Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vituo vya kulelea watoto mchana sio anasa

Katika ulimwengu wa sasa ambapo maisha yanahitaji juhudi kubwa ili kupata kipato cha kila siku, wazazi wengi wamejikuta katika hali ya kutafuta njia bora ya kuwalea watoto wao huku wakiendelea na shughuli zao.

Mojawapo ya suluhisho muhimu ni vituo vya kulelea watoto mchana, maarufu kama daycare. Hata hivyo, upatikanaji wa vituo na gharama kubwa ya huduma hizi imekuwa kikwazo kwa familia nyingi hasa maeneo ya pembezoni kama nilivyoshuhudia hivi karibuni mkoani Kigoma.

Hivi karibuni nilitembelea katika kijiji cha Bubangu kilichopo kata ya Bitale mkoani Kigoma, nikiwa njiani nilikutana na mama anaenda shamba akiwa na watoto wawili.

Mtoto wa miaka miwili alimbeba mgongoni na mwingine wa miaka minne anatembea, kilichonisogeza kuzungumza naye ni namna alivyokuwa akihangaika kumvuta huyu mtoto anayetembea ambaye alikuwa analia.

Nilipomuuliza kwanini mtoto analia akajibu hataki kwenda shamba, nikamhoji tena mtoto wa umri huo anaenda kufanya shughuli gani shambani akasema hana anachofanya ila ni salama zaidi akiwa naye shambani kuliko kumuacha nyumbani.

Nilipotaka kujua kama anapoishi kuna kituo cha kulelea watoto wakati wa mchana akasema hakuna na kutokana na utundu wa watoto wake hawezi kuwaacha nyumbani peke yao.

Kisa kingine kinachofanana na hicho nilikutana nacho katika soko lililo jirani na hospitali ya Maweni, mama muuza mitumba alikuwa na mtoto wake wa miaka mitatu.

Nilipotaka kujua sababu za mtoto huyo kuwa sokoni alijibu hana mtu wa kumuachia nyumbani na hana uwezo wa kulipia gharama za kituo cha kulelea watoto ambacho pia kipo mbali na eneo analoishi.

Katika halmashauri ya wilaya ya Kigoma yenye jumla ya kata 16 kuna vituo vitano vya kulelea watoto na vyote vinamilikiwa na watu binafsi.

Kwa mujibu wa ofisa ustawi wa jamii wa halmashauri hiyo Saada Amani licha ya uchache wa vituo hivyo bado watu wengi wanashindwa kuwapeleka watoto kwa sababu wanashindwa kulipia gharama zinazotozwa.

“Gharama zao sio kubwa ila kutokana na hali ya uchumi wa watu wengi katika maeneo yetu wapo wanaoshindwa kumudu licha ya kuwa na uhitaji mkubwa wa sehemu salama ya kuwaacha watoto wao walelewe wakati wao wanahangaika na shughuli za kuwaingizia kipato,”anasema.

Anachosema ofisa ustawi wa jamii huyo hakina tofauti na uhalisia wa hali ilivyo katika maeneo mengi hasa ya pembezoni ambapo wazazi wanalazimika kuwaacha watoto sehemu zisizo salama kwasababu hakuna vituo vya malezi au wanashindwa kumudu gharama.

Nafikiri Serikali ina wajibu mkubwa katika kuhakikisha kwamba huduma hizi zinapatikana kwa urahisi na bila mzigo mkubwa wa kifedha kwa wananchi.

Kwa kushirikiana na sekta binafsi, serikali inaweza kutoa ruzuku au punguzo la kodi kwa wamiliki wa vituo wanaotoa huduma kwa gharama nafuu. Hatua hii itawavutia wawekezaji wengi kuanzisha vituo vipya na kuongeza ushindani, hali itakayopunguza gharama kwa wazazi.

Serikali pia inaweza kushirikiana na jamii katika kuanzisha vituo vya kulelea watoto vinavyoendeshwa na jamii yenyewe. Katika mpango huu, wanajamii wanaweza kuchangia kwa njia ya kazi, vifaa, au fedha kidogo ili kuweka mazingira salama ya kulea watoto wao.

Hii ni njia endelevu na ya gharama nafuu ambayo pia huimarisha mshikamano wa kijamii kwa kuwa kuwepo kwa vituo vya kulelea watoto mchana bila gharama kubwa si tu kutasaidia wazazi kiuchumi, bali pia kutachangia katika maendeleo ya kijamii na kielimu kwa watoto.