Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Singeli haitopanda ndege ikifuata nyayo za mnanda, mchiriku

Muktasari:

Usemi huo unarandana na muziki wa Bongofleva, ambao ulianza kwa kukosolewa na baadhi ya watu ambao walikuwa wakiamini kwa asilimia 100 kuwa ulikuwa ni wa vijana wahuni na wavuta bangi.

Kuna msemo usemao “Toto baya ndilo linalokua”. Ukiwa na maana jambo lolote ambalo huanza kwa kunyooshewa vidole vya ubaya na kupingwa vikali huwa na kawaida ya kudumu na kufika mbali.

Usemi huo unarandana na muziki wa Bongofleva, ambao ulianza kwa kukosolewa na baadhi ya watu ambao walikuwa wakiamini kwa asilimia 100 kuwa ulikuwa ni wa vijana wahuni na wavuta bangi.

Wapo ambao hawakuwahi kuwa na ndoto ya kuiona Bongofleva ikifika ilipo leo, wengi waliamini kwamba ni muziki usiofaa na hata vijana wao walipojaribu kuwaambia kuwa wanaingia katika fani ya muziki huo, waliwakataza kwa kuwaona wanapotoka.

Lakini leo hii Bongo Fleva imekuwa ajira, tena ile inayoingiza kipato kikubwa kwa msanii ukilinganisha na kijana aliyeajiriwa ofisini hata kama analipwa mshahara wa juu kiasi gani.

Leo hii muziki wa Bongo Fleva, umekuwa miongoni mwa nembo za Taifa, unaitambulisha nchi na kuitangaza katika mataifa mbalimbali na hata kuvizidi vivutio mbalimbali vilivyopo ndani ya nchi.

Wakati Bongo Fleva ikishika hatamu hivi sasa imeibuka Singeli, muziki ambao umejichukulia umaarufu na kuwa gumzo katika kila kona ya nchi.

Mpenda muziki gani Tanzania utakayemuuliza kuhusu “Hainaga Ushemeji ” ya Man Fongo na akakwambia haifahamu au yuko wapi ambaye utampa habari za Msaga Sumu na akabaki na kigugumizi asijue unazungumzia nini?

Kwa kifupi, inapofikia hatua hata msanii mkubwa kama Profesa Jay anapofanya muziki wa aina hii, inatosha kushindwa kujizuia kunyoosha mikono juu, kusalimu amri na kukiri kuwa Singeli imeshinda vita ya ndani.

Lakini hali halisi ilivyo, inaonyesha kuwa muziki wa Singeli ni ‘Toto Baya’ zaidi ya ilivyokuwa Bongo Fleva. Na inawezekana hata asilimia 90 ya watu waliopata bahati ya kuusikiliza muziki huu wanashindwa kukataa kwamba wanamuziki wake huvuta bangi kabla ya kuingia studio kurekodi. Sikiliza kwa makini kinachoimbwa kwenye nyimbo zao utabaini kitu.

Achilia mbali wanamuziki, hata asilimia kubwa ya mashabiki wa Singeli unapowatazama, wanakuwa na hulka za ajabu pindi wanaposakata rhumba la Singeli, mtu anayecheza muziki na panga kibindoni, unaweza ukamuelezea vipi kwa mfano?

Sababu za aina hiyo hazina tofauti na zile zilizoumaliza mchiriku na mnanda, aina ambazo kama zingepata wasanii wenye kujua thamani ya sanaa wanayoifanya basi pengine leo hii tusingekuwa tunamuongelea Diamond na ‘Afropop’ yake labda na yeye angekuwa anaimba kama au zaidi ya alivyokuwa marehemu Omary Omary.

Mchiriku na mnanda lilikuwa ‘Toto Baya’ lililoshindwa kukua kwa sababu lilishindwa kuthibitisha kwamba lilikuwa toto zuri. Kwa kipindi kile, kila ulipokuwa ukipigwa muziki wa Mchiriku basi eneo hilo litageuka kuwa maskani ya kuvutia bangi usiku mzima na lazima kesho yake ungesikia watu wakilalamika kuvunjiwa nyumba zao, kuporwa au hata kukabwa.

Ukirudi kwa Singeli, wenyewe ni muziki unaofanana vionjo na mchiriku, muziki wenye ladha ya Kiafrika kwa asilimia 100 jambo ambalo linaweza kuwa ni pointi ya msingi katika kuuwezesha kufanya vizuri kimataifa.

Huu ndiyo muda mwafaka wa wasanii na wadau wa muziki wa singeli kuhakikisha haupiti njia za mnanda na mchiriku. Wasanii wahakikishe kwamba wanaimba vitu vya maana na siyo pumba kwa wingi kama wengi wao wanavyofanya sasa hivi, lakini pia wadau wanatakiwa kuhakikisha wanautengenezea muziki huu mashabiiki wenye taswira nzuri kwa jamii ili kuendelea kuupa uhai na thamani zaidi.

Kucheza na mapanga na nyembe kwenye mifuko ya shati ni ‘ushamba wa mwendokasi’.

0713 482816