Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

El Classico yaziwahi Liverpool, Arsenal

Barcelona/Liverpool. Mechi mbili za kibabe zinapigwa leo katika ligi mbili kubwa duniani zikihusisha miamba minne ya soka, moja ikizikutanisha Barcelona dhidi ya Real Madrid na nyingine ikiwa baina ya Liverpool na Arsenal.

Hata hivyo kati ya mechi hizo mbili, ule unaozikutanisha Barcelona na Real Madrid maarufu kwa jina la El Classico ndio unaonekana utateka hisia za kundi kubwa la mashabiki wa soka duniani kulinganisha na mechi baina ya Liverpool na Arsenal.

Mchezo huo wa El Classico ambao utaanza mapema saa 11:15 jioni katika Uwanja wa Olímpic Lluís Companys una nafasi kubwa ya kuamua mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Hispania 'La Liga' msimu huu kama zitawahi au zitachelewa kumalizika.

Barcelona inayoongoza msimamo wa La Liga ikiwa na pointi 79, ikiibuka na ushindi katika mechi hiyo ya nyumbani leo, itajiweka karibu na ubingwa wa ligi hiyo msimu huu kwani itafikisha pointi 82 na hivyo itahitaji ushindi katika mechi moja tu kati ya tatu itakazobakiza ili itwae ubingwa.

Real Madrid inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 75, ushindi katika mechi ya leo itapunguza pengo la pointi baina yake na Barcelona kubakia moja na hivyo itaweka hai matumaini yake ya kutwaa taji hilo msimu huu baada ya kukosa mataji matatu msimu huu.

Timu hiyo imekosa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, taji la Copa Del Ray na lingine ni Super Cup.

Jambo la kuumiza zaidi kwa Real Madrid ni kwamba mataji mawili kati ya hayo matatu, iliyakosa kwa kufungwa na Barcelona katika fainali.

Kwa upande mwingine, mchezo huo wa leo ni fursa nzuri kwa Real Madrid kutokubali unyonge wa moja kwa moja dhidi ya Barcelona msimu huu kwani tayari imeshawafunga katika mechi nne zilizopita za mashindano tofauti, moja ikiwa ya La Liga na mbili zikiwa za Copa Del Ray na Super Cup.

Katika mechi tano zilizopita hivi karibuni za mashindano tofauti, Barcelona imepata ushindi mara tatu, kutoka sare moja na kupoteza mchezo mmoja wakati huo Real Madrid ikiwa imepata ushindi mara tatu na kupoteza michezo miwili.

Meneja wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema kuwa timu yake inahitajika kupata ushindi katika mechi hiyo lakini itapaswa kutoweka akilini matokeo ya kupoteza mechi iliyopita baina yao kwa mabao 3-2.

"Tutakuwa na nafasi nzuri, lazima tujiandae vyema kwa kiasi kikubwa ni mechi ya maamuzi. Mechi ya mwisho ilikuwa ya ushindani, tulikaribia sana kushinda na sidhani kama tunapaswa kubuni mambo mengi mapya (kimbinu)," alisema Ancelotti.

Meneja wa Barcelona, Hans Flick amesema kuwa kitendo cha timu yake kutolewa na Inter Milan kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kimewapa chachu ya kupambana kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi hiyo.

"Tunatakiwa tuendelee na maisha na tunatakiwa tupate ushindi. Kupoteza (dhidi ya Inter) kunatakiwa kuamsha njaa yetu ya kushinda taji. Hilo ndilo la muhimu kwangu," alisema Flick.

Wachezaji Inigo Martinez, Pablo Torre, Jules Kounde, Dani Rodriguez na Marc Bernal wa Barcelona watakosekana kwa sababu ya kuuguza majeraha.

Upande wa Real Madrid, Antonio  Rudiger hatokuwepo kwa sababu anatumikia adhabu wakati huo akiuguza goti na wengine watakaokosekana ambao ni majeruhi ni David Alaba, Eduardo Camavinga, Eder Militao  na Dani Carvajal.

Refa wa kati wa mchezo huo ni Alejandro Hernandez ambaye atasaidiwa na Jose Naranjo na Marcos Cerdan huku refa wa akiba akiwa ni Jose Pardeiro.

Liverpool, Arsenal kusaka heshima

Kwenye Uwanja wa Anfield, wenyeji Liverpool wakiwa tayari wameshatwaa taji la Ligi Kuu England (EPL) msimu huu wataikaribisha Arsenal.

Hakutakuwa na cha kupoteza kwa Liverpool kwenye mchezo huo na kikubwa ambacho inakihitaji ni kuweka heshima nyumbani kwa kutopoteza mbele ya mashabiki wake dhidi ya Arsenal ambayo inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa EPL ikiwa na pointi 67.

Arsenal ndio inahitaji kwa udi na uvumba matokeo mazuri kwenye mechi hiyo ili ifikishe pointi 70 ambazo zitaiweka katika nafasi nzuri ya kumaliza ikiwa katika nafasi iliyopo lakini pia iweze kujihakikishia kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Mchezo wa mzunguko wa kwanza wa EPL msimu huu baina ya timu hizo ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2, ambapo mabao ya Arsenal yalipachikwa na Bukayo Saka na Mikel Merino huku yale ya Liverpool yakifungwa na Virgil van Dijk na Mohamed Salah.

Arsenal wamekuwa na ubabe dhidi ya Liverpool hivi karibuni ambapo hawajapoteza katika mechi tano zilizopita za EPL baina yao.

Salah amekuwa mchezaji tishio kwenye kikosi cha Liverpool msimu huu ambapo ndiye mfungaji bora wao akiwa na mabao 28, ambayo ni zaidi ya mchezaji yeyote mpinzani kwenye ligi msimu wa 2024/2025.

Wenyeji Liverpool wamekuwa na ubabe Anfield msimu huu ambako wameshinda mara 14, sare mbili, na kupoteza moja pekee katika mechi 17 walizocheza hapo za ligi.

Liverpool wanatazamia kuendeleza rekodi yao ya kupata ushindi katika mechi 15 mfululizo za Ligi Kuu bila kupoteza tangu Septemba 2024 walipofungwa bao 1-0 na Nottingham Forest.