Tanzania tunahitaji lugha zaidi ya Kiingereza

Kiswahili ndio lugha mama ya mawasiliano nchini Tanzania, na imekuwa maarufu kwa watu wa Afrika Mashariki.
Hata hivyo, wakati mfumo wa elimu wa sasa unaruhusu kufundisha lugha kimataifa, ipo haja ya kuwa na mafunzo ya lugha nyingine nje ya Kiingereza.
Oman ni taifa la Kiarabu ambalo lugha yake ya taifa ni Kiarabu kisha Kiingereza, hata hivyo ziko baadhi ya shule zimeanza kufundisha lugha ya Kichina na inawezekana pia kuongeza lugha ya Kiswahili ambayo nayo inazungumzwa na wengi.
Ukuaji uchumi wa Tanzania umekuwa ukiwavutia wawekezaji kutoka nje na wageni kutoka mataifa mbalimbali. Ni kwa sababu hii, nashauri iwepo fikra ya kufundishwa lugha za kigeni shuleni mbali ya Kiingereza.
Lugha kama Kifaransa na Kichina kwa sasa zimetawala katika mataifa mbalimbali ulimwenguni na hii ni kutokana na mwingiliano wa biashara na uwekezaji na ndio maana hapa Oman mpango huo upo.
Kufundishwa lugha za kigeni hapa Oman huenda ni kuona umuhimu wa mawasiliano baina ya watu katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, na ikumbukwe kuwa taifa hili limeendelea kiuchumi na kuwafanya watu kutoka mataifa mbalimbali duniani kuitembelea.
Sekta ya mafuta na gesi hapa Oman ndio nguzo kuu ya uchumi na kwa mujibu wa kumbukumbu, mwaka 1960 kwa mara ya kwanza mafuta yaligunduliwa eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.
Nchini Tanzania kuna hatua kubwa imefikiwa katika uwekezaji ikiwemo ujio wa bomba la mafuta kati ya Hoima nchini Uganda na Chongoleani mkoani Tanga ambapo wapo wageni wengi wanataka kuwekeza baada ya kuona fursa zilizopo..
Mbali ya bomba la mafuta iko miradi mingi ya uwekezaji ikiwemo bandari, ujenzi na uzalishaji mali viwandani, ambayo inahitaji lugha ya mawasiliano baina ya pande mbili, badala kuwa na mkalimani mmoja wa maneno na hivyo kupunguza kasi ya ufanisi katika kazi.
Dhamira ya Serikali kufungua milango ya uwekezaji ni moja ya vivutio vya wageni kutaka kuwekeza na ndio maana nikasema uwepo umuhimu wa lugha za kigeni zaidi kufundishwa shuleni nje ya Kiingereza.
Mwaka 2016, Serikali ilitarajia kuanza kufundisha lugha ya Kichina kama somo katika shule za sekondari na vyuo, ambapo ilidaiwa kutengwa kwa shule sita za majaribio ya ufundishaji katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.
Kwa mujibu wa tovuti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), serikali ya China ilitoa walimu zaidi ya 130 ili kufundisha lugha ya Kichina katika shule na vyuo nchini Tanzania.
Hata hivyo, vipo vyuo binafsi Tanzania ambavyo vinafundisha lugha za kigeni Bara na Visiwani zikiwemo Kichina, Kifaransa, Kijerumani na Kitaliano, lakini haitoshi na badala yake, ni vyema lugha hizo zikafundishwa kwa utaratibu shuleni.
Utalii visiwani Zanzibar umekuwa chachu ya vijana wengi kuhamasika kutaka kujifundisha lugha za kigeni mbali ya Kiswahili na Kiingereza.
Lugha ya Kiarabu inachukua nafasi ya tatu kuzungumzwa visiwani Zanzibar (Unguja na Pemba) na ikumbukwe kuwa lugha hiyo inafundishwa kuanzia shule za awali, msingi, sekondari pamoja vyuo.
Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) mbali ya kuendesha kozi mbalimbali za masomo ikiwemo kilimo, afya, biashara, uhