Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chama angekuwepo angefanya kama Sadio Mane?

Muktasari:

Soma zaidi hapa...



Nyota wa Zambia kutoka mjini Ndola, Clatous Chama, amerejea kufanya kazi kwa mara ya tatu na klabu ya Simba.

Alijiunga na Simba mwaka 2018 na kuhudumu hadi 2021 alipohamia Berkane ya Morocco...kisha kurudi tena Simba dirisha dogo la 2022.

Mwaka 2024 akatimkia Yanga, halafu 2025 akajiunga na Singida Black Stars...na sasa amerejea Simba...ni hattrick!

Ahmed Ally, meneja habari wa Simba, amenukuliwa na kurasa rasmi za klabu hiyo akisema kwamba Chama amerudi Simba kufanya kazi kama ya Sadio Mane wa Senegal.

Itakumbukwa kwamba fainali ya AFCON 2025 ilikaribia kuharibu taswira ya mpira wa Afrika kufuatia kitendo cha Simba wa Teranga, timu ya taifa ya Senegal, kususia mchezo dakika za mwisho.

Ni bahati kwamba Senegal wanaye nyota mwenye ushawishi mkubwa kwa wenzake, Sadio Mane. Akatumia ushawishi wake kulegeza nyoyo za wenzake na hatimaye wakurudi uwanjani.

Kwa hiyo kwa mujibu wa Ahmed Ally, Simba ilikuwa inakosa mtu wa aina hii ndani ya kikosi chao, hivyo wamemrudisha ili kuwaongoza wenzake.

Ukurasa huu hauamini kama Simba wanakosa mtu mwenye ushawishi  ndani ya kikosi hicho kwa sababu kuna wachezaji waandamizi zaidi ya Chama, kama Shomary Kapombe.

Pia wakati wa Chama akiwa Simba katika awamu mbili za kwanza, walikuwa wakiishia robo fainali tu ya mashindano ya Afrika, alipoondoka wamefika fainali.

Kama Chama angekuwa na ushawishi mkubwa wa kuhamasisha wenzake kupambania timu na wakamtii, basi fainali wangeshafika zamani...hata ubingwa wangebeba.

Kwa sababu Simba yenye Chama iliyokuwa ikiishia robo fainali hadi kuitwa Mwakarobo, ilikuwa na kikosi bora kuliko kilichofika fainali ambacho hakikuwa na Chama.

Kilichopo hapa ni kwamba Simba kupitia Ahmed Ally wametafuta tu kichaka tu cha kujifichia kuepuka maneno ya kejeli kwani walipomuacha walisema hana kipya cha kuwapa...mdogo huo huo wa Ahmed Ally uliyatamka haya.

Kama ni kuwaongoza wenzake kama Sadio Mane, basi labda kama Simba wana mpango wa kususia mechi msimu huu, tabia waliyokuwa nayo zamani.

Na kama kufanya kama Sadio Mane, basi labda kama Chama angekuwepo Simba miaka ya hiyo na kuwashawishi wenzake warudi uwanjani na kuendelea na mchezo pale walipogoma.

Maana katika historia yake, Simba wa Msimbazi ameshafanya sana matukio kama ya Simba wa Teranga, tena yeye alienda mbali zaidi na kugoma kurudi uwanjani.

Simba wa Teranga walirudi uwanjani kwa sababu walikuwa na Mane, mtu ambaye Simba wa Msimbazi hawakuwa naye. Je wangerudi uwanjani endapo wangekuwa na Chama nyakati hizo?


LIGI YA BARA AGOSTI 10, 1985

Ilikuwa mechi ya mwisho ya msimu wa 1985 wa Ligi ya Bara, na Simba alitakiwa kumaliza na Yanga. Mechi hii ilifanana kidogo na ile ya msimu uliopita kwa sababu zote zilitakiwa kuamua bingwa.

Simba waliingia kwenye mchezo huo wakiwa nyuma kwa alama moja tu dhidi ya Yanga, hivyo endapo wangeshinda wangekuwa mabingwa.

Yanga walihitaji sare tu, wawe mabingwa. Baada ya sare ya 0-0 kipindi cha kwanza, Yanga wakapata penati kipindi cha pili baada ya beki wa Simba, Talib Hilary, kudaka mpira wa kona ndani ya eneo la hatari.

Sio tu kwamba aliunawa, hapana...aliudaka kama kipa. Baadaye akasema alisikia filimbi akadhani mwamuzi alisimamisha mchezo. Simba wakagomea penati hiyo na kutoka uwanjani...hawakurudi tena.

Kwa maelezo ya Ahmed Ally, Chama angekuwepo angevaa uhusika wa Clatous Chama na kuwashawishi uwanjanj.


LIGI YA MUUNGANO NOVEMBA 13, 1991

Kuanzia 1982 hadi 2003 kulikuwa na mashindano hapa Tanzania yaliyoitwa Ligi ya Muungano. Mashindano hayo yalikuwa muendelezo ya ligi ya Tanzania iliyoanza 1965 kwa jina la KLABU BINGWA YA TAIFA.

Kwa hiyo 1982 jina likabadilika kutoka Klabu Bingwa ya Taifa na kuwa Ligi Kuu ya Muungano. Kimsingi hii ndio ilikuwa ligi kuu ya Tanzania na ndio ilitoa wawakilishi wa nchi kwenye mashindano ya CAF.

Kwanza zilianza ligi za kila upande wa muungano, halafu timu bora zilizomaliza nafasi za juu (idadi ilitegemea mwaka)  kutoka kila upande wa muungano zilikutana kutafuta bingwa wa jumla wa nchi. Bingwa huyo ndio alitambuliwa na CAF na FIFA kama bingwa rasmi wa Tanzania.

Sasa mwaka 1991 mechi ya mzunguko wa pili ya ligi ya muungano kati ya Simba na Yanga ilivunjika baada ya kipindi kimoja tu.

Baada ya sare ya 0-0 kipindi cha kwanza, Simba hawakurudi kipindi cha pili wakimlalamikia mwamuzi Hafidh Ally (marehemu) kwamba amepanga kuwafungisha.

Simba walibaki kwenye vyumba vya kubadilishia nguo hadi giza likaingia na kumlazimu mwamuzi huyo kutoka Zanzibar ambaye ndio alikuwa bora zaidi Tanzania wakati ule, amalize mchezo.

Endapo Chama angekuwepo, labda angebeba majukumu ya Sadio Mane na kuwashawishi wenzake kama kipa Idd Pazi, kiungo fundi Method Mogella (marehemu) na wengine kurudi uwanjani.


LIGI YA BARA JULAI 10, 1999

Mwaka 1999 kwenye Ligi Kuu Bara lilizuka neno maarufu la UZALENO ambalo kimsingi lilianzia Lindi kwenye uwanja wa Ilulu.

Neno hili liliihusu timu ya Kariakoo ya Lindi ambayo katika uwanja wao wa nyumbani ilikuwa haramu kwa wapinzani kupata sare...achilia mbali kushinda. Msimu huo kulikuwa na sare moja tu...0-0 dhidi ya Yanga, basi. Simba walienda pale na kukutana na kipigo cha 1-0 kwa bao la Jemedari Said dakika ya 51.

Kipa na nahodha wa Simba, Mohamed Mwameja, sambamba na katibu mkuu wa TFF aliyepita, Kidao Wilfred, wakaongoza mgomo na kuwashawishi wachezaji wenzao kususia mechi na kutoka uwanjani.

Wakatoka na hawakurudi tena...endapo Chama angekuwepo labda angewashawishi kurudi uwanjani, kama alivyofanya Sadio Mane.


LIGI YA BARA SEPTEMBA 11, 1999

Uwanja ni Manungu, mechi ya Ligi Kuu kuu Bara kati ya Mtibwa na Simba. Dakika ya 38 beki wa Simba, Amry Said 'Stam' anaoneshwa kadi nyekundu na kugoma kutoka uwanjani.

Nahodha wa Simba, Mohamed Mwameja akawaongoza vijana kumuunga mkono beki wao na kugoma kuendelea na mchezo.

Amry Said akagoma kutoka na Simba wakagoma kuendelea na mchezo...na hatimaye wakatoka uwanjani...na hawakuridi tena. Labda Chama angekuwepo angewasaidia kama Saido Mane.