CAF yaipa pigo Simba, mashabiki wafungiwa
Muktasari:
- Katika msimu uliopita, Simba ilifungiwa kucheza bila mashabiki katika mechi ya hatua ya makundi dhidi ya CS Constantine na faini ya Doła 40,000 (Sh98 milioni).
Dar es Salaam. Simba imepewa adhabu ya kucheza bila mashabiki katika mechi yake ya nyumbani ya hatua ya kwanza ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya Gaborone United, Septemba 28, 2025.
Mbali na kifungo hicho cha mashabiki, Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) pia imeipa Simba adhabu ya faini kiasi cha Dola 50,000 (Sh123 milioni).
Barua iliyotumwa na Kamati ya Nidhamu ya CAF kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefafanua kwamba adhabu hiyo imetokana na makosa ya kinidhamu ambayo Simba iliyafanya katika mechi ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Masry, Aprili 9, 2025.
“Kamati ya Nidhamu imeamua, Simba imekutwa na hatia ya kuvunja Ibara ya 82 na 83.2 ya kanuni za nidhamu na pia Ibara za 32, 33 na 35 za kanuni za Usalama na Ulinzi.
“Simba imeamriwa kulipa faini ya Dola 50,000 kwa kuvunja usalama ikiwemo kutumia fataki na kuvamia uwanja.
“Kwa kuzingatia Ibara ya 108 ya muongozo wa Nidhamu wa CAF, na uamuzi wa Bodi ya Nidhamu uliotaarifiwa Januari 14, 2025, adhabu ya kutocheza mechi moja bila mashabiki inafanya kazi moja kwa moja ikianza katika mechi inayofuata ya mashindano ya klabu,” imefafanua barua hiyo.
Kamati hiyo ya Nidhamu ya CAF imesisitiza kwamba malipo ya faini ya fedha yanapaswa kufanyika ndani ya siku 60 baada ya kutolewa.
Ikumbukwe dhidi ya CS Constantine, Simba ilicheza bila mashabiki kutokana na vurugu ambazo mashabiki wake walifanya katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita dhidi ya CS Sfaxien.
Katika mchezo huo ambao Simba ilishinda kwa mabao 2-1, zilitokea vurugu ambazo zilisababisha viti 256 kuvunjwa.