UCHAMBUZI: Uchakavu wa nyasi kwa Mkapa fedheha

Alipokuwa akiwakilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo ya mwaka wa fedha 2022/23, Waziri Mohammed Mchengerwa aliomba Bunge liidhinishe Sh35.4 bilioni ikiwamo Sh10 bilioni kwa ajili ya kukarabati viwanja saba vya michezo.

Viwanja hivyo ni Jamhuri (Dodoma), Sheikh Amri Abeid (Arusha), Sokoine (Mbeya), CCM Kirumba (Mwanza), Mkwakwani (Tanga), Uhuru na Benjamin Mkapa vya jijini Dar es Salaam.

Katika ukarabati huo, viwanja vitano vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) na viwili cha Uhuru na Benjamin Mkapa ni vya Serikali.

Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa sasa ndiyo uwanja mkubwa na wa kisasa kulinganisha na vingine vyote vilivyopo nchini, ulijengwa wakati wa utawala wa awamu ya tatu, una uwezo wa kubeba watu 60,000 waliokaa kwenye viti.

Katika bajeti hiyo, waziri Mchengerwa aligusia pia kuwekwa vifaa vya kisasa vya mazoezi (gym) kwenye Uwanja huo ingawa kwa namna ulipofikia sasa unahitaji ukarabati mkubwa.

Ukiachana na mazingira ya majukwaa, vyumba vya kubadilishia nguo, vyooni na mazingira mengine ya uwanja huo ambayo yanahitaji ukarabati.

Eneo jingine linalohitaji ukarabati ni kapeti la kukimbilia ‘Tartan’ za uwanja wa Benjamin Mkapa ambao kwa muda mrefu limechoka.

Kapeti hilo wakati wa jua linayeyuka na unapolikanyanga unakuwa kama umepita kwenye gundi au tope, hivyo kama hauko makini linaweza pia kusababisha uteleze na kudondoka.

Hilo ndilo kapeti ambalo ni uwanja maalumu kwa ajili ya riadha, kapeti ambalo haliendani na hadhi ya uwanja huo kwa sasa.

Serikali ikiona vyema, kuliko kukarabati viwanja vitano vya CCM, bajeti hiyo ambayo imechangiwa na kodi za wananchi, bora ingetupia jicho la kubadilisha ‘tartan’ za uwanja huo ambao ni wao.

Tunapoendelea kuzitumia tartan hizo, kwanza tunahatarisha hata afya za wanamichezo wanaozitumia, kwani siku zinaweza kusababisha janga jingine, mchezaji akateleza na kuumia.

Lakini pia zinaondoa ule ubora wa uwanja wetu, unakosa hadhi ile ya kuwa miongoni mwa viwanja bora Afrika Mashariki.

Kama haitoshi, unadhihirisha kwamba uwanja huo sasa umekosa matunzo, na hiyo inaangazia vitu vingi, mfano ni majukwaa hasa ya mzunguko wa orange na bluu, viti vingi vimeng’oka.

Uwanja una ‘mapengo mapengo’ kwenye majukwaa, achilia mbali uchakavu mwingine, kabla haijafikia hatua mbaya zaidi, Serikali ione ni namna gani inauboresha kwa kiwango bora na si kuziba ‘viraka’ kama ambavyo imekuwa ikifanya kwenye uwanja wa Ndani wa Taifa.

Tunafahamu mikakati wa Serikali kwenye suala la miundo mbinu ya michezo ambayo Bungeni Dodoma, waziri Mchengerwa alikaririwa akisema ni tatizo sugu ambalo wanalishughulikia.

Wakati wakiendelea kukamilisha miradi ya kihistoria ambayo inakwenda kufanyika kwenye sekta ya michezo, kuna haja ya kuumurika kwa upana uwanja wa Benjamin Mkapa, uchakavu wake unatia aibu.

Inaonyesha dhahiri uwanja huo umekosa matunzo, ule mvuto, ubora na muonekana wake unatoweka kwa uchakavu.

Hata mazingira yake ya usafi pia si rafiki, kifupi unahitaji ukarabati wa kiwango kikubwa ili kuurejesha kwenye hadhi yake.

Kama mchezo wa juzi, wakati Simba ikiikaribisha Coastal Union kwenye mchezo wa hatua ya mtoano ya timu 32 za Kombe la FA (ASFC), waliokuwa uwanjani waliona nini ambacho kinaonekana kwenye uwanja wao mkubwa nchini katika upande wa soka na riadha.

Lakini hata waliokuwa nyumbani kufuatilia kupitia runinga watakubaliana na mimi kuwa kuna mambo mengi yanafanyika katika nyasi, kitu ambacho si msaada katika utunzaji.

Ni kweli kwamba ni uwanja wa Serikali, lakini ulitengenezwa kwa dhumuni kubwa la michezo ya soka. Kinachoendelea katika michezo nje ya soka inayofanyika katikati ya uwanja kinatoa majibu moja kwa moja kwa umma.

Hatuwezi kuipangia Serikali nini cha kufanya katika uwanja wanaoumiliki wenyewe, lakini ni vizuri wakazingatia tenda wanazopokea kama zinaweza kutunza miundombinu.

Lakini yote kwa yote, kila mmoja ana nafasi ya kuutunza uwanja kwa njia moja ama nyingine. Kwa upande wangu nimeamua kulisemea hili kama njia mojawapo, kwamba wahusika wanatakiwa kuangalia kitu gani kinafaa kwa ajili ya kuendelea kuwa na uwanja bora.

Lakini kwa matamasha yanayoharibu nyasi na kisha tutarajie kesho yake tutazame mchezo wa soka kwenye uwanja huo huo itakuwa kitu kigumu mno.