Arsenal haikamatiki Ligi Kuu England
Muktasari:
- Saka, ambaye jana alicheza mechi yake ya 300 akiwa na jezi ya Arsenal, alifunga bao la tisa akiwa na timu hiyo msimu huu katika mashindano yote.
London, England. Arsenal imeongeza tofauti ya pointi kileleni mwa Ligi Kuu England hadi pointi saba baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Brighton huku wapinzani wao wa karibu Manchester City wakibanwa nyumbani na Nottingham Forest.
Bao la mapema la Bukayo Saka limetosha kuipa timu ya Mikel Arteta pointi tatu muhimu, huku wapinzani wao katika mbio za Ubingwa, Manchester City wakishindwa kupata ushindi dhidi ya Nottingham Forest kufuatia sare ya 2-2.
Arsenal waliingia uwanjani bila beki wao tegemeo William Saliba, aliyepata majeraha ya kifundo cha mguu katika mchezo uliopita dhidi ya Chelsea.
Nafasi yake ilichukuliwa na Cristhian Mosquera, ambaye alipata wakati mgumu, akionyeshwa kadi ya njano mapema na baadaye kuonekana kuyumba kabla ya Riccardo Calafiori kuchukua nafasi yake.
Mshambuliaji wa Arsenal, Bukayo Saka, akishangilia baada ya kufunga bao lililoipa timu yake pointi tatu katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Brighton iliyopigwa Machi 4, 2026. Picha na Mtandao
Saka, ambaye jana alicheza mechi yake ya 300 akiwa na jezi ya Arsenal, alifunga bao la tisa akiwa na timu hiyo msimu huu katika mashindano yote, akifunga sita kwenye Ligi Kuu, mawili katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na moja kwenye Kombe la Karabao.
Brighton hawakuwa wasindikizaji tu. Georginio Rutter alikaribia kusawazisha lakini shuti lake la kona lilipanguliwa kwa ustadi na David Raya.
Kwa matokeo hayo, Arsenal sasa wanaongoza kwa pointi saba huku Man City wakiwa bado na mchezo mmoja mkononi.
Katika mechi nyingine zilizopigwa jana kwenye Ligi Kuu England, Chelsea ilipata ushindi mnono ugenini ikiichapa Aston Villa mabao 4-1, Fulham ikiwa nyumbani ilikubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya West Ham.
Mchezo mwingine uliokuwa wa kukata na shoka, ilishuhudiwa kwa mara ya kwanza Manchester United wakipoteza mchezo chini ya kocha wao wa muda, Michael Carrick dhidi ya Newcastle.
Leo tena kutakuwa na mechi moja ambapo Tottenham watakuwa nyumbani dhidi ya Crystal Palace