Sababu TFF kuihamisha Yanga Uwanja wa KMC
Mwonekano wa Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam. Picha na Mtandao
Muktasari:
- TFF pia imezikumbusha klabu zote nchini kuendelea kutunza na kuboresha miundombinu ya viwanja vyao ili kukidhi vigezo vya mashindano.
Dar es salaam. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kuufungia Uwanja wa KMC Complex, uliopo Mwenge, Dar es Salaam kutumika kwa michezo ya Ligi Kuu, kutokana na kukosa vigezo vinavyohitajika.
Kupitia taarifa hiyo ambayo imetolewa leo Alhamisi, Januari 29, 2026, na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Ndimbo, TFF imesema uwanja huo haujakidhi matakwa ya Kanuni kama yalivyoainishwa kwenye masharti ya Leseni za Klabu, hali iliyolazimu kuchukuliwa kwa uamuzi huo.
Mwonekano wa Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam. Picha na Mtandao
TFF imeeleza kuwa, kuanzia sasa, timu zote zinazoutumia Uwanja wa KMC kwa michezo yao ya nyumbani zitalazimika kutumia viwanja mbadala, kama kanuni zinavyoelekeza, hadi pale uwanja huo utakapofanyiwa marekebisho.
“Timu husika zitatumia viwanja vingine kwa michezo yao ya nyumbani mpaka Uwanja wa KMC utakapofanyiwa marekebisho na kukaguliwa upya na TFF,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Shirikisho hilo pia limetumia fursa hiyo kuzikumbusha klabu zote nchini kuendelea kutunza na kuboresha miundombinu ya viwanja vyao ili kukidhi vigezo vya mashindano.
Mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube (Kulia), Laurindo Aurélio 'Depu' (Kushoto) wakishangilia moja ya bao katika ushindi wa 3-1 ilioupata Yanga dhidi ya Dodoma Jiji, Januari 27, 2026. Picha na Yanga
Uwanja huo ulikuwa ukitumiwa na klabu za KMC na Yanga kwa michezo yao ya nyumbani ya Ligi Kuu. Mara ya mwisho Yanga kuutumia uwanja huo ilikuwa juzi Jumanne, Januari 27, 2026, ambapo ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji.
Kwa upande wa KMC, mara ya mwisho kuutumia uwanja huo ilikuwa Novemba 25, mwaka jana, walipolazimishwa sare tasa dhidi ya Mtibwa Sugar