Waliofumbia, kuidhinisha ujenzi holela wawajibishwe
Muktasari:
Vilevile, ni utekelezaji wa tamko namba 8.2.1 la Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 linalosema: “Serikali za mitaa zitawajibika kushirikiana na Wizara ya Ardhi kuhakikisha usimamizi mzuri wa ardhi katika maeneo yao.”
Baada ya onyo la muda mrefu, hatimaye wiki hii Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na halmashauri za manispaa za Kinondoni na Temeke, zimeanza kazi ya ubomoaji nyumba zote zilizojengwa, bila kufuata utaratibu, kwenye maeneo ya wazi na hifadhi za barabara.
Ubomoaji nyumba hizo ulioanza juzi wilayani Temeke na jana kufuatiwa na Kinondoni, unafanywa kwa kuzingatia tamko namba 6.6 la Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 linalosema: “Serikali itahakikisha kwamba maeneo yote mijini yaliyotengwa kwa shughuli za umma yanatumika kwa shughuli zilizokusudiwa na yalindwe ili yasivamiwe.”
Vilevile, ni utekelezaji wa tamko namba 8.2.1 la Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 linalosema: “Serikali za mitaa zitawajibika kushirikiana na Wizara ya Ardhi kuhakikisha usimamizi mzuri wa ardhi katika maeneo yao.”
Inasikitisha kuona watu wanabomolewa nyumba zao za kuishi au za biashara walizojenga baada ya kuhangaika kwa miaka mingi kutafuta fedha, lakini tunadhani hiyo ndiyo dawa pekee dhidi ya watu wasiotaka kufuata sheria na taratibu zilizopo au wenye kiburi cha fedha.
Kwa miaka mingi, maeneo ambayo ramani za mipango miji zinaonyesha yametengwa ama kwa ajili ya viwanja vya michezo au mapumziko, upanuzi wa shule au hospitali au majengo ya Serikali, tumeshuhudia yakivamiwa na wenye fedha. Maeneo hayo zimejengwa nyumba za kuishi na mengine shughuli za biashara.
Pia, tumeshuhudia wenye fedha wakipora na kujenga nyumba katika maeneo ya hifadhi ya barabara na pengine juu ya mabomba ya maji na mafuta. Mbaya zaidi wapo ambao kwa jeuri ya fedha wamethubutu hata kuziba mifereji inayopitisha maji machafu na hivyo kusababisha adha kubwa kwa wakazi wengine kwani majitaka husambaa ovyo na hata kuingia kwenye majumba ya watu mvua zikinyesha.
Tunapongeza uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kusimamia sheria zilizopo za mipango miji kwa kuamua siyo tu kutangaza kiama kwa waliojenga nyumba katika maeneo yasiyoruhusiwa, bali pia kubomoa na hivyo kutoa onyo kwa wengine.
Kitu ambacho hatuna uhakika nacho ni ikiwa usimamizi wa sheria na sera ya mipango miji utakuwa endelevu. Mpaka sasa waliobadilika katika Serikali hii ni viongozi wa juu, watendaji katika halmashauri ni walewale ambao wanaona mtu akivamia eneo, anachimba msingi, anajenga nyumba, lakini hawahoji.
Baada ya nyumba kukamilika na watu kuhamia ndipo inatolewa amri ya kubomoa nyumba hiyo. Kwa nini udhibiti haufanyiki tangu siku ya kwanza mhusika anaposafisha eneo hilo?
Mbali ya baadhi ya watendaji kufumbia macho ukiukwaji wa sheria, labda kwa sababu ya rushwa, pia wapo wengine waliotoa vibali. Tumeshuhudia Serikali inapotaka kubomoa nyumba hizo imekuwa ikikwama kwa vile wahusika hukimbilia kuomba zuio la mahakama.
Tunashauri baada ya kukamilika kwa mchakato huu wa kurejesha maeneo yote ya umma yaliyovamiwa, wote waliohusika kutia saini kuidhinisha hati za umiliki wa viwanja na ujenzi katika maeneo yasiyoruhusiwa wawajibishwe maana hao ndio waliofanikisha ukiukwaji wa taratibu.
Kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu” iendane na kuwaondoa watumishi wasio waadilifu na ambao ndiyo kiini cha operesheni hii itakayotumia gharama kubwa kwa sababu ya watu walioamua kutumia vibaya madaraka yao.