Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Azam vs Yanga fainali ya wakubwa Gombani

Muktasari:

  • Majira ya saa 1:00 usiku, kipute kitaanza kupigwa kwenye Uwanja wa Gombani kumsaka bingwa mpya wa Kombe la Mapinduzi.

Pemba. Kuna vita nyingi zinakwenda kushuhudiwa leo Jumanne katika fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba ambapo Azam itakapocheza dhidi ya Yanga, lakini kukiwa na mambo mawili makubwa, mbinu na ufundi ndizo zitakazoamua bingwa wa msimu huu.

Kama hujui hii ni fainali ya kwanza katika Kombe la Mapinduzi inazikutanisha Azam na Yanga tangu 2007 ilipoanza michuano hiyo rasmi kwa kushirikisha timu kutoka nje ya Zanzibar.

Licha ya kwamba timu hizo sio mara ya kwanza kucheza fainali ya michuano hii na kubeba ubingwa kila moja, lakini safari hii kuna ladha tofauti tunakwenda kuishuhudia zinapokutana.

Tayari zimechezwa fainali kadhaa za Mapinduzi zikihusisha timu kutoka Bara. Azam imewahi kucheza dhidi ya Simba pekee, huku Yanga ikicheza dhidi ya Mtibwa na Simba.

Majira ya saa 10:00 jioni, kipute kitaanza kupigwa kwenye Uwanja wa Gombani kumsaka bingwa mpya wa Kombe la Mapinduzi.


DIMBA LITACHAFUKA

Mbinu za makocha wa timu zote mbili, Florent Ibenge wa Azam na Pedro Goncalves wa Yanga, zinatarajiwa kutoa mechi nzuri leo kutokana na kile tulichoshuhudia kuanzia makundi hadi nusu fainali.

Mara moja pekee tumeshuhudia Azam ikitanguliwa kufungwa bao, lakini ikajipanga vizuri na kusawazisha kisha kupata ushindi.

Mbali na hilo, mara moja Azam imeongoza lakini mpinzani akasawazisha na matokeo kuwa sare. Kwa Yanga, haijawahi kutanguliwa wala kuruhusu bao.

Hii yote inatokana na mbinu bora za makocha hao wakitumia zaidi viungo wa kati kuiweka timu kuwa imara muda wote wa mechi.

Yanga ilikuwa inamtegemea Mohamed Damaro na Duke Abuya eneo la kiungo wa kati wakicheza chini, kisha Maxi Nzengeli akiibia kule juu. Pia wakati mwingine Damaro na Abuya wanapishana kwenda juu.

Mechi ya leo, Damaro anakosekana kutokana na kadi nyekundu aliyoonyeshwa mechi ya nusu fainali dhidi ya Singida Black Stars, hivyo kuna uwezekano Mudathir Yahya akaanza kutokana na kupona majeraha.

Azam mechi tatu zilizopita ilimkosa Sadio Kanoute aliyekuwa majeruhi, lakini mazoezi ya mwisho ameonekana akifanya pamoja na timu ikiashiria kupona na huenda akawepo leo.

Hata hivyo, wakati yeye hayupo, nahodha Himid Mao na James Akaminko walikichafua sana pale kati na wanaweza kuendelea kukichafua kwani ushirikiano wao umelipa kwa kuivusha timu hadi fainali.

Dimba la kati anapokuwepo Abuya ambaye amekabidhiwa kitambaa cha unahodha katika michuano hii, huku Mudathir na Maxi wakiimarisha Yanga, kule Azam Akaminko na Himid, lazima pachimbike.

Katika kushambulia, makocha wote wanatumia pembeni, lakini kila mmoja amechagua upande wake.

Azam inatumia zaidi upande wa kulia anapocheza Nathaniel Chilambo na Cheikna Diakite. Pia Azam ni wazuri katika kutumia mipira ya kutenga kiasi ambacho Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker alikiri hilo kwa kusema kikosi hicho kilipoteza kwa bao 1-0, kupitia shambulizi lililoanzia mpira wa kona.

Kwa upande wa Yanga ipo imara wa mashambulizi ni wa kushoto kule anapocheza Pacome Zouzoua na Chadrack Boka. Pia timu zote zinatumia katikati kujenga mashambulizi na kutawanya pembeni.


