Prime
Wakala afunguka kitakachomng'oa Ngoma Simba
![](/resource/image/4924322/landscape_ratio2x1/320/160/d8358b9f01ff7cbbdb2948a270aa367d/sJ/ngoma-pc.jpg)
Muktasari:
- Mukandila anayemsimamia pia Djibrill Sillah wa Azam FC alisema kuwa hadi sasa Ngoma hajasaini mkataba wowote iwe wa kubaki Simba au kuondoka na uamuzi wa hilo utategemea nguvu ya ushawishi.
Wakala wa Fabrice Ngoma, kiungo nyota wa Simba, Faustino Mukandila amesema maslahi mazuri zaidi ambayo kiungo huyo atawekewa mezani ndio yataamua kama ataondoka au kubaki Msimbazi.
Mukandila ametoa kauli hiyo baada ya Al Ittihad ya Libya kuonyesha nia ya kuhitaji huduma za nyota huyo wa zamani wa AS Vita Club ya DR Congo na Raja Casablanca ya Morocco.
Mukandila anayemsimamia pia Djibrill Sillah wa Azam FC alisema kuwa hadi sasa Ngoma hajasaini mkataba wowote iwe wa kubaki Simba au kuondoka na uamuzi wa hilo utategemea nguvu ya ushawishi.
“Hakuna chochote kilichofanyika kati yetu na Simba wala timu nyingine. Kwa sasa mchezaji yupo na Simba na ibakie kuwa hivyo, lakini kama ataondoka au atabaki ni suala muda sahihi ukifika uamuzi utafanyika.
“Hakuna mazungumzo yoyote yanayoendelea baina yetu na Simba au klabu nyingine. Mchezaji kwa sasa yupo kwenye klabu yake na kumbuka kuwa kinachohitajika ni fedha. Hawa wachezaji wanacheza kwa ajili ya kutafuta fedha, hivyo inapokuja ofa nzuri ataipa kipaumbele,” alisema Mukandila.
Mukandila alisema Ngoma hana presha ya mkataba mpya kwa sasa na akili zake amezielekeza katika kuisaidia Simba kwenye mashindano ambayo inashiriki.
Mkataba wa Ngoma umebakiza miezi minne hivi sasa ili ufikie tamati na kwa sasa yuko huru kuingia makubaliano ya awali na timu yoyote tofauti na Simba kwa vile mkataba alionao uko chini ya muda wa miezi sita.
Mmoja wa viongozi wa Simba aliliambia Mwanaspoti kuwa hadi sasa hawajafanya mazungumzo yoyote na Ngoma ingawa wanaamini kuwa kiungo huyo kutoka DR Congo atabaki.
“Amekuwa akicheza vizuri na ni tegemeo katika timu pale katikati mwa uwanja. Ana nafasi kubwa ya kubakia kikosini ingawa hilo litatetegemea na kile kitakachomriwa hapo baadaye baada ya kukaa naye chini na kufanya mazungumzo.
“Unajua katika mazungumoz ya mkataba kuna vitu vingi vya kuvizingatia halafu baada ya hapo ndio uamuzi unafanyika. Wanasimba wanapaswa kuwa na subira kila kitu kitakaa sawa,” alisema mmoja wa viongozi wa klabu hiyo.
Ngoma alijiunga na Simba, Julai 14, 2023 akitokea Al Hilal kwa mkataba wa miaka miwili ambao utafikia tamati baada ya msimu huu kumalizika.
Uhamisho huo wa Ngoma kujiunga na Simba ulikuwa huru kwa vile kiungohuyo alikuwa amevunja mkataba wa kuitumikia Al Hilal.
Ngoma amekuwa mchezaji tegemeo wa Simba chini ya kocha Fadlu Davids na kudhihirisha hilo amecheza mechi 12 za Ligi Kuu Bara na pia amecheza michezo sita ya Kombe la Shirikisho Afrika.