Dube aachia barua ya kuaga Azam

Muktasari:
- Kupitia akaunti yake ya Instagram, Dube ameposti barua yenye ujumbe wa kuishukuru klabu hiyo akionyesha kuwa ndiyo basi, hataki kubaki tena kwenye timu hiyo
Baada ya jana mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube kufuta picha zote alizopiga akiwa na jezi za timu hiyo, leo ameendeleza kuonyesha umwamba wake pamoja na kwamba bado ana mkataba wa miaka miwili na timu hiyo.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Dube ameposti barua yenye ujumbe wa kuishukuru klabu hiyo akionyesha kuwa ndiyo basi, hataki kubaki tena kwenye timu hiyo, akisema:
“Nikiwa katika hisia mchanganyiko natangaza kuondoka katika klabu ya Azam. Safari ya miaka minne kwangu ilikuwa nzuri sana iliyojaa ushindi, changamoto, furaha.”
“Nawashukuru wote kwenye klabu hii kuanzia uongozi, benchi la ufundi, wachezaji wenzangu na kwa upekee zaidi mashabiki.
“Ninavyoondoka kwenda kufungua ukurasa mwingine wa maisha yangu ya soka, naondoka na mafunzo yote mema niliyoyapata hapa na siku zote nitatangaza mazuri yote tuliyoyapata pamoja.
“Nina imani na uwezo mkubwa wa timu hii, naamini itaendelea kufanya vizuri na kufikia malengo, nawatakia kila la kheri na asanteni.”
Dube aliandika barua ya kuonyesha anaondoka Azam na kupewa masharti ya kufuata utaratibu wa kuvunja mkataba, licha ya kuwa hakuweza kuyafuata.
Ili kuvunja mkataba Dube, anatakiwa kuilipa Azam dola 300,000 zaidi ya sh 750 milioni, ambapo taarifa zinadai kuwa nyota huyo alipeleka nusu ya pesa na Azam walizikataa kwani anatakiwa kulipa zote kwa wakati mmoja.
Inaonekana njia anazopita Dube ni sawa na zile ambazo Feisal Salum 'Fei Toto' alizitumia kuondoka Yanga.