Fabrice Ngoma aaga Simba, akiwataja MO Dewji, Fadlu

Muktasari:
- Kabla ya kuitumikia Simba, Ngoma amewahi kuzichezea Raj Casablanca ya Morocco na AS Vita Club ya DR Congo.
Dar es Salaam. Kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma ametangaza kuondoka ndani ya timu hiyo ikionekana mpango wa kuongeza mkataba mpya umeshindikana.

Ngoma aliyejiunga na Simba, Julai 2023 akitokea Al Hilal ya Sudan, mkataba wake unafikia tamati mwezi ujao na ametumia ukurasa wake wa Instagram kuiaga Simba.
“Nachukua muda huu kumshukuru kila mmoja aliyefanya nijisikie nipo nyumbani hapa Simba. Asante kwa Salim Try Again na Bosi Mo walionileta hapa miaka miwili iliyopita.
“Asante kwa kocha, mastafu na wachezaji ambao nilichangia nao chumba cha kubadilishia nguo pamoja. Hatukuweza kufikia baadhi ya malengo yetu lakini kumbukumbu zote zitabaki mileleni akilini na moyoni mwangu.
“Kwenu mashabiki wa Simba, asanteni kwa sapoti yenu. Msiiangushe klabu, nyakati nzuri zinakuja hasa kwa kocha kama Fadlu,” ameandika Ngoma.

Mchezaji huyo inaripotiwa kwamba ana ofa kadhaa kutoka baadhi ya timu za Morocco na Libya.
Ngoma amekuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Simba aliyetoa mchango mkubwa kuiwezesha timu hiyo kutinga hatua ya Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2024/2025.

Wakati msimu ukielekea ukingoni, uongozi wa Simba ulifanya naye mazungumzo kwa ajili ya mkataba mpya ambayo yameshindwa kuzaa muafaka baina ya pande hizo mbili.
Habari za uhakika ambazo Mwananchi Digita inazo ni kwamba Simba inataka kumpa mchezaji huyo mkataba wa mwaka mmoja huku mchezaji mwenyewe akihitaji mkataba wa miaka miwili.