Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CHAN imeonesha rangi halisi ya Watanzania

Mechi za Yanga na Simba kwenye mashindano ya CAF ziliidanganya Afrika kwamba Tanzania kuna wendawazimu wa mpira.

Picha za majukwaa ya Benjamin Mkapa yakiwa yamefurika mashabiki zikaipamba mitandao ya kijamii barani Afrika. Waandishi kutoka nchi mbalimbali wakaripoti habari hii njema na kuiweka juu Tanzania kama moja ya nchi zenye mapenzi yaliyopitiliza ya soka.

Lakini mashindano ya CHAN yanayoendelea Afrika Mashariki yametoa picha tofauti kabisa na hii ndio picha halisi ya ushabiki wa soka hapa nchini.

Hakuna mahudhurio mazuri kwenye mechi zinazofanyika Tanzania, hata Taifa Stars inapocheza. Wenzetu Kenya na Uganda wametuacha mbali sana, tena sana.

Mechi ambazo hazihusishi mataifa yao zinapata watazamaji wengi tofauti na sisi. Mechi ambazo Taifa Stars haichezi hazipati watu kabisa pale Kwa Mkapa. Jibu ni moja tu kwamba Tanzania hakuna mashabiki halisi wa mpira bali kuna mashabiki wa Simba na Yanga.

Mechi zinazoihusu Taifa Stars hazipati watu wengi kama ambavyo huwa kwa Yanga na Simba. Kwa sababu Yanga na Simba ndio timu zao, sio timu ya taifa. Machi 4, 2022 Simba waliwakaribisha US Gendermarie ya Niger katika mchezo uliofanyika saa 4 usiku.

Huwezi kuamini, uwanja ulijaa wote bila kujali ni usiku sana na nafasi ndogo ya Simba kufuzu robo fainali. Simba iliingia kwenye mchezo huu ikiwa ya tatu kwenye msimamo, nyuma ya Asec na Berkane lakini watu waliijaa.

Hofu ilikuwa kubwa sana kwamba watu wasingejitokeza kwa sababu ni usiku sana, na usafiri wa Dar es Salaam ni shida sana usiku lakini walijaa.

Novemba 17, 2020, Taifa Stars ilicheza na Tunisia, mchezo wa kufuzu AFCON mechi ilianza saa nne usiku hakukuwa na watu wengi uwanjani. Sababu eti ni usiku sana.

Lakini tatizo halikuwa usiku hata mechi ya mchana za Taifa Stars huwa hazipati watu wengi. Kwenye hii CHAN, Taifa Stars ndio timu inayocheza vizuri zaidi na kushinda zaidi kati ya timu zote za wenyeji.

Uganda walianza kwa kipigo cha 3-0, Kenya walishinda 1-0 dhidi ya DRC lakini kwa kiwango hafifu sana. Lakini mechi ziliizofuata watu walijaa uwanjani utadhani timu zao ziliwapa uhakika wa asilimia 100 kwamba zitashinda.

Lakini hii haikuwa kwa Tanzania. Ilianza kwa ushindi mnono wa 2-0 na mpira mkubwa sana lakini mechi iliyofuata, watu walikuwa wachache kuliko mechi ya kwanza. Jibu hapa ni moja tu kwamba Tanzania hatuna ushabiki wa mpira bali wa Simba na Yanga.

Tusijilinganishe tena na nchi zingine linapokuja suala la ushabiki wa mpira sisi hatupendi mpira kama mpira.


NINI CHA KUFANYA

Kuna kitu kikubwa sana cha kufanya ili kubadiisha akili za watanzania la sivyo hatutostahili tena kuandaa mashindano yoyote makubwa ya kimataifa.


1. TUACHE UPENDELEO

Yanga na Simba zinapata upendeleo mkubwa sana kutoka mamlaka zote, za kimpira na hata za kiserikali.

Mamlaka za mpira zinapopanga ratiba ya mechi za ligi kuu kuchezwa hadi saa nane mchana, Yanga na Simba hawaguswi na hilo...hupendelewa waziwazi.

Na hilo ni moja kati ya mengi ambayo timu hizi hufaidika nayo kutokana na kuandaliwa mazingira bora na mamlaka za mpira.

Lakini pia mamlaka za kiserikali nazo ziko mstari wa mbele sana kuzisaidia Yanga na Simba.

Rejea sakata la HATUCHEZI, rais wa nchi aliingia kati kuepusha panga na kisheria kuwakuta Yanga endapo wasingecheza Juni 15.

Ile isingetokea kwa timu nyingine nje ya hizi mbili.


2. TIMU ZINGINE ZIIMARIKE

Inasikitisha sana kwamba kwa miaka 25 iliyopita, yaani kuanzia mwaka 2000, ni timu mbili zilifanikiwa kuwazuia Yanga na Simba kutwaa ubingwa wa ligi kuu.

Mtibwa Sugar mwaka 2000 na Azam FC mwaka 2014, lakini zaidi ya hapo ni aidha Yanga au Simba.

Na hata ukienda kwenye historia ya ligi kwa ujumla, ni wao tu.

Katika miaka 60 ya ligi, ni mara 8 tu hawa jamaa wakikosa ubingwa.

1967 - Cosmopolitan (Dar es Salaam)

1975 - Mseto (Morogoro)

1982 - Pan African (Dar es Salaam)

1986 - Tukuyu Stars (Mbeya)

1988 - Coastal Union (Tanga)

1999 - Mtibwa Sugar (Morogoro)

2000 - Mtibwa Sugar (Morogoro)

2014 - Azam FC (Dar es Salaam)

Ligi ya Tanzania ilianza 1965, hadi 2025 ni miaka 60, maana yake kunatakiwa kuwa na mabingwa 60.

Yanga na Simba wamekuwa mabingwa mara 52 huku wengine wakiwa mabingwa mara nane.

Hii imefanya Yanga na Simba kuzalisha mashabiki wengi zaidi kila mwaka na hao mashabiki kubaki na Simba na Yanga tu.

Kungekuwa na kunyang'anyana ubingwa mara kwa mara kwa timu mbalimbali, mashabiki wa timu hizi wasingejawa na kiburi kama walichonacho.


3. KUONGEZA UZALENDO

Uzalendo ni mapenzi mema aliyonayo raia kwa taifa lake.

Kulipenda taifa lako ni kuuvaa umiliki wa kila kitu kinacholihusu taifa lako; raslimali za taifa, alama za taifa, tunu za taifa na tamaduni za taifa.

Timu ya taifa ni moja ya alama na tunu za taifa...raia anatakiwa kuipenda bila masharti.

Lakini hii haipo kwa watanzania....hawana uzalendo wa kweli.

Ni kawaida kwa mtanzania kuharibu mali ya umma na mtu anamuona na hamkemei.

Mara ngapi watu huchimba mchanga pembeni ya barabara na kusababisha mmomonyoko unaosababisha barabara kubomoka?

Unadhani hajui kama anaharibu barabara? Na anafanyia hivyo hadharani na watu wanamuona....lakini hawamkatazi, unadhani nao hawajui?

Wote wanajua lakini wanaona kama barabara ni ya serikali, sio mali ya taifa.

Na hiyo ipo katika maeneo mengi sana ndio inaenda hadi kwenye timu ya taifa.

CHAN 2024 imetufundisha mengi sana!