu kwani hata katika kikosi cha Taifa Stars amekuwa tegemeo na kwa kuthibitisha hilo, kiungo huyo alipewa tuzo ya Mchezaji Bora wa mechi katika mchezo wa ufunguzi wa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024 dhidi ya Burkina Faso.

Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' amesema kuwa uamuzi wa kumuongezea mkataba Fei umechangiwa na mchango mkubwa ambao amekuwa akiwapa.

"Kwanza Fei alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na sisi hivyo kwa kuongeza mmoja maana yake ana miwili ya kuichezea Azam FC. Ni mchezaji mzuri na ndio maana tumeona haja ya kuendelea naye," amesema Popat.