Wanahabari rekebisheni mambo haya

Vyombo vya habari ni mifumo na nyenzo zinazofanya kazi ya kukusanya, kuandika, kuhariri, na kuripoti taarifa zenye umuhimu na sifa ya kuwasilishwa kwa umma, yaani habari.
Taarifa ili kupata hadhi ya kuwa habari, inapaswa kuwa na sifa mbalimbali, ikiwemo kuwa ya ukweli na iwe na umuhimu wa kuwasilishwa kwa umma.
Pia, taarifa husika inapaswa kuhusiana na mambo yaliyotokea karibuni na iwe kamili kwa kuhusisha pande zote zinazotajwa (siyo ya upande mmoja).
Vyombo vya habari vyote vina jukumu muhimu la kutoa taarifa (habari), elimu na burudani katika jamii.
Pia, kutokana na nafasi na umuhimu wa vyombo vya habari katika jamii, vina ushawishi mkubwa katika maendeleo na mustakabali wa nchi.
Tanzania ni nchi inayoendeshwa kwa misingi ya kidemokrasia, ndiyo maana kupitia ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania imetoa ithibati ya uhuru wa kujieleza kwa kila mwananchi pasipo kuingiliwa.
Mbali na hilo, Tanzania kwa kutambua nguvu na ushawishi mkubwa wa vyombo vya habari, iliamua kuunda vyombo mbalimbali vya kusimamia shughuli za habari nchini, ikiwemo: Wizara ya Habari, Baraza la Habari Tanzania na Idara ya Habari - Maelezo.
Navipongeza vyombo vya habari nchini kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya kuhabarisha umma ipasavyo. Ila Waswahili hunena “kizuri hakikosi kasoro”.
Mbali na kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari nchini, kuna mambo yanafanywa na vyombo hivyo, ambayo kimsingi yanafifisha nafasi na mchango wa vyombo vya habari nchini.
Mosi, kumekuwa na uwasilishaji wa maudhui ya kikubwa yanayohusiana na mambo ya kimahaba, ambapo baadhi maudhui hayo yamekuwa yakiwasilishwa katika majira ya mchana, kitu ambacho ni kinyume na “Kanuni za Huduma za Utangazaji (2018)” zilizotungwa chini ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari (2016).
Kanuni hizo zinaelekeza maudhui ya kiutuuzima yenye mrengo wa mahaba, yanatakiwa kuwasilishwa kwa umma kuanzia saa tatu usiku, wakati ambapo inadhaniwa watoto wengi wamelala.
Cha kushangaza baadhi ya vyombo vya habari, hasa vya kimtandaoni vimekuwa vikitangaza maudhui ya kiutuzima au vimekuwa vikiongelea mambo ya kimahaba katika muda ambao haujaelekezwa na mamlaka husika.
Kitu ambacho kinakiuka kanuni, kadhalika kinawapa nafasi watoto kusikiliza vitu vilivyo juu ya umri wao. Pia, kutokea kwa jambo hili mbali na kuvunja kanuni za maadili ya habari, vilevile kunavunja miiko ya utamaduni wa Mtanzania.
Pili, kumekuwa na utamaduni kwa baadhi ya wanahabari pindi wanapofanya mahojiano na watu mbalimbali, kutowapa uhuru wa kuzungumza.
Unakuta mwanahabari anamuuliza swali mhojiwa, kipindi mhojiwa anajibu swali husika hapohapo mwanahabari anamkatisha ama kwa kuuliza swali lingine au kuchomekea kitu kingine kipya.
Hii inamnyima mhojiwa uhuru wa kuzungumza. Kutokea kwa jambo hilo kunakofanywa na wanahabari ni kinyume kabisa na sheria na maadili yanayoongoza vyombo vya habari nchini.
Tatu, baadhi ya wanahabari wamekuwa na tabia ya kuzungumzia mambo yao binafsi pindi wawapo hewani katika vipindi mbalimbali ndani ya vyombo vya habari. Jamii inaamini kuwa, wanahabari ni watu wanaoaminika kutokana na kufuatilia na kuhabarisha matukio yanayojitokeza katika jamii.
Ila cha kushangaza, katika vipindi mbalimbali vinavyorushwa hewani, hasa vya redioni, baadhi ya wanahabari wamekuwa wakizungumzia mambo yao binafsi, ambayo kimsingi hayana tija kiuhabarishaji, yaani hayana sifa au umuhimu wa kuwasilishwa kwa umma.
Kadhalika, wanahabari wengine wamefikia hatua ya kupiga soga kabisa, soga ambazo hazina afya kiuhabarishaji na kujisahau kwamba wapo hewani na wanasikilizwa na wananchi.
Napendekeza kufanyika kwa mambo yafuatayo ili vyombo vya habari nchini viondokane na changamoto zilizobainishwa.
Mosi, vyombo vya habari vizingatie sheria, kanuni, na maadili yanayoongoza uhabarishaji, ikiwezekana wajidhibiti kabla ya kudhibitiwa.
Pili, mamlaka za habari na mawasiliano, ikiwemo TCRA na Baraza la Habari Tanzania (MCT) ziendeshe kozi za mafunzo ya mara kwa mara kwa wanahabari, ili wanahabari wawe na weledi katika kuripoti masuala ya kihabari kwa uangalifu na kwa kuzingatia maadili ya jamii.
Tatu, jamii iwe macho kwa watoto na vijana dhidi ya maudhui yasiyofaa kwa kutumia mbinu mbalimbali, ikiwemo kwa kutumia teknolojia za udhibiti wa wazazi (parental control settings).
Nabil ni mwanasafu katika gazeti la Mwananchi na mtaalamu wa lugha ya Kiswahili. 0621229465.