Arteta alia na washambuliaji Arsenal
Muktasari:
- Arteta alionyesha kusikitishwa na jinsi timu yake ilivyoshindwa kutumia vizuri nafasi zake ili kufunga bao la nne ambalo lingeua kabisa matumaini ya Chelsea, lakini alitoa sifa nyingi kwa Zubimendi, si tu kwa kufunga bao la tatu la Arsenal bali pia kwa kiwango chake kwa jumla.
London, England. Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema amekwazika kwa timu yake kushindwa kufunga mabao manne katika mechi ya nusu fanali ya michuano ya Carabao Cup dhidi ya Chelsea iliyomalizika kwa kushinda mabao 3-2.
Hii inakuwa ni mechi ya kwanza kwa kocha mpya wa Chelsea, Liam Rosenior kupoteza tangu aanze kazi na inakuwa ni mechi ya pili kwa matajiri hao wa Jiji la London kufungwa na Arsenal wa msimu huu ingawa mechi ya kwanza ilikuwa inakosa huduma za wachezaji tegemeo kama Reece James, Cole Palmer, Malo Gusto, Liam Delap, Jamie Gittens na Moises Caicedo ambao baadhi walikuwa na majeraha, magonjwa na adhabu.
Arteta alionyesha kusikitishwa na jinsi timu yake ilivyoshindwa kutumia vizuri nafasi zake ili kufunga bao la nne ambalo lingeua kabisa matumaini ya Chelsea, lakini alitoa sifa nyingi kwa Zubimendi, si tu kwa kufunga bao la tatu la Arsenal bali pia kwa kiwango chake kwa jumla.
“Tuliona wazi tulikuwa na nafasi ya kushinda mechi kwa mabao zaidi ya haya tuliyopata, mwishoni tulikuwa na nafasi mbili za kufunga lakini hatukuzitumia. Tungefunga matokeo yangekuwa tofauti sana. Tukizungumza kuhusu Zubimendi, ni wazi anaweza kufanya chochote anachotaka. Kwa kiasi fulani unaweza kumfananisha Declan. Tunapaswa kuendelea kumtumia vizuri zaidi katika mfumo wetu kwa sababu ana uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali."
“Anakokota mpira, anapiga chenga, anapora mipira na ana uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi anapokuwa katika boksi la timu pinzani. Kimsingi ni mtulivu sana. Anaona mchezo kwa uwazi na kwa jicho la pili."
Baada ya filimbi ya mwisho, kulizuka mabishano kati ya wachezaji wa pande zote mbili pia Rosenior alijivunia namna wachezaji wake walivyopambana licha ya kukosa baadhi ya mastaa tegemeo.
Kipa Robert Sanchez alifanya makosa makubwa yaliyosababisha mabao mawili ya kwanza ya Arsenal, lakini Rosenior alikubali kuchukua lawama zote, akisema: “Wachezaji wangu wanapokosea, mimi ndiye ninayewajibika. Hilo ni kosa langu. Alifanya saves moja kipindi cha pili ambayo ilikuwa ya kiwango cha dunia. Asingedaka ingeweza kabisa kututoa mchezoni lakini alitusaidia. Nitaendelea kumwamini kama ninavyoamini wachezaji wengine. Kazi yangu ni kuwasaidia, si kuwalaumu."