Baada ya kusoma chini ya mti, wanafunzi sasa wajengewa madarasa

Mafundi wakiendelea na ujenzi wa vyumba vingine vitatu vya madarasa pamoja na ofisi ya walimu. Picha na Haika Kimaro
Muktasari:
Tayari vyumba viwili vya madarasa vimeshaezekwa huku wanafunzi wa darasa la tatu na nne wakivitumia na vyumba vingine vitatu pamoja na ofisi ya walimu vikibakia kidogo kukalika kujengwa.
Mtwara. Baada ya kusoma chini ya miti na katika madarasa ya udongo yaliyoezekwa kwa nyasi kwa muda mrefu hatimaye wanafunzi wa Shule ya Msingi Mitambo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara , sasa wanasoma katika madarasa ya kudumu.
Tayari vyumba viwili vya madarasa vimeshaezekwa huku wanafunzi wa darasa la tatu na nne wakivitumia na vyumba vingine vitatu pamoja na ofisi ya walimu vikibakia kidogo kukalika kujengwa.
Januari 24, 2018 MCL Digital ilieleza hali halisi ya wanafunzi 229 wa darasa la tatu, nne, tano na sita wa shule hiyo kusomea chini ya miti kutokana na uhaba wa madarasa.
Awali, shule hiyo ilikuwa na madarasa matatu pakee ya kudumu ambayo yalitumiwa na wanafunzi wa darasa la kwanza, pili na saba kutokana na kuhitaji kuwa chini ya uangalizi zaidi.
Akizungumza leo Mei 16, 2018 mmoja wa walimu aliyekuwa na darasa chini ya mti, Halima Juma amesema kwa sasa amekuwa na furaha baada ya wanafunzi wake kuanza kusomea ndani ya madarasa.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Rashidi Chalido amesema licha ya Serikali na wadau kuonyesha jitihada za kuiboresha shule hiyo, bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji.