Chama aishika pabaya Simba, mabosi wapagawa

MABOSI wa Simba wanakuna kichwa baada ya kiungo fundi na mkali wa asisti wa kikosi hicho, Clatous Chama kuwashika pabaya. Mwanaspoti linajua kwamba mkataba wake wa mwaka mmoja anafikia ukingoni na sasa ishu inayoendelea ndani ni namna gani ya kumuongeza.

Chama ana asisti sita sawa na Ayoub Lyanga wa Azam, huku akifunga bao moja katika Ligi Kuu Bara na yupo kwenye kiwango kikubwa kiasi cha kuwapagawisha mashabiki wa timu hiyo kama viongozi wanavyohaha ndani kwa ndani kumtia kitanzi cha miaka miwili.

Utamu wa Chama kwa sasa umewavuruga mabosi wa Simba baada ya kukumbuka kuwa, mkataba wake wa mwaka mmoja upo ukingoni kwenye dirisha dogo na hivyo wanalazimika kukaa naye chini ili kuweka mambo sawa, kwani bado wanamhitaji mno kwa mechi za michuano ya ndani na ile ya CAF.

Kiungo huyo Mzambia alirejea Msimbazi dirisha dogo lililopita akitokea RS Berkane ya Morocco, inaelezwa kabla ya Simba kwenda michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023 chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ na Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez unataka kila kitu kikamilike.

Habari zinasema lengo la Simba ambao wanafanya siri kubwa suala hilo ni kumuongezea mkataba mpya wa miaka miwili kama pande zote mbili zitakubaliana, kwani wa awali unafikia ukingoni mwishoni mwa Januari mwakani.

Habari za ndani ya kamati ya usajili zinasema kwamba awali Simba walimpa mkataba wa mwaka mmoja, licha kuwepo kwa mapendekezo ya kupewa miaka miwili ila lilishindikana kwa vile kulikuwa na wasiwasi na kiwango chake kutokana na kushindwa kufanya vizuri alipotoka Berkane huku ikidaiwa wakati huo kwamba alikuwa na pancha.

Chanzo hicho cha kuaminika kilidokeza kuwa, huenda isiwe kazi ngumu kwa mabosi hao wa Msimbazi kumuongezea mkataba Chama kwa vile kwenye ule wa awali wa mwaka mmoja kulikuwa na kipengele cha kuongeza mwingine kama itakuwa imeridhika na huduma yake. Hata hivyo, hofu iliyo sasa ni kama ataamua kuweka masharti ya masilahi yao kwa kiwango alichokionyesha hivikaribuni.

Inaelezwa mabosi wa Simba akiwamo Barbara Gonzalez anayefanya kazi ya kuzungumza na kuwasainisha makocha, wachezaji wapya na waajiriwa wengine kwenye timu hiyo watahitajika kuandaa mkwanja mrefu si chini ya Sh150 Milioni ili kumbakisha Chama.

“Ni kama tulibugi sana awali tulipohofia kumpa mkataba mrefu na kwa kiwango alichonacho, huenda akasumbua kidogo kuongeza dau, lakini tumejipanga kuhakikisha tunabaki naye kwa misimu mingine inayo, Chama ni mchezaji muhimu kikosini,” kilisema chanzo hicho. Barbara aliiambia Mwanaspoti wiki iliyopita kwamba wanaingia kwenye dirisha dogo kwa nguvu na watatumia fedha nyingi kununua, kuvunja mikataba.

Chama atakuwa kwenye wakati mzuri katika mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya kwani ni mchezaji wa kutegemewa kwenye kikosi cha kwanza kutokana na ubora aliyokuwa nao wakati huu mechi nyingi anapokuwa uwanjani Simba inafanya vizuri na kupata ushindi.

Hivi karibuni kiungo huyo alifungiwa mechi tatu, Simba ikashinda mechi moja na kutoka sare michezo miwili kabla ya kurejea kwa moto.

Chama amefunga bao moja dhidi ya Geita Gold na kuasisti mabao sita ya Ligi Kuu, huku kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ameasisti pasi nne za mabao na kufunga bao moja na kuivusha timu hiyo makundi ikisubiri kujua watakaopangwa nao wakati droo itakapofanyika Desemba 12.

Simba walitua Tanga kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union, ikiondoka na karibu wachezaji wote.