Arsenal yapewa Ubingwa wa UEFA, Madrid yaporomoka

Muktasari:
- Pamoja na historia yao ya mataji 15, Real Madrid wameshuka hadi nafasi ya mwisho katika orodha ya timu zilizosalia.
Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kikosi cha Arsenal kimepewa nafasi kubwa ya kutwaa taji la UEFA msimu huu, kwa mujibu wa makadirio ya kompyuta ya Opta.

Timu hiyo inayoongozwa na kocha, Mikel Arteta iliwaduwaza mabingwa wa kihistoria Real Madrid kwa ushindi wa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Emirates Jumanne wiki hii, ushindi uliotokana na mabao mawili ya kiungo Declan Rice kupitia mipira ya adhabu na jingine kutoka kwa Mikel Merino.
Matokeo hayo yameibua mabadiliko makubwa kwenye makadirio ya mashine hiyo ya takwimu, ambayo hutumia mchanganyiko wa rekodi za muda mfupi na mrefu za timu shiriki.
Kwa sasa, Arsenal wana nafasi ya asilimia 28.4% kutwaa taji hilo, wakiwazidi Barcelona (22.4%), Inter Milan (21.1%), na PSG (18.8%).

Pamoja na historia yao ya mataji 15, Real Madrid wameshuka hadi nafasi ya mwisho katika orodha ya timu zilizosalia, wakiwa na nafasi finyu ya asilimia 1.1% kutwaa taji hilo na asilimia 4% za kufika nusu fainali.
Barcelona, ambao walikuwa vinara kabla ya mechi za robo fainali kuanza, wameshuka hadi nafasi ya pili. Inter Milan, iliyowafunga Bayern Munich 2-1 ugenini, wamepanda hadi nafasi ya tatu ya kutwaa taji, huku PSG wakifuatia katika nafasi ya nne.