Prime
MZEE WA FACT: Pérez kama Wassira, yupo na atakuwepo tu!
Mwaka 1998, Real Madrid ikiwa chini ya uongozi wa Rais Lorenzo Sanz, ilishinda ubingwa wa kwanza wa Ulaya baada ya miaka 32.
Waliifunga Juventus kwa bao 1-0 na kukata kiu cha muda mrefu. Nahodha wa klabu hiyo wa wakati huo, Manolo Sanchis, alisema ushindi huu ulikuwa muhimu zaidi katika historia ya klabu yao.
Ubingwa huu ni kama ukarudisha urafiki wao na makombe la Ulaya kwani miaka miwili baadaye, 2000, wakashinda ubingwa mwingine wa Ulaya kwa ushindi mnono wa 3-0 dhidi ya Valencia.
Mashabiki wote wa Real Madrid walikuwa na furaha kubwa na mafanikio ya klabu yao, kasoro shabiki mmoja aliyeitwa Florentino Pérez.
Yeye hakuangalia tu makombe ya Ulaya ambayo yaliitesa klabu yao kwa mida mrefu, bali klabu yenyewe kwa ujumla.
Akasema klabu yao inapitia kipindi kibaya kiuchumi huku ikielemewa na madeni makubwa
Pérez akayachambua matatizo ya kiuchumi ya Real Madrid na kusema klabu yao inahitaji usimamizi mzuri zaidi wa kiuchumi.
Akaenda mbali na kusema watu wasihadaike na mataji ya Ulaya kwani mashindano ya ndani pia ni muhimu lakini klabu haifanyi vizuri.
Baada ya kusema haya, akatangaza kugombea urais kupitia uchaguzi wa Julai 2000.
Katika kampeni zake akaahidi akichaguliwa atakuja na sera ya GALACTICOS yaani atasajili wachezaji nyota watupu.
Akasema ataanza na Luis Figo, nyota wa FC Barcelona, ambaye mashabiki wa Real Madrid walikuwa wakimuota. Perez hakuahidi hivi hivi tu ili kufurahisha genge.
Alikuwa aafahamiana na wawakilishi wa Figo na katika mazungumzo yao ya kawaida, akawaambia atagombea urais wa Real Madrid, na atashinda.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez (katikati), wakati akitia saini zawadi ya jezi kwa Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino. Picha na Mtandao
Jamaa wakambishia, basi akawaambia kama hawaamini waweke dau...kwamba akishinda atamsajili Figo, akishindwa atawalipa pesa nyingi...wakaandikishiana ili mambo yawe kwa ushahidi.
Basi yeye akayatumia yale makubaliano katika kampeni na mashabiki wakamuelewa.
Akawahidi kwamba endapo hatomsajili Figo basi atawalipia ada ya mwaka wanachama wote wenye tiketi za msimu mzima wa klabu hiyo.
Perez akashinda uchaguzi na wawakilishi wa Figo wakawa hawana namna...Figo akajiunga na Real Madrid na ndio ukawa mwanzo wa GALACTICOS.
Akaja Zidane, akaja Ronaldo de Lima, akaja Beckham...mambo yawa mambo.
Julai mwaka huu, 2026, itatimia miaka 26 tangu haya yatokee.
Katika miaka hii, Perez ameiongoza Real Madrid katika vipindi viwili.
2000 hadi 2006 alipojiuzulu.2009 akarudi tena, na ndio bado yupo hadi sasa.
Katika utawala wake, Perez ameisaidia Real Madrid kama klabu kushinda mataji 66, yakiwemo 37 kwenye mpira wa miguu, na mengine 29 kwenye mpira wa kikapu.
Rais wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), Aleksander Čeferin (kushoto), akiwa na Rais wa Real Madrid, Florentino Perez. Picha na Mtandao
Mpira wa miguu
Ubingww wa Ulaya - 7
Klabu Bingwa ya Dunia- 7
Ngao ya Jamii ya Ulaya - 6,
La Liga - 7
Kombe la.Mfalme - 3
Ngao ya Jamii ya Hispania -
Mpira wa kikapu
Ubingwa wa Ulaya - 3
Kombe la Mabara - 1
La Liga - 9 ,
Kombe la Mfalme - 7
Ngao ya Jamii ya Hispania- 9
Mafanikio haya ya uwanjani na ukichanganya na ya nje ya uwanja kama hali nzuri ya kiuchumi ya klabu na ujenzi wa uwanja wa kisasa wa Santiago Bernabeu na mji wa starehe ya michezo wa Real Madrid City, bado Perez anakabiliwa na upinzani kutoka kwa mashabiki.
Hawafurahii klabu yao kukosa mataji makubwa, ya ndani ya kimataifa kwa msimu wa pili sasa.
Mwaka jana, 2025, Real Madrid ilifanya uchaguzi mkuu na Perez akapita bila kupingwa...lakini mwaka huu presha imekuwa kubwa na Real Madrid itafanya tena uchaguzi.
Uchaguzi huu unakuja baada ya presha kumzidi Perez hadi kuitisha kura imani kwa Rais, lakini tume ya uchaguzi ya klabu hiyo ikaona bora ufanyike uchaguzi kamili badala ya kura za imani kwa Rais.
Pérez ametangaza kwamba atagombea uchaguzi huu, na kama ilivyo demokrasia, na wengine wanakaribishwa.
Hata hivyo, kuna asilimia kubwa Perez kupita bila kupingwa kama ilivyokuwa mwaka jana na miaka mingine mingi nyuma, sio tu kwa sababu anapendwa sana...bali masharti ya uchaguzi.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez. Picha na Mtandao
Masharti
1. Uwe raia wa Hispania
2. Uwe na kadi hai ya uanachama ya Real Madrid kwa angalau miaka 20 mfululizo
3. Uwasilishe dhamana ya benki yenye thamani ya asilimia 15 ya bajeti ya mwaka ya Real Madrid. Bajeti ya mwaka ya Real Madrid ni Euro 187,200,000...sawa na shilingi za Tanzania bilioni 568,788,4000.
4. Upitie mchujo wa ndani wa kura za maoni za wanachama.
5. Usiwe sehemu ya uwekezaji wowote wa kutoka nje ya Hispania.
Masharti haya ni magumu na hakuna anayeweza kuyafikia.
Ukiwa raia wa Hispania na kufuzu sharti namba moja, na kisha kuwa na kadi hai ya miaka 20 na kufuzu sharti namba mbili, unaweza kukwama sharti namba tatu.
Dhamana ya asilimia 15 ya bajeti ya Real Madrid ni nyingi sana.
Wanaoweza kuwa na hela nyingi kiasi hiki ni wafanyabiashara wakubwa, ambao wakijitokeza ni lazima watakwama kwenye sharti namba tano, ambalo linakataza mgombea kuwa na hisa kwenye kampuni za kutoka nje.
Wafanyabiashara wakubwa wenye uwezo wa kuwa na fedha za kukidhi sharti la tatu ni wale wa kimataifa ambao mtaji wao una hisa nyingi katika makampuni ya nje.
Kwa vyovyote vile, Perez ataendelea kuwepo tu kama Wassira, kwa sababu atapita tena bila kupingwa.