Yanga, Prisons mechi ya rekodi

Dar es Salaam. Yanga leo saa 1:00 usiku inashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons.

Yanga inaingia kwenye mchezo huo huku ikimkosa beki kisiki, Dickson Job ambaye ana adhabu ya kadi tatu za njano, nahodha Bakari Mwamnyeto ni majeruhi ilihali ikiwa na wasiwasi wa kuwakosa mshambuliaji hatari, Fiston Mayele mwenye mabao 10 na winga Jesus Moloko.

Akizungumzia mchezo huo sambamba na kuwakosa wachezaji hao, kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alisema licha ya kuwakosa, lakini wapo wengine.

“Tutamkosa Dickson (Job) kwa sababu ya adhabu, lakini tutaendelea kukosa huduma ya Mwamnyeto (Bakari), upande wa Fiston (Mayele) na Moloko (Jesus) hawa bado wapo 50 kwa 50 tutawaangalia jioni (ya jana),” alisema Kaze.

“Farid (Mussa) na Djuma (Shaban) wamerejea kwenye kikosi sambamba na Morrison (Benard), lakini yeye bado hayupo sawa sana kwa hiyo tutakuwa na mabadiliko kidogo kwenye mchezo wetu na Prisons.”

Kaze alisema licha ya kuwa na mabadiliko kwenye mchezo huo, lakini imani yao ni kuwa watakuwa na mchezo bora na mzuri zaidi ya waliocheza na Ihefu.

“Mechi iliyopita hatujafanya vizuri sana na tunajua Prisons ni nzuri na hata msimu uliopita tulitoka nayo sare hapa nyumbani. Tumekiandaa kikosi vizuri kwa ajili ya mchezo huu,” alisema Kaze.

Kukosekana kwa Job kutampa nafasi Ibrahim Bacca kuanza katika mchezo huo kwani alikicheza katika eneo hilo kwenye baadhi ya mechi za hivi karibuni.

Akizungumzia mchezo huo, mchezaji wa Yanga, Yusup Athuman alisema: “Mchezo wetu na Prisons utakuwa na kitu cha tofauti na lengo ni kuhakikisha tunapata pointi tatu.”

Kocha msaidizi wa Tanzania Prisons, Shaban Mtupa alisema wamefanya maandalizi mazuri na wamepata muda mwingi wa kupumzika tangu wacheze mchezo dhidi ya KMC jijini Dar es Salaam.

Mtupa alisema walikuwa na shida eneo la ulinzi, lakini suluhu na KMC maana yake wameanza kuimarika katika eneo hilo.

“Wachezaji wetu wakikutana na timu hizi siku zote wanakuwa na akili ya kutaka kushinda mchezo. Imani yetu tutafanya vizuri kwenye mchezo huo,” alisema Mtupa. Nahodha wake, Benjamin Asukile alisema mchezo huo utakuwa mkali.