Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Crystal Palace kufungiwa Europa, Nottingham na Brighton kufaidika

Muktasari:

  • UEFA haiko tayari kuruhusu udhibiti wa vilabu viwili au zaidi kushiriki michuano ya bara hilo vikiwa chini ya mmiliki mmoja.

Katika kile kinachoonekana kama pigo kubwa kwa Crystal Palace ni Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) limeshafanya uamuzi wa kufungia klabu hiyo kushiriki michuano ya Europa League msimu wa 2025/26, kutokana na kukiuka kanuni za umiliki wa vilabu zaidi ya kimoja. Taarifa hizo zimeibuka kufuatia mkutano wa dharura uliofanyika Jumanne, Juni 3 kati ya viongozi wa Crystal Palace na maafisa wa UEFA huko Nyon, Uswisi.

Chanzo kikuu cha mgogoro huu ni mmiliki mwenza wa Crystal Palace, John Textor, ambaye anamiliki asilimia 43 ya hisa za klabu hiyo ya London, huku pia akiwa na hisa katika klabu ya Lyon ya Ufaransa ambayo nayo imefuzu kushiriki Europa League msimu ujao.

UEFA inalinda sana uadilifu wa michuano yake, na ina kanuni madhubuti zinazokataza mtu mmoja kuwa na ushawishi au usimamizi wowote wa vilabu viwili au zaidi vinavyoshiriki michuano hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na The Guardian, juhudi za Textor na mwekezaji mwingine wa Palace, David Blitzer, kuweka hisa zao kwenye blind trust ambao ni mfumo wa muda wa kujitenga na ushawishi wa moja kwa moja zimekataliwa na UEFA. Lengo la hatua hiyo lilikuwa kuhakikisha Palace inaruhusiwa kushiriki michuano hiyo, lakini UEFA imekataa kwa sababu klabu hiyo haikufanya hivyo tarehe ya mwisho ya kuwasilisha mpango huo ambayo ilikuwa ni Machi 1.

David Blitzer pia anamiliki sehemu kubwa ya klabu ya Brondby ya Denmark, ambayo nayo itashiriki mashindano ya UEFA, jambo linaloongeza ugumu wa kuwaruhusu Palace kubaki kwenye Europa League. Mbaya zaidi, hata wazo la Palace kushushwa hadi UEFA Conference League halitekelezeki, hivyo kuiweka Cystal Palace kwenye mashindano yoyote ya UEFA kunakiuka kanuni za msingi za shirikisho hilo.

Hali hii imewapa nafasi ya kipekee Nottingham Forest, ambao sasa wanatarajiwa kupandishwa kutoka UEFA Conference League hadi Europa League, ikiwa Palace wataondolewa rasmi. Kwa upande mwingine, Brighton waliomaliza nafasi ya nane kwenye Ligi Kuu ya England msimu uliopita, wanatarajiwa kuchukua nafasi ya Palace kwenye UEFA Conference League.

Katika mazungumzo yake na The Mail, Textor alikiri kuwa yuko tayari kuuza hisa zake ili kulinda maslahi ya klabu, lakini inavyoonekana muda umeshapita na UEFA haitarajii kubadilisha msimamo wake.

“Nilichokuwa nikijaribu ni kulinda ndoto ya wachezaji wetu na mashabiki, lakini kama UEFA haitaki kusikia mpango wetu wa blind trust, basi huenda nikauza hisa zangu,” amesema Textor.

Mara ya mwisho, vilabu vya Manchester City na Manchester United vilifanikiwa kutumia njia ya blind trust ili kutatua matatizo ya aina hiyo, lakini waliwasilisha mipango hiyo mapema, kabla ya tarehe ya mwisho. Crystal Palace wameshindwa kufuata utaratibu huo kwa wakati, hali inayoonesha uzembe wa kiuongozi.

Tukio hili linatoa ujumbe mzito kwa vilabu vyote barani Ulaya kuwa UEFA haiko tayari kuruhusu udhibiti wa vilabu viwili au zaidi kushiriki michuano ya bara hilo vikiwa chini ya mmiliki mmoja.

Kwa sasa, mashabiki wa Crystal Palace watalazimika kusubiri msimu mwingine kuona timu yao ikirudi kwenye michuano ya Ulaya, huku Nottingham Forest na Brighton wakifaidika kwa kiasi kikubwa na sakata hili la kiutawala ambalo linawaumiza Crystal Palace.