Kikosi cha Zimamoto ni dhaifu, hakitufai

Muktasari:
Hapa nchini hakuna mtu ambaye hajaguswa na matukio hayo kwa namna moja ama nyingine. Kwa muda mrefu sasa, Kikosi cha Zimamoto nchi nzima kimeendelea kutia
Moto mkubwa ulioteketeza bidhaa za mabilioni ya fedha katika maghala ya Kampuni ya Sunda, jijini Dar es Salaam juzi, yamethibitisha hofu iliyotanda nchi nzima hivi sasa kwamba udhaifu uliopo katika Kikosi cha Zimamoto nchini ni ishara tosha kwamba Serikali imeshindwa kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao.
Katika tukio hilo la juzi, ambalo tunaweza kusema limeifadhaisha Serikali kwa kiasi kikubwa, magari zaidi ya 20 ya vikosi vya Zimamoto na Uokoaji vya taasisi mbalimbali vilishindwa kuzima moto huo ulioanza juzi asubuhi na kuendelea hadi mchana wa siku iliyofuata.
Hapa nchini hakuna mtu ambaye hajaguswa na matukio hayo kwa namna moja ama nyingine. Kwa muda mrefu sasa, Kikosi cha Zimamoto nchi nzima kimeendelea kutia kichefuchefu kutokana na kushindwa kutokea mapema katika matukio ya moto. Mara nyingi magari ya kikosi hicho yamefika katika matukio hayo bila kuwa na maji, huku yakiwa yamechelewa sana na kukuta mali zote zikiwa zimeteketea.
Tunapata shida kuelewa sababu zinazoifanya Serikali ishindwe kuboresha huduma za kikosi hicho, mbali na kila mwaka kutoa hotuba tamu bungeni ikiwahakikishia wananchi kuwapo kwa mikakati ya kukiboresha. Lakini miundombinu imeendelea kuwa mibovu, kwa maana ya kikosi hicho kutoweza kufika kwa urahisi katika sehemu za matukio ya moto.
Mipango ya Serikali ya kupanua huduma za kikosi hicho katika miji yetu imebaki katika makabrasha. Jijini Dar es Salaam ambako matukio ya moto ni jambo la kila siku, Serikali imeshindwa kuhakikisha inafungua vituo vya Zimamoto katika sehemu nyingi za mkoa huo muhimu. Misururu ya magari inaendelea, hivyo magari ya Zimamoto yanashindwa kupenya kuwahi kwenye sehemu za matukio.
Tunaitaka Serikali ione umuhimu wa kuboresha Kikosi cha Zimamoto. Kwanza itandaze mabomba ya maji ili vikosi hivyo vipate maji hayo karibu na maeneo ya matukio ya moto. Askari wa kikosi hicho wanahitaji mafunzo na vifaa vya kisasa, ikiwa pamoja na vituo vyao kuwa na huduma za mawasiliano ya uhakika.
Badala ya kuwa mtazamaji tu huku matukio ya moto yakisababisha vifo vya watu na kuharibu mali za mabilioni, Serikali sasa izinduke na kuonyesha njia. Tunashauri kwamba katika mipango miji Serikali itoe kipaumbele kwa vituo vya Zimamoto kama ilivyo kwa vituo vya Polisi, afya, masoko na kadhalika. Ili uwepo ufanisi, Serikali ifikirie uwezekano wa kubadilisha mfumo wa kikosi hicho cha Zimamoto ambao ndio moja ya vikwazo vinavyoathiri ufanisi wake.