Shule ya Mitambo yatoka chini ya mikorosho, yajengewa madarasa

Muktasari:
Hiyo ni kauli ya Khadija Likumbo, mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Mitambo iliyoko halmashauri ya wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara alipokuwa akizungumzia maboresho ya miundombinu na madarasa shuleni hapo.
“Asante gazeti la Mwananchi. Habari kuhusu miundombinu mliyoiandika imetuwezesha, sasa tunasoma kwenye madarasa bora kutoka yale ya miti tuliyokuwa tukitumia awali, mvua iliponyesha tulikatisha masomo kwenda kujihifadhi kwenye madarasa ya udongo yaliyoezekwa kwa nyasi na sasa tunasoma kwa bidii na walimu wanatufundisha.”
Hiyo ni kauli ya Khadija Likumbo, mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Mitambo iliyoko halmashauri ya wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara alipokuwa akizungumzia maboresho ya miundombinu na madarasa shuleni hapo.
Akizungumza wakati wa mahojiano maalum shuleni hapo, Khadija alionekana kuwa mchangamfu na kuomba nafasi ya kuzungumza.
Alizungumzia ubora wa vyumba vya madarasa vinavyojengwa kwa ushirikiano kati ya wadau wa elimu, wazazi na Serikali na pia akapongeza ari na bidii ya kufundisha na kujifunza miongoni mwa walimu na wanafunzi.
Januari 25, gazeti la Mwananchi lilichapisha habari kuhusu wanafunzi 229 wa darasa la tatu, nne, tano na sita wa shule hiyo waliokuwa wakisomea chini ya miti na wenye bahati walikuwa wakisoma kwenye madarasa ya udongo yaliyoezekwa kwa nyasi kutokana na uhaba wa madarasa shuleni hapo.
Habari na makala hiyo ilimfanya mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa kufanya ziara katika shule za halmashauri hiyo na kubaini kuwepo shule 10 zenye hali na mazingira kama Shule ya Mitambo.
Ziara hiyo ya mkuu wa mkoa ilihitimishwa kwa kufanyika kikao cha wadau wa elimu ambapo kwa pamoja Serikali, wadau na wazazi waliazimia kutafuta ufumbuzi wa upungufu wa zaidi ya vyumba 48 vya madarasa katika shule alizotembelea kiongozi huyo.
Ujenzi uliokamilika wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Mitambo iliyorejesha nuru ya matumaini, ari na bidii ya kufundisha na kujifunza miongoni mwa walimu na wanafunzi ni matokeo ya makala hizo.
INAENDELEA UK 28
INATOKA UK 27
Makala hizo zilihamasisha juhudi za Serikali na wadau wa elimu mkoani Mtwara kujenga vyumba bora vya madarasa, vyumba viwili zaidi vipo katika hatua za mwisho kukamilika na baadaye kutumiwa na wanafunzi wa shule hiyo.
Walimu, wanafunzi wafurahia
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Rashidi Chalido anapongeza juhudi za kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia shuleni hapo huku akiomba ujenzi wa vyumba vya madarasa uende sambamba na upatikanaji wa huduma nyingine ikiwemo maji.
“Tunawashukuru wadau wote waliojitokeza kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa akiwemo mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia lakini bado tuna changamoto ya huduma ya maji kwa matumizi ya wanafunzi na walimu,” anasema Chalido.
Kauli hiyo ya mwalimu mkuu inaungwa mkono na mwalimu Halima Juma aliyekuwa akifundisha madarasa ya chini ya miti akisema utimilifu wa kuboresha huduma na miundombinu shuleni hapo utakamilika siku maji yatakapoanza kupatikana.
Mwanafunzi wa darasa la nne, Issa Masoud ambaye naye darasa lake lilikuwa chini ya mti wa mkorosho hakuficha furaha yake na kuiomba Serikali na wadau wa elimu kutupia macho pia suala la huduma ya uhakika wa maji safi na salama shuleni hapo.
“Kama unavyoniona nina furaha, tofauti na tulipozungumza awali; furaha hii inatokana na kusoma kwenye darasa jipya tofauti na awali tulipokuwa tukisomea chini ya miti ya mikorosho. Furaha yangu itakamilika tukipata huduma ya maji,” anasema Masoud.
Mmoja wa wazazi wenye watoto shuleni hapo, Hadija Hassan anaiasa jamii kutimiza wajibu kwa kuchangia gharama za kuboresha mazingira na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia badala ya kubweteka na utekelezaji wa sera ya elimu bure ya msingi inayotekelezwa na Serikali.
Maji ya ujenzi yapatikana kilomita mbili
Si kazi rahisi kutekeleza mradi wa ujenzi wa madarasa katika shule hiyo kutokana na ukosefu wa maji, iliwalazimu wazazi ambao walijitolea nguvu kazi kulazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita mbili kwenda na kurudi kwa ajili ya kuteka maji.
“Wananchi wote bila kujali jinsi zao walikuwa wakijitwisha ndoo na madumu ya maji kutoka umbali wa kilomita mbili, tunashukuru hili limefanyika kwa moyo bila watu kusukumwa,” anasema Salum Akola, mwenyekiti wa kijiji cha Mitambo akizungumzia mradi huo.
Anaongeza: “Wenye baiskeli walipata nafuu kidogo lakini wananchi hawakukata tamaa na bado tunaendelea hadi tukamilishe madarasa yote.”
Mkakati wa halmashauri
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Omari Kipanga anasema ifikapo Desemba, mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa utakuwa umekamilika katika shule 10 zenye upungufu wa vyumba vya madarasa.
“Jumla ya madarasa 16 kati ya 48 yanayohitajika katika shule hiyo tayari yamekamilika na wanafunzi kuanza kuyatumia,” anasema Kipanga
Baada ya awamu ya pili ya ujenzi unaohusu madarasa 32 yaliyosalia, kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, nguvu zaidi zitaelekezwa katika miundombinu mingine ikiwemo vyoo, ofisi na nyumba za walimu na madawati ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anasoma akiwa ameketi chini.
Akizungumzia changamoto ya huduma ya maji, Kipanga anasema halmashauri inatekeleza miradi ya kuchimba visima na kuvuna maji ya mvua kama moja ya njia za kukabiliana na tatizo la ukosefu wa maji katika halmashauri ya wilaya ya Mtwara.
“Tumepanga kuchimba visima 30 katika kijiji cha Mitambo, tayari tumechimba visima vinane kati ya 15 vilivyopo katika awamu ya kwanza ya mradi,” anasema.
Anazitaja shule za Msingi Nanyani na Nanyati kuwa miongoni mwa shule ambazo tayari mradi wa visima vya maji na matanki ya kuvuna maji ya mvua imetekelezwa.