Arsenal yashusha kocha mwingine
Muktasari:
- Liverpool ilinyakua ubingwa wa Ligi Kuu England katika kipindi cha Gronnemark alipokuwa katika timu hiyo na Klopp alisifu mchango wake.
London, England. Arsenal inataka iwe tishio zaidi kwenye mipira iliyokufa baada ya kumchukua gwiji wa mipira ya kurusha, Thomas Gronnemark.
Arsenal imekuwa wafalme wa mipira iliyokufa chini ya kocha Mikel Arteta kwa miaka kadhaa sasa.
Miamba hiyo ya Emirates ni miongoni mwa timu zilizofunga mabao mengi kwa mipira hiyo iliyokufa kwenye Ligi Kuu England msimu huu ikilingana na Chelsea na Leeds United. Lakini, kwenye mabao yao hayo hakuna hata moja lilifungwa kutokana na mpira wa kurushwa, hivyo Arteta anataka kumaliza tatizo hilo.
Arsenal imefanya mawasiliano na Gronnemark, ambaye amefanya umaarufu mkubwa kama mmoja wa makocha bora kabisa wa mipira ya kurusha duniani.
Gronnemark amefanya kazi na zaidi ya klabu 30, lakini alipata umaarufu mkubwa alipokuwa chini ya Jurgen Klopp huko Liverpool.
Liverpool ilinyakua ubingwa wa Ligi Kuu England katika kipindi cha Gronnemark alipokuwa katika timu hiyo na Klopp alisifu mchango wake.
Klopp alisema: “Niliposikia kuhusu Thomas, nilikuwa na uhakika wa asilimia 100 nataka kumwaajiri. Tulimleta Thomas na alibadili ishu ya mipira ya kurusha.”
Arsenal ni moja ya timu chache kwenye Ligi Kuu England zinazotumia staili ya kurusha mipira mirefu na sasa wameongeza silaha nyingine. Wachezaji Declan Rice na Riccardo Calafiori ndiyo ambao wamekuwa na kazi hiyo ya kurusha mipira. Kocha Arteta alisema Rice atakuwa mtaalamu wa mipira ya kurusha kama ambavyo amekuwa hodari katika kupiga mipira ya friikiki.
Arteta alisema: “Kila kitu ni lazima kihusishwe. Nafahamu ni ubora gani alionao Declan katika mipira iliyokufa. Najua hilo halikuanza tu, alijifunza mara nyingi na ninavyomwona Declan, anaweza kufanya karibu kila kitu.”