WAZEE WA KUAMUA MECHI

Jephte Kitambala wa Azam, ndiye kinara wa mabao aliyebaki katika mashindano haya akiwa nayo mawili. Ndiye mshambuliaji tegemeo wa Azam kuelekea mechi hii ya fainali.

Safu ya ulinzi ya Yanga inapaswa kumchunga, kwani amekuwa hatari kwa wapinzani tangu atue msimu huu.

Tayari mshambuliaji huyo ameitungua Simba katika mechi ya Ligi Kuu alipokutana nayo kwa mara ya kwanza. Pia anakwenda kucheza dhidi ya Yanga kwa mara ya kwanza.

Mbali na Kitambala, kuna Zidane Sereri, anayeunda pacha naye safu ya ushambuliaji ya Azam. Naye amefunga bao moja. Pia aliifunga Simba msimu uliopita, hivyo sio mgeni wa mechi kubwa.

Yanga ina Pacome Zouzoua, amefunga na kutoa asisti, ni mmoja wa wachezaji hatari eneo la kutengengeneza mashambulizi. Azam imchunge sana.

Mwingine ni Maxi Nzengeli. Ana tuzo zake mbili za mchezaji bora, hiyo inaonyesha ni mtu hatari ndani ya uwanja. Amefanikiwa kufunga bao moja.

Yote kwa yote, kila upande una kazi ya kufanya kuhakikisha inabeba ubingwa. Azam iliyofunga mabao sita katika mechi nne, ina kazi ya kuipenya ngome ya Yanga ambayo haijaruhusu nyavu zake kutikiswa hadi sasa ikishuka dimbani mara tatu.

Hata hivyo, Azam imekuwa na rekodi ya kufunga bao kila mechi iliyocheza, hivyo timu hiyo leo ina kazi kuendeleza mwendo wao huo dhidi ya timu isiyofungika.

Yanga ina kazi ya kulinda lango lake na kuweka rekodi ya kumaliza bila nyavu zake kutikiswa, huku pia ikihitaji bao kuifanya pia ifunge kila mechi.


REKODI, KISASI

Azam inasaka taji la sita baada ya kubeba mwaka 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019, inasaka nafasi ya kutanua rekodi iliyonayo, kwani hivi sasa ndio timu iliyobeba mara nyingi, huku Yanga ikilisaka kwa mara ya tatu ikiifukuzia Simba yenye manne. Tayari Yanga imelichukua mwaka 2007 ikiifunga Mtibwa na 2021 ilipoichapa Simba.

Yanga hii inakuwa fainali ya nne katika historia ya Kombe la Mapinduzi ikifanya hivyo mwaka 2007, 2011, 2021 na sasa 2026. Azam ni fainali ya saba, kati ya sita zilizopita imebeba ubingwa mara tano na kukosa moja mwaka 2022 ilipochapwa na Simba.

Wakati Yanga na Azam hii ikiwa mara ya kwanza zinakutana katika fainali ya Kombe la Mapinduzi, rekodi zinaonyesha mara ya mwisho zilikutana katika fainali ya Kombe la FA iliyochezwa Zanzibar Juni 2, 2024 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex. Yanga ilishinda kwa penalti 6-5 baada ya muda wa kawaida matokeo kuwa 0-0. Leo Azam ina nafasi ya kulipa kisasi cha kupoteza dhidi ya Yanga mara ya mwisho zilipocheza Zanzibar.

Kwa upande wa makocha, Pedro Goncalves wa Yanga anasaka taji lake la kwanza tangu atue kikosini hapo, huku pia Florent Ibenge wa Azam naye analitolea macho taji hilo ashinde kwa mara ya kwanza akiwa klabuni hapo.


ZIMEFIKAJE HAPA?

Azam iliyokuwa Kundi A, ilianza safari ya kusaka taji la sita kwa kutoka 1-1 dhidi ya Singida Black Stars, kisha ikaifunga Mlandege 2-0 na kumalizia kuichapa URA 2-1.

Hatua ya nusu fainali, ilikwenda kuichapa Simba bao 1-0, hivyo hadi kumaliza michuano hii, Azam itakuwa imekutana na timu tatu zilizomaliza nne bora ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita ambazo ni Singida, Simba na Yanga.

Kwa upande wa Yanga ilikuwa kundi C, imeshinda mechi zote ikianza kuifunga KVZ 3-0, ikaja kuichapa TRA United 1-0, nusu fainali ikaifunga Singida Black Stars 1-0.


MTEGO WA FAINALI

Kuna wachezaji kadhaa wanaweza kukosekana baada ya kupata majeraha katika mashindano haya, hali hiyo inaweza kufanya kuziona sura mpya zikaibuka leo ili kuziba mapengo yaliyopo na umuhimu wa mechi yenyewe.

Sadio Kanoute wa Azam anaweza kuwepo au asiwepo, hii itategemea na uimarikaji wake baada ya kupona kutoka kwenye majeraha.

Lassine Kouma na Aziz Andabwile upande wa Yanga wana hatihati kubwa ya kuwepo, waliumia mechi za mwanzoni, huku pia Damaro anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa hatua ya nusu fainali, hayupo.

Damaro alikuwa mchezaji tegemeo eneo la kiungo mkabaji, hivyo kukosekana kwake itamlazimu Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves kumpa majukumu mwingine. Iwe Duke Abuya au Mudathir Yahya ambaye amepona hivi karibuni.

Kiungo mkabaji aliyebaki, Moussa Balla Conte amerudishwa kucheza beki wa kati baada ya Andabwile ambaye naye ni kiungo aliyekuwa akicheza beki wa kati kuumia. Hata hivyo, kuna beki mwingine wa kati, Nizar Abubakar Othuman 'Ninju' ambaye mechi iliyopita dhidi ya Singida aliishia benchi, akacheza Conte, kabla ya hapo alicheza dhidi ya KVZ na TRA United.

Frank Assinki amebaki kuwa beki wa kati pekee tegemeo, hivyo kunaweza kutokea mabadiliko makubwa eneo hilo leo kutokana na uhaba wa viungo na mabeki wa kati.


WASIKIE MAKOCHA

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, alisema: "Kufika fainali ni sehemu ya kuyafikia malengo yetu tuliyojiwekea wakati tunakuja kushiriki mashindano haya. Tunautaka ubingwa lakini pia tupo hapa kuimarisha kikosi kuelekea mechi za CAF ndio maana natoa fursa kwa wachezaji tofauti tuliokuja nao."

Kocha wa Azam, Florent Ibenge naye alisema: "Niliweka malengo ya kucheza mechi tano katika mashindano haya na hiyo inakwenda kutimia siku ya fainali. Lakini pia malengo ya ubingwa yapo palepale.

"Ubingwa utatupa nafasi nzuri ya kuona wapi tumefanikiwa kwani tunakabiliwa zaidi na mechi ngumu ya CAF ugenini dhidi ya Nairobi United."


FAINALI ZA AZAM

2012 Azam 3-1 Jamhuri

2013 Azam 2-1 Tusker

2017 Azam 1-0 Simba

2018 Azam 0-0 URA (penalti 4-3)

2019 Azam 2-1 Simba

2022 Simba 1-0 Azam


FAINALI ZA YANGA

2007 Yanga 2-1 Mtibwa

2011 Simba 2-0 Yanga

2021 Yanga 0-0 Simba (penalti 4-3)


TAKWIMU


MAKUNDI

Kundi A: Mlandege, Azam, Singida Black Stars, URA

Kundi B: Simba, Muembe Makumbi City, Fufuni

Kundi C: Yanga, KVZ, TRA United


MATOKEO

Desemba 28, 2025

Mlandege 1-3 Singida BS (1:00 usiku)

(Said Khamis Matola 80') (Idrissa Diomande 72', Emmanuel Keyekeh 77, Joseph Guede 90')


Desemba 29, 2025

Fufuni 1-1 Muembe Makumbi (Saa 10:15 jioni)

(Mboni Steven Kibamba 56') (Abdallah Idd Pina 63')

KVZ 1-1 TRA United (Saa 2:15 usiku)

(Michael Joseph Godlove 66') (Enock Mkanga 54')


Desemba 31, 2025

Mlandege 0-1 URA (Saa 10:15 jioni)

(Amaku Fred 6')


Singida BS 1-1 Azam (Saa 2:15 usiku)

(Joseph Guede 75') (Jephte Kitambala 69')


Januari 2, 2026

Azam 2-0 Mlandege (Saa 2:15 usiku)

(Zidane Sereri 6', Himid Mao 54')


Januari 3, 2026

Singida BS 1-1 URA (Saa 10:15 jioni)

(Idriss Diomande 45') (Mulikyi Hudu 26')


Simba 1-0 Muembe Makumbi (Saa 2:15 usiku)

(Mohamed Bajaber 21')


Januari 4, 2026

Yanga 3-0 KVZ (Saa 11:00 jioni)

(Pacome Zouzou 32', Rahim Andrea 54 (OG), 75' (OG)


Januari 5, 2026

Azam 2-1 URA (Saa 10:15 jioni)

(Jephte Kitambala 23', Albogast Kyobya 90+5') (Nelson Ssenkatuuka 10')


Fufuni 1-2 Simba (Saa 2:15 usiku)

(Mboni Stephen Kibamba 14') (Hussein Mbegu 23', Naby Camara 90')


Januari 6, 2026

Yanga 1-0 TRA (Saa 2:15 usiku)

(Celestine Ecua 31')


Januari 8, 2026

Nusu Fainali ya Kwanza

Azam 1-0 Simba (Saa 2:15 usiku)

(Lameck Lawi 73')


Januari 9, 2026

Nusu Fainali ya Pili

Yanga 1-0 Singida BS (Saa 2:15 usiku)

(Maxi Nzengeli 54')


Januari 13, 2026

Fainali

Azam vs Yanga (Saa 1:00 usiku)



WAFUNGAJI

2 Joseph Guede (Singida BS)

    Idrissa Diomande (Singida BS)

    Mboni Stephen Kibamba (Fufuni)

    Jephte Kitambala (Azam)


1 Emmanuel Keyekeh (Singida BS)

   Said Khamis Matola (Mlandege)

   Abdallah Idd Pina (Muembe Makumbi)

   Michael Joseph Godlove (KVZ)

   Enock Mkanga (TRA United)

   Amaku Fred (URA)

   Zidane Sereri (Azam)

   Himid Mao (Azam)

   Mulikyi Hudu (URA)

   Mohamed Bajaber (Simba)

   Pacome Zouzoua (Yanga)

   Nelson Ssenkatuuka (URA)

   Albogast Kyobya (Azam)

   Hussein Mbegu (Simba)

   Naby Camara (Simba)

   Cestine Ecua (Yanga)

   Lameck Lawi (Azam)

   Maxi Nzengeli (Yanga)


MCHEZAJI BORA

Morice Chukwu - Singida BS (vs Mlandege & URA)

Mboni Stephen Kibamba - Fufuni (vs Muembe Makumbi City)

Abdulaziz Makame - TRA United (vs KVZ)

George Masembe - URA (vs Mlandege

Himid Mao - Azam (vs Singida BS)

Aishi Manula - Azam (vs Mlandege)

Chamou Karaboue - Simba (vs Muembe Makumbi)

Maxi Nzengeli - Yanga (vs KVZ & Singida)

Jephte Kitambala - Azam (vs URA)

Naby Camara - Simba (vs Fufuni)

Lameck Lawi - Azam (vs Simba)


MCHEZAJI MWENYE NIDHAMU

Aimar Hafidh 'Haaland' - Mlandege (vs Singida BS)

Yakoub Said Mohamed - Muembe Makumbi (vs Fufuni & Simba)

Michael Joseph Godlove - KVZ (vs TRA United)

Jamal Saleh - Mlandege (vs URA)

Abdulmalick Zakaria - Singida BS (vs Azam & Yanga)

Okorasma Manyemi - Mlandege (vs Azam)

Mulikyi Hudu - URA (vs Singida BS)

Majid Khamis 'Dudu' - KVZ (vs Yanga)

Otti Ronald - URA (vs Azam)

Karim Ali Khamis - Fufuni (vs Simba)

Naby Camara - Simba (vs Azam)


WALIOJIFUNGA

Rahim Andrea - KVZ (vs Yanga - 2)


PENALTI

Yussuf Suleiman Haji - Mlandege (vs Singida) AMEKOSA


KADI NYEKUNDU

David Kameta - Simba (vs Azam)

Mohamed Damaro - Yanga (vs Singida)

Morice Chukwu - Singida (vs Yanga)


MABINGWA KOMBE LA MAPINDUZI

2007 Yanga

2008 Simba

2009 Miembeni

2010 Mtibwa Sugar

2011 Simba

2012 Azam

2013 Azam

2014 KCCA

2015 Simba

2016 URA

2017 Azam

2018 Azam

2019 Azam

2020 Mtibwa Sugar

2021 Yanga

2022 Simba

2023 Mlandege

2024 Mlandege

2025 Zanzibar Heroes