Tusikubali watoto kusoma chini ya miti

Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa
Tumeguswa na kauli aliyoitoa juzi Waziri Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa, akishangaa kuwapo kwa baadhi ya shule ambazo wanafunzi wake wanasomea chini ya mikorosho.
Alisema hilo aliliona katika ziara aliyofanya mkoani Mtwara na kushangaa kuwa licha ya halmashauri kupokea fedha za maendeleo, zipo shule zisizo na vyumba vya madarasa.
Kwetu sisi, uwepo wa shule ambazo wanafunzi wanasoma chini ya miti nchini, ni suala linalohitaji kuangaliwa kwa undani na kulitafutia ufumbuzi wa haraka na wa kudumu.
Tunaamini Serikali yetu ina jukumu la kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu katika mazingira bora, salama na yenye kufaa. Kuwa na shule ambazo bado zinatumia madarasa ya miti zama hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia, ni kielelezo cha udhaifu katika mipango ya maendeleo ya elimu, na ni jambo linalowaumiza watoto, wazazi na jamii kwa jumla.
Kama alivyosema Mchengerwa, shule hizi ni alama ya ukosefu wa usimamizi na uwajibikaji katika sekta ya elimu, ndiyo maana mbali na hatua nyinginezo za kiutumishi, wale wanaobainika kutufikisha katika hatua hii ya aibu ikiwezekana wafunguliwe milango. Hatuwezi kuwa na watendaji walio tayari kuhonga mamilioni, kama alivyoeleza waziri, ili waonekane wanawajibika ilhali wanashindwa kutekeleza mambo ya msingi, ikiwamo kusimamia maendeleo ya elimu.
Sisi hatudhani kama Serikali haina rasilimali za kujenga vyumba vya madarasa, tena vya kisasa. Ni lazima kuna changamoto mahali.
Kuendelea kutumia madarasa ya miti ni aibu kwa Serikali, ambayo ina rasilimali zinazoweza kutumika kwa kuboresha hali ya shule na kuandaa mazingira bora kwa watoto wa kizazi hiki. Vyumba hivi vina madhara makubwa.
Wanafunzi hawa hawawezi kupata elimu bora kwa sababu wanakosa mazingira tulivu na ya kisasa, ambayo ni muhimu kwa ustawi wao kimaisha na kitaaluma.
Pili, hali hii inahatarisha usalama wa wanafunzi. Wanafunzi wanaosoma chini ya miti wanakutana na changamoto nyingi.
Kwa mfano, mvua ikinyesha au jua kali linapokuwapo, wanafunzi hawa wanakosa ulinzi wa kutosha. Pia, katika baadhi ya maeneo, mvua, upepo au radi vinaweza kuleta madhara kwa wanafunzi, kuathiri usalama wao na hata afya zao.
Ni wazi kuwa Serikali inapaswa kutoa kipaumbele katika kuhakikisha kuwa mazingira ya shule ni salama na ya kuvutia ili wanafunzi waweze kufurahia na kujivunia elimu wanayoipata.
Kwa wasichana hali ni mbaya zaidi, kwa kuwa wanakutana na changamoto za ziada kutokana na mazingira magumu, kama vile ufinyu wa nafasi na kukosa faragha.
Wakati wa mvua, wanafunzi hawa wanakosa mahali pa kubadilisha mavazi au kujificha kutokana na mazingira yanayokosekana ya kujikinga. Hii inachangia kupunguza uthubutu wa wasichana katika kuendelea na masomo yao na hivyo kuchangia kuongezeka kwa viwango vya matokeo duni na hata mdondoko kwao.
Shule zinazotumia miti kama madarasa ni kikwazo cha maendeleo. Elimu bora ndiyo msingi wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Kama taifa, tunapaswa kuwa na shauku ya kuona kila mtoto anapata elimu bora katika mazingira bora.
Ni aibu kwa Serikali yenye rasilimali za kutosha kuwa na shule za aina hii, hasa wakati huu. Wito wetu, Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka na za dharura ili kumaliza hali hii, ili wanafunzi waweze kujifunza katika mazingira bora.
Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kufanya tathmini ya fedha zinazotolewa kwa minajili ya ujenzi wa madarasa na miradi mingine ya maendeleo. Na ikibainika ubadhirifu wowote, wahusika wachukuliwe hatua stahiki za kisheria na kinidhamu.