Walimu, wanafunzi tumieni likizo kupumzika

Joseph Gatahwa
Muktasari:
- Ni muda wa likizo kwa wanafunzi na baadhi ya walimu. Walimu wana utaratibu tofauti wa likizo. Hata hivyo ukweli ni kwamba wote wako likizo.
- Likizo maana yake ni mapumziko. Ni muda wa kupumzisha akili na mwili kwa ajili ya kujiandaa na muhula wa masomo unaofuata.
Mwezi huu wa sita shule zote za msingi na sekondari hapa nchini zimefungwa, baada ya kumalizika muhula wa kwanza wa masomo.
Ni muda wa likizo kwa wanafunzi na baadhi ya walimu. Walimu wana utaratibu tofauti wa likizo. Hata hivyo ukweli ni kwamba wote wako likizo.
Likizo maana yake ni mapumziko. Ni muda wa kupumzisha akili na mwili kwa ajili ya kujiandaa na muhula wa masomo unaofuata.
Lakini siku hizi, shule zinapofungwa, bado tunashuhudia harakati za wanafunzi katika vituo na shule mbalimbali za msingi na sekondari wakiendelea kusoma.
Kwa jinsi hali inavyojionyesha ni kama shule zinabadilisha ratiba au utaratibu wa masomo. Badala ya kuamka asubuhi mapema, saa 11 au 12 asubuhi na kuvaa sare rasmi za shule, sasa huamka wakiwa wamechelewa pasipo sare na utawaona wakienda na kurudi kutoka katika vituo vya twisheni.
Wazazi nao kwa upande wao huwatafutia watoto wao walimu wa kuwafundisha nyumbani au katika vituo vya masomo. Huingia gharama nyingine za kuwalipia watoto wao masomo ya ziada.
Hali hii imeshakuwa ni kama utaratibu rasmi katika jamii yetu. Dhana ya likizo kuwa mapumziko haipo tena.
Hata hivyo, pamoja na utaratibu huu wa twisheni ulioshamiri, bado umuhimu wa kupumzika uko palepale kwa wanafunzi na walimu.
Kwa wanafunzi, ni vema wakati wa likizo ukatumika kukuza vipaji vyao na kujifunza vitu tofauti na vilivyo nje na mtalaa rasmi. Kwa mfano, wanaweza kusoma vitabu vya hadithi na vya fani au ujuzi mbalimbali kulingana na mapenzi yake.
Pia, kama mwanafunzi ana kipaji cha mchezo fulani, au sanaa ndio muda mwafaka wa kujiendeleza na kipaji chake husika.
Wakati wa likizo pia ndio muda wa kufanya utalii wa ndani kwa mwanafunzi na hata mwalimu. Utalii wa ndani sio lazima kwenda katika mbuga za wanyama. Kitendo cha kwenda kuwatembelea ndugu na jamaa ni namna ya kufanya utalii na kujifunza kwa kujionea mandhari tofauti na alivyozoea.
Kwa walimu, muda wa likizo kwao pia ni muda wa kupumzika. Kwao muda huo ndio mwafaka kwa kushughulikia dharura za kifamilia na za kibinafsi.
Aidha, ni muda wa kujiongezea maarifa kuhusiana na kazi yake ya ualimu kwa kusoma vitabu vinavyohusika na taaluma hiyo.
Ni kipindi mwafaka kwa mwalimu kuandaa zana za kufundishia na kujifunzia.
Ni muda sahihi kwa shule, taasisi na Serikali kuendesha programu za mafunzo kwa walimu kwa lengo la kuongeza ujuzi na maarifa ya ufundishaji
Ni muda pia wa kufanya tathmini ya matokeo ya ufundishaji wao kutokana na matokeo ya wanafunzi katika shule, chuo, taasisi, wilaya au mkoa ili kupanga mikakati mipya.
Vitendo kama hivyo, ni motisha pia kwa walimu kuliko kuwalazimisha kubaki vituoni kuendelea na ufundishaji.
Faida ya kupumzika ni kwamba mwanafunzi au mwalimu anaupumzisha mwili au akili yake. Wakati wa kufungua shule hurudi akiwa na hamu na hamasa ya kujifunza na kufundisha.
Madhara ya kusoma au kufundisha mfululizo hadi wakati wa likizo yapo ingawa hatuwezi kuyaona kirahisi.
Mwanafunzi hudumaa katika kujifunza na mwalimu hukinai au huchukia kazi.
Kudumaa kwa mwanafunzi ni akili kuchoka na kushindwa kutunza kumbukumbu. Matokeo yake mwanafunzi kufeli hata mtihani rahisi.
Mwalimu aliyechoka pia hupunguza morali wa kazi na kushindwa kuwa mbunifu katika kazi yake.
Joseph Gatahwa ni mwalimu kitaaluma. 0785909051