Chelsea yaitandika PSG ikitwaa Kombe la Dunia
Muktasari:
- Chelsea imefunga bao katika kila mechi ya Kombe la Dunia la Klabu ambapo imecheza idadi ya michezo saba.
Cole Palmer amekuwa shujaa wa Chelsea baada ya kuiongoza timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya PSG katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia la Klabu uliochezwa kwenye Uwanja wa Metlife, New Jersey.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23, amefunga mabao mawili na kupiga pasi moja ya mwisho na kuiwezesha Chelsea kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.
Palmer amefunga bao la kwanza katika dakika ya 22 akimalizia pasi ya Mało Gusto na dakika nane baadaye akatumia vyema pasi ya Levi Colwill kuifungia Chelsea bao la pili.
Wakati PSG wakipambana kupata angalau bao moja kabla ya mapumziko, Palmer alipiga pasi ya mwisho iliyotumiwa vyema na Joao Pedro kuipatia Chelsea bao la tatu na lililoihakikishia taji la mashindano hayo.
Hilo ni taji la pili kwa Chelsea msimu huu baada ya kufanikiwa kuchukua Kombe la UEFA Conference.
Katika mechi hiyo, PSG ilijikuta ikimaliza ikiwa pungufu kufuatia kiungo Joao Neves kuonyeshwa kadi nyekundu na Refa Alireza Faghani katika dakika ya 84 baada ya kumvuta nywele Marc Cucurella.
Kwa kutwaa ubingwa wa mashindano hayo, Chelsea imejihakikishia zawadi ya fedha kiasi cha Pauni 29 milioni (Sh102 bilioni).
PSG kwa kumaliza katika nafasi ya pili, imejihakikishia kupata kifuta jasho cha Pauni 21.8 milioni.
Kichapo hicho kwa upande mwingine kimeifanya PSG ishindwe kuandika rekodi ya kutwaa mataji matano msimu huu baada ya kufanikiwa kuchukua Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Ufaransa, Kombe la Ufaransa na Kombe la Washindi Ufaransa.