Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ateba ataja sababu mbili za kuchora tattoo ya Simba

Muktasari:

  • Ateba, amesema kilichomsukuma kuchora mchoro huo ni mnyama Simba ni mambo mawili na amefanya kwa upendo wa dhati na sio kulazimishwa.

Dar es Salaam. Wakati Meneja Habari wa klabu ya Simba, Ahmed Ally akitamba kwamba straika wa timu hiyo, Leonel Ateba amechora tattoo ya Mnyama Simba kutokana na mahaba aliyonayo kwa klabu hiyo, nyota huyo kutoka Cameroon amevunja ukimya na kutaja mambo mawili yaliyomsababisha kufanya hivyo.

Ateba amechora tatoo hiyo katika bega la kushoto na kuzua maswali mengi kabla ya Ahmed kutoa ufafanuzi huo, akidai amefanya hivyo kuonyesha mahaba aliyonayo kwa klabu hiyo ya Msimbazi aliyojiunga nayo msimu huu akitokea USM Alger ya Algeria.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo mwenye mabao manane katika Ligi Kuu Bara kwa sasa akiwa sambamba na nyota mwenzake wa Simba, Jean Charles Ahoua, amefafanua ukweli kuhusu mchoro huo alipozungumza na Mwananchi.

Ateba, amesema kilichomsukuma kuchora mchoro huo ni mnyama Simba ni mambo mawili na amefanya kwa upendo wa dhati na sio kulazimishwa.

Ametaja sababu ya kwanza ni timu ya taifa lake inaitwa Indomitable Lions (Simba wasiofungika) waliobeba ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mara tano  AFCON, lakini jingine ni  klabu yake ya sasa ya Simba, hivyo akaamua kuchora tattoo hiyo kama ishara ya kuonyesha upendo wake wa kufurahi kuzitumikia.

"Ni timu ninazozipenda ndio maana nimeona kitu pekee kitakachoonyesha upendo ni kuchora tattoo, ambayo inawakilisha klabu ninayoitumikia na timu yangu ya taifa ya Cameroon ambao nao wanaitwa Simba, lakini ni wale wasiofungika," amesema Ateba ambaye msimu uliopita akiwa na USM Alger alifunga bao moja katika mechi 12.

Nyota huyo mwili jumba, amesema ameona namna ambavyo mashabiki wa Simba walivyoipokea tattoo yake kwa upendo, huku wengine wakimposti katika mitandao yao ya kijamii, jambo linalomuongezea nguvu ya kupambana zaidi, ili mchango wake wa kupigania ubingwa kwa msimu huu uwe mkubwa.

"Najisikia faraja na naamini nitakuwa nimewajibu vyema watu ambao walikuwa wanajiuliza kuhusiana na jambo hilo," amesema Ateba ambaye akishirikiana na nyota wenzake wameiwezesha Simba kurudi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 47, moja zaidi na ilizonazo Yanga.