Crystal Palace yaichapa Liverpool ufunguzi msimu mpya EPL
Muktasari:
- Mchezo wa Ngao ya Jamii England hukutanisha timu bingwa wa Ligi Kuu England (EPL) na timu bingwa wa Kombe la FA England.
London, England. Liverpool imeanza msimu kwa kushindwa kutwaa taji la kwanza baada ya leo Jumapili, Agosti 10, 2025 kupokea kichapo cha mikwaju ya penalti 3-2 kutoka kwa Crystal Palace katika mechi ya Ngao ya Jamii iliyochezwa kwenye Uwanja wa Wembley, London, England.
Matokeo hayo yameifanya Crystal Palace kutwaa taji la Ngao ya Jamii ambalo msimu uliopita lilichukuliwa na Manchester City.
Licha ya Liverpool kutangulia kufunga mara mbili, safu yake ya ulinzi haikuwa makini katika kujilinda na kuiruhusu Crystal Palace kusawazisha mabao yote mawili na kulazimisha mshindi wa mchezo huo kuamriwa kwa mikwaju ya penalti ndipo Liverpool ikapoteza.
Kabla ya mikwaju ya penalti, Liverpool ilitangulia kufunga katika dakika ya nne kupitia kwa Hugo Ekitite akimalizia pasi ya Florian Wirtz.
Dakika ya 17, Jean Mateta aliisawazishia Crystal Palace kwa mkwaju wa penalti lakini bao hilo lilidumu kwa dakika nne tu kwani Jeremie Frimpong aliifungia Liverpool bao la pili katika dakika ya 21.
Zikiwa zimebaki dakika 13 mechi hiyo Ismaila Sarr aliifungia Crystal Palace bao la kusawazisha akimalizia pasi ya Adam Wharton.
Hadi refa Chris Kavanagh anapuliza filimbi ya kumaliza dakika 90, hakukuwa na mbabe baina ya timu hizo jambi ambalo lililazimu mikwaju ya penalti kutumika kusaka mshindi.
Crystal Palace imefunga penalti zake tatu kupitia kwa Jean Mateta, Sarr na Justin Devenny huku Eberechi Eze na Borna Sosa wakikosa.
Liverpool ilifunga penalti zake mbili kupitia kwa Cody Gakpo na Dominik Szoboszlai huku Mohamed Salah, Alexis MacAllister na Harvey Elliot wakikosa.
Hiyo imekuwa mara ya kwanza kwa Crystal Palace kutwaa taji la Ngao ya Jamii wakati Liverpool imeshindwa kulitwaa kwa mara ya tano.
Manchester United ndio timu kinara kwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii ambapo imefanya hivyo mara 12 ikifuatiwa na Arsenal iliyotwaa mara tisa.