Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Haaland, Mourinho wanavyochochea vita ya urais Real Madrid

Muktasari:

  • Mgombea urais, Enrique Riquelme ameonekana akiwa ameshikilia jezi ya Real Madrid yenye jina la Haaland mgongoni, akiahidi kumleta mshambuliaji huyo Santiago Bernabeu.

Madrid, Hispania. Kampeni za uchaguzi wa urais wa klabu ya Real Madrid zimezidi kupamba moto baada ya mgombea wa nafasi hiyo, Enrique Riquelme, kuahidi kuwa atamsajili mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland, iwapo atashinda uchaguzi dhidi ya rais wa sasa, Florentino Perez.

Riquelme, ambaye anampinga Perez mwenye umri wa miaka 79, ameonekana kwenye kipindi cha televisheni akiwa ameshikilia jezi ya Real Madrid yenye jina la Haaland mgongoni, akiahidi kumleta mshambuliaji huyo Santiago Bernabeu.

Hatua hiyo imezua hasira kwa Manchester City, ambao wamekanusha vikali uwezekano wa mchezaji huyo kuhamia Real Madrid na kutangaza kuwa wanatafakari kuchukua hatua za kisheria.

“Habari zilizoibuka nchini Hispania kuhusu mustakabali wa Erling Haaland si za kweli. Hakuna uwezekano wa jambo hilo kutokea na hakuna kipengele chochote kwenye mkataba wake kinachoruhusu hali hiyo. Tunazingatia kuchukua hatua za kisheria kutokana na matumizi ya picha ya mchezaji wetu katika mazingira haya,” imesema taarifa ya klabu hiyo.

Mgombea urais wa Real Madrid, Florentino Perez (kushoto), akiwa na kocha wa zamani wa timu hiyo Jose Mourinho. Picha na Mtandao

Wakati huo huo, Perez ameanza kutumia jina la Jose Mourinho kama sehemu ya kampeni zake za kuwania muhula mwingine wa urais.

Ingawa kurejea kwa Mourinho Bernabeu bado hakujatangazwa rasmi, kurasa rasmi za kampeni za Perez zimechapisha video iliyomwonyesha kocha huyo wa zamani wa Real Madrid akiwa mbele ya kamera akisema kwa Kihispania neno “ndiyo”, huku video hiyo ikiambatana na ujumbe uliosomeka: “Historia nyingi bado zinapaswa kuandikwa.”

Mourinho, mwenye umri wa miaka 63, anatajwa kuwa amekubali kusaini mkataba wa kuinoa Madrid hadi mwaka 2028, ukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.

Kocha wa zamani wa Real Madrid, Jose Mourinho. Picha na Mtandao

Kocha huyo wa zamani wa Chelsea, Manchester United na Tottenham anatarajiwa kurejea katika klabu inayokabiliwa na changamoto mbalimbali baada ya msimu uliogubikwa na migogoro ya ndani ya wachezaji, kutolewa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kushuhudia Barcelona ikitwaa ubingwa wa LaLiga.

Perez pia ameahidi kutangaza usajili wake mkubwa wa kwanza katika siku zijazo, huku mabeki Ibrahima Konate wa Liverpool na Denzel Dumfries wakitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa kutua Bernabeu.

Mgombea urais wa Real Madrid, Enrique Riquelme wakati alipokuwa kwenye kipindi cha televisheni akiwa ameshikilia jezi ya Madrid yenye jina la Haaland mgongoni. Picha na Mtandao

Hata hivyo, Riquelme amesema hatamteua Mourinho iwapo atashinda uchaguzi huo.

“Kama nitashinda uchaguzi, nitamleta Real Madrid kocha mkubwa zaidi. Jose Mourinho si chaguo letu. Tutamleta kocha ambaye mashabiki wa Real Madrid wanamtaka kweli,” amesema Riquelme.

Mbali na Haaland, mgombea huyo pia ameahidi kumsajili kiungo wa Man City na timu ya taifa ya Hispania, Rodri, huku akipanga kumteua nguli wa klabu hiyo, Raul Gonzalez, kuwa mkurugenzi wa michezo.

Aliyekuwa beki wa Liverpool, Ibrahima Konate. Picha na Mtandao

Licha ya ahadi hizo, Perez anaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuendelea kubaki madarakani kutokana na ushawishi wake mkubwa ndani ya klabu hiyo, ambapo hajawahi kupata mpinzani katika chaguzi tano zilizopita.

Kwa upande mwingine, beki wa Liverpool, Ibrahima Konate, tayari amethibitisha kuondoka Anfield baada ya mazungumzo ya kuongeza mkataba wake kuvunjika, hatua inayomfanya kuwa karibu zaidi na kujiunga na Real Madrid.