Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tunashindwaje kulijenga Jiji la Dar es Salaam?

Kama wewe ni mkereketwa wa sekta ya ujenzi na majengo, basi si ajabu kwamba umekuwa ukifuatilia namna ambavyo wakazi wa Nairobi Kenya, wamekuwa wakiweka machapisho kwenye mitandao ya kijamii, hasa Facebook wakiisifia Nairobi.

Wanakwenda mbali zaidi na kuweka majengo marefu ya kupendeza na pia kuonesha mipango ya ujenzi itakayofanyika siku za usoni.

Ukifika pale Nairobi, eneo la Westland kuna majengo marefu ya kuvutia yenye ghorofa zaidi ya arobaini. Aidha ujenzi wa barabara ya Nairobi Expressway umebadilisha sana taswira ya Nairobi.

Pamoja na hayo, kuna miradi mingine ya ujenzi inayoendelea kama 88 Nairobi Condominium Tower (ghorofa 44), Montave Sourthen Tower (ghorofa 40), The Pinnacle Tower I (ghorofa 70) na Pinnacle Tower II (ghorofa 46).

Miradi hii ni baadhi tu iliyo kwenye mipango, ikiwamo ujenzi wa smart cities mbalimbali ndani ya Nairobi, kama Africa’s Silicon Savannah.

Ukienda Ethiopia (Addis Ababa) ambayo ipo ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki kuna jengo la Commercial Bank of Ethiopia, lenye ghorofa 46 pamoja na majengo mengine ambayo ujenzi wake unaendelea.

Miradi hii, siyo kwamba inakusudia tu kubadilisha sura ya miji hiyo, lakini pia inaongeza wigo wa vivutio vya utalii wa majengo.

Majengo marefu, barabara za kisasa zinazotumia teknolojia za kisasa huvutia wengi na kuwafanya wavutiwe kutembelea miji ya namna hiyo.

Dar es Salaam, ambayo ni lango la kuingia au kutoka kwenda nchi za ng’ambo, lazima liwe na sura ya kusisimua.

Msisimko wa kwanza anaoupata msafiri anayeingia kwenye jiji lolote lile, huanza na mwonekano wa majengo na miundombinu ya barabara anamopita. Majengo marefu huufanya mji uonekane wa kisasa na hii hutengeneza fursa zaidi za uwekezaji.

Nikiitazama Dar es Salaam yetu, siioni ikiwa kwenye ushindani na miji kama Nairobi, Addis Ababa, Johannesburg, Cairo, Lagos na miji mingine.

Ni kama vile Dar es Salaam imelala kana kwamba imeshajijenga ikamaliza na haihitaji kujijenga tena. Kati ya mwaka 2005 na 2015 ilikuwa ni jambo la kawaida kuona mitambo ya ujenzi ikining’inia angani kwa ujenzi wa majengo.

Ujenzi wa mwisho wa jengo refu, ulikuwa ni ule wa Mzizima Tower (ghorofa 35) ambao nao ulisimama kidogo kabla ya kuendelea miaka ya hivi karibuni.

Pengine kuna miradi mingine ipo kwenye makaratasi inasubiri wakati mwafaka kutolewa hadharani.

Lakini usingizi ambao Dar es Salaam imelala, unainyima fursa nyingi sana za kuwa mji wenye ushindani ndani Afrika Mashariki, Afrika chini ya jangwa la Sahara na Afrika nzima kwa ujumla.

Natambua kuwa kuna miradi ya ujenzi wa barabara za mwendokasi, upanuzi wa baadhi ya barabara zinazoingia jijini na miradi mingineyo.

Miradi hii pekee haitoshi kuiremba Dar es Salaam na kuifanya ionekane kuwa jiji hai sawa na mingine Afrika ambayo uhai wake si wa kutafuta kwa tochi.

Dar es Salaam ni kama haipo kwenye mashindano ya kuwa mji wenye ushawishi ndani ya Afrika.

Yalikuwa ni matumaini yangu kwamba, kasi ile ya ujenzi wa Jiji la Dar es Salaam iliyoonekana kati ya mwaka 2005 na 2015 ingekuwa mara 10 zaidi kwa leo. Tulitegemea kuona majengo marefu zaidi ya ghorofa ya TPA One Stop Center yakijengwa.

Tulitarajia pia kuona ujenzi wa maduka makubwa zaidi ya Mlimani City, maeneo makubwa ya maegesho, barabara za chini ya ardhi, maeneo ya wazi yaliyoboreshwa na fukwe zilizoboreshwa.

Sambasamba na ujenzi wa miundombinu ambayo inapendezesha mji, tulitarajia pia kuona mifumo ya mawasiliano ya kimtandao, inakuwa bora zaidi.  Jiji letu lina shida ya kupata mtandao tofauti na maeneo mengine.

Mambo haya yanaifanya Dar es Salaam kupoteza ile hadhi ya mji mkuu wa kibiashara, hali ambayo siyo tu kwamba inafifisha hadhi yake, lakini pia inafifisha ukuaji wa miji mingine ambayo ingepambana kuifikia.

Inawezekana kuna miradi mingi kwenye makabrasha ambayo haijatangazwa, lakini ukweli unabakia kuwa tumeacha kuijenga Dar es Salaam yetu.

Taratibu tunaanza kuiondoa kwenye ile orodha ya majiji yanayokua zaidi duniani ambapo miaka 10 iliyopita, Dar es Salaam ilikuwa namba tisa kati ya miji inayokua duniani. Tuamshe tena ari ya kuijenga Dar es Salaam.

Sekta binafsi ipewe nafasi kubwa na ijengewe mazingira wezeshi ya kuijenga Dar es Salaam kama ambavyo nchi nyingine zimefanikiwa kujenga miji yao kupitia sekta binafsi.


George Mwiga ni wakili wa kujitegemea. WhatsApp: 0786046484