Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CAF kumenoga, mambo yameanza kujipa

Muktasari:

  • Sundowns walionyesha kile ambacho kwa miaka ya karibuni kimekuwa alama yao, kutawala mpira, nidhamu ya kimkakati na ufanisi wanapopata nafasi.

Wikiendi imekuwa na msisimko wa aina yake kutokana na uwepo wa mechi za mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ambayo ni Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Jana jioni kulikuwa na mechi moja ya Kombe la Shirikisho ambapo AS Maniema waliichapa USM Alger mabao 2-1, kisha baadaye zilipigwa nyingine mbili, moja ya Ligi ya Mabingwa iliyozikutanisha Esperance dhidi ya Al Ahly ambapo Al Ahly ililala 1-0 ugenini na ya Kombe la Shirikisho, Olympique de Safi dhidi ya Wydad mechi ikimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Kwa mechi zilizochezwa Ijumaa na Jumamosi, ni Mamelodi Sundowns pekee iliyopata ushindi tena ikiwa nyumbani ikiichapa Stade Malien mabao 3-0. Zingine zimeisha kwa sare na kufanya mechi za marudiano kuanza upya lakini ni faida kwa watakaokuwa wenyeji kwani wanaingia na bao la ugenini.

Kwa kifupi, matokeo ya michezo ya kwanza ya robo fainali yameanza kutoa taswira ya namna vita ya kufuzu nusu fainali itakavyokuwa.

Baadhi ya wachezaji wa kikosi cha Pyramids ya Misri wakati walipokuwa wakipasha misuli kabla ya mechi dhidhi ya AS FAR. Picha na Mtandao


Ligi ya Mabingwa

Ushindi wa mabao 3-0 walioupata Sundowns mjini Pretoria si tu umeonyesha tofauti ya kiwango kati ya timu hizo mbili, bali pia umeweka msingi mzuri kwa mabingwa hao wa Afrika Kusini kuelekea mchezo wa marudiano nchini Mali.

Sundowns walionyesha kile ambacho kwa miaka ya karibuni kimekuwa alama yao, kutawala mpira, nidhamu ya kimkakati na ufanisi wanapopata nafasi. Bao la kwanza la Khuliso Mudau liliwapa utulivu, huku mabao ya kipindi cha pili yakizidi kuwavunja nguvu wapinzani wao.

Matokeo ya 3–0 yana maana kubwa, hasa unapokwenda kucheza ugenini. Stade Malien sasa wanahitaji kushinda kwa tofauti ya mabao manne ili kusonga mbele moja kwa moja, au angalau 3–0 ili kulazimisha mikwaju ya penalti. Hilo linaifanya kazi yao kuwa ngumu sana.

Kwa Sundowns, mkakati katika mchezo wa marudiano unaweza kuwa rahisi zaidi kulinda faida waliyonayo huku wakitafuta bao la ugenini litakaloweza kuua kabisa matumaini ya wapinzani wao.

Tofauti na mchezo wa Sundowns, pambano kati ya AS FAR na Pyramids lilikuwa na ushindani mkubwa zaidi. AS FAR waliingia kwa kasi na kupata bao la mapema kupitia Ahmed Hammoudan, lakini walishindwa kulinda uongozi wao hadi mwisho baada ya Mahmoud Zalaka kusawazisha.

Kwa upande wa Pyramids, sare hiyo inaonekana kuwa matokeo mazuri kutokana na kwamba wamepata bao la ugenini na sasa watarudi nyumbani nchini Misri wakiwa na faida.

Hata hivyo, sare ya 1–1 inaacha kila kitu wazi. AS FAR wana uwezo wa kushtua iwapo wataweza kufunga ugenini katika mchezo wa marudiano, kwani bao moja linaweza kubadilisha kabisa hesabu za kufuzu.

Mshambuliaji wa Pyramids, wakati akijaribu kuwatoka mabeki wa AS FAR katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyomalizika kwa sare ya 1-1

Washindi wa Kombe la Shirikisho msimu uliopita ambao sasa wanashiriki Ligi ya Mabingwa, RS Berkane wamelazimika kusubiri uamuzi wa mchezo wa marudiano baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya wageni Al-Hilal ya Sudan katika mchezo wa kwanza wa robo fainali.

Wageni Al-Hilal ndio walioanza kuonyesha makali mapema, wakitumia vyema nafasi yao ya kwanza ya wazi kufunga bao katika dakika ya 13 kupitia Omar Abdel Rahman, aliyemalizia shambulizi lililopangwa kwa ustadi na kuwanyamazisha mashabiki wa wenyeji. Bao hilo liliipa Al-Hilal kujiamini na kuifanya RS Berkane kuanza kutafuta njia ya kurudi mchezoni.

Baada ya kuruhusu bao hilo la mapema, RS Berkane waliongeza kasi ya mashambulizi wakitawala sehemu kubwa ya mchezo, lakini walikumbana na uimara wa safu ya ulinzi ya Al-Hilal iliyokuwa makini kuzuia hatari. Shinikizo la wenyeji liliongezeka zaidi katika kipindi cha pili huku wakijaribu kupenya ngome ya wapinzani wao.

Dakika za mwisho za mchezo zilileta afueni kwa RS Berkane baada ya mwamuzi kuipa timu hiyo penalti. Mounir Chouiar alisimama kuipiga na kufunga kwa utulivu, akiisawazishia timu yake na kuokoa matumaini yao kuelekea mchezo wa marudiano.

Sare hiyo inaacha kila kitu wazi kabla ya pambano la pili, ambapo Al-Hilal watarejea nyumbani wakiwa na faida ya kufunga bao ugenini mapema, huku RS Berkane wakihitaji matokeo mazuri zaidi ili kuendelea na safari yao ya kutinga nusu fainali.

Baadhi ya wachezaji wa Zamaleck wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS Otoho.


Kombe la Shirikisho

Mabingwa wa Misri, Zamalek SC, wamejiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kutoka sare ya 1–1 ugenini dhidi ya AS Otoho katika mchezo wa kwanza wa robo fainali uliochezwa mjini Brazzaville, Congo.

Matokeo hayo yanaipa Zamalek faida ndogo lakini muhimu kabla ya mchezo wa marudiano utakaochezwa kwenye Cairo International, ambapo sare tasa pekee inaweza kuwatosha kufuzu nusu fainali. Hata hivyo, ushindani ulioonekana katika mchezo wa kwanza unaonyesha wazi kuwa pambano hilo bado liko wazi.

Katika mechi ya juzi, wenyeji Otoho waliingia uwanjani kwa ari kubwa wakitumia vizuri faida ya uwanja wa nyumbani na mashabiki wao. Dakika ya 13 walifanikiwa kupata bao la kuongoza kupitia Charles Atipo, aliyepiga mpira wa adhabu.

Bao hilo liliwapa nguvu wenyeji na kwa muda mfupi Zamalek walionekana kukosa utulivu, wakilazimika kucheza kwa tahadhari huku wakitafuta namna ya kurudi mchezoni.

Hata hivyo kadri muda ulivyokwenda, uzoefu wa kimataifa wa Zamalek ulianza kujitokeza. Wakaanza kutawala umiliki wa mpira na kulazimisha Otoho kucheza zaidi kwa kujilinda.

Shinikizo hilo lilizaa matunda dakika ya 32 baada ya pasi nzuri ya Ahmed Rabie kumpata Oday Al-Dabbagh, ambaye alimalizia kwa utulivu kusawazisha mabao.

Kuanzia hapo, Zamalek walionekana kuwa na udhibiti zaidi wa mchezo na hata kukaribia kupata bao la pili kabla ya mapumziko kupitia mashambulizi ya pembeni yaliyokuwa yakiongozwa na Chico Banza.

Mwisho wa siku, sare hiyo inaonekana kuwa na thamani kubwa zaidi kwa Zamalek kuliko wenyeji. Bao la ugenini linawapa faida ya kisaikolojia kuelekea mchezo wa marudiano.

Kwa upande wa Otoho, bado wana kazi kubwa mbele yao kwani watalazimika kufunga ugenini jijini Cairo ili kuwa na nafasi ya kufuzu.

Kwa ujumla, matokeo ya mchezo huu yanaacha pambano la robo fainali likiwa wazi, lakini uzoefu na mazingira ya nyumbani vinaifanya Zamalek kuingia mchezo wa pili wakiwa na matumaini makubwa ya kusonga mbele.

Katika mchezo mwingine wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho, CR Belouizdad waliibuka na sare ya 1–1 ugenini dhidi ya Al Masry baada ya kusawazisha katika dakika za mwisho za mchezo.

Wenyeji Al Masry walionekana kuwa njiani kupata ushindi baada ya Salah Mohsen kufunga kwa penalti kipindi cha pili.

Hata hivyo, matumaini yao yalipotea katika muda wa nyongeza wakati Lotfi Boussouar alipofunga bao muhimu la kusawazisha na kuiacha mechi hiyo ikiwa wazi kabla ya marudiano yatakayochezwa Algeria.

Sasa Al Masry watalazimika kutafuta ushindi ugenini, huku Belouizdad wakifaidika na sare hiyo muhimu waliyoipata ugenini.