Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tushirikiane kukomesha uchimbaji huu

Vijana hao ni sehemu ndogo sana ya vijana wengi waliotapakaa kwenye mabonde kadhaa jijini Dar es salaam na maeneo mengine nchini ambao wanachimba mchanga kwa ajili ya kuuza na kujipatia riziki.PICHA|MAKTABA

Muktasari:

Sote ni mashuhuda wa madhara makubwa ambayo yanaonekana wakati huu wa mvua za masika.

Siyo siri kwamba tatizo la uharibifu wa mazingira, ukiwamo uchimbaji holela wa mchanga katika maeneo mbalimbali nchini, hasa katika miji mikubwa, limekithiri.

Katika toleo letu la juzi (Mei 21), ukurasa wa pili, tulichapisha picha ya vijana waliokuwa chini ya daraja la Ubungo jijini Dar es salaam wakichimba mchanga kwa ajili ya kuuza kwa watu wanaoutumia kwa shughuli za ujenzi na nyinginezo.

Vijana hao ni sehemu ndogo sana ya vijana wengi waliotapakaa kwenye mabonde kadhaa jijini Dar es salaam na maeneo mengine nchini ambao wanachimba mchanga kwa ajili ya kuuza na kujipatia riziki.

Kwa bahati mbaya, uchimbaji huo ni uharibifu wa mazingira kwa kuwa hauzingatii taratibu na hivyo kuwa tishio kwa ardhi nzuri na inayofaa kwa matumizi ya maendeleo na kwa miundo mbinu ya usafiri ambayo imejengwa kwa mabilioni ya fedha.

Matokeo yake, kila mvua zinaponyesha madhara yamekuwa makubwa, kiasi cha kuhitaji hatua za makusudi za kukabiliana nalo ili kuepuka majanga zaidi yanayoweza kusababishwa na hali hiyo.

Kwa kiasi kikubwa mvua zinazoendelea kote nchini zimeacha kingo za mito zikiwa hoi, madaraja mengi yameathirika mashikio au msingi wake kiasi cha kutofaa kutumika tena kama hakutakuwa na ukarabati mkubwa.

Sote ni mashuhuda wa madhara makubwa ambayo yanaonekana wakati huu wa mvua za masika.

Tunadhani, ipo haja ya kila mmoja wetu kuona ukubwa wa tatizo hilo na athari zake kwa jamii yetu na hivyo kushiriki kwa kuchukua hatua za makusudi katika kukabiliana na tatizo hili linalozidi kuongezeka mijini na vijijini.

Tunasema kuna haja ya kila mwananchi kuliona tatizo hilo kwa kuwa tunajua kuwa tunajua kuwa mwananchi ndiyo serikali ya kwanza ya kuweza kulidhibiti tatizo hilo kabla ya mamlaka za nchi kutumia uwezo wake kupambana nalo.

Kwa mujibu wa mfumo wa utawala, uongozi huanzia kwenye ngazi za nyumba kumi, ambako wananchi wanayajua maeneo yao vizuri na wanajua wanaoshiriki kuchimba mchanga na kuuza na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na miundombinu.

Ni vizuri basi kwa wananchi kushirikiana na viongozi wao wa kuanzia ngazi hiyo kuhakikisha maeneo yao yanatunzwa na kulindwa ili yasiwe tishio kwa maisha yao ya baadaye.

Taasisi za kiraia ambazo zinajishughulisha na mazingira na zile zinazoshughulikia haki za ardhi, pia zina wajibu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhakikisha wanaelewa vizuri wajibu wao katika masuala hayo badala ya kusubiri matatizo yatokee ndipo zijitokeze kulaani.

Lakini juhudi za kufanikisha azma hiyo haziwezi kufanikiwa kama serikali itakaa kando na kusubiri kuchukua fedha za mirabaha kwa wasafirishaji wa mchanga na madini mengine ya ujenzi.

Serikali ndiyo ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa inashirikiana na wananchi katika kukabiliana na tatizo hilo kwa kupanga maeneo ya uchimbaji mchanga ili kuondoa uchimbaji holela na pia kutoa elimu na kuwashughulikia kisheria wote wanaoharibu mazingira kwa kufanya shughuli za uchimbaji kiholela katika mito, makazi na mabonde.

Kufanya kazi kwa operesheni au zimamoto hakuwezi kusaidia kuliondoa tatizo hilo, bali kwa kuwa na mfumo bora wa kuhakikisha wavunjaji wa sheria zinazohusu mazingira wanadhibitiwa kwa hali na mali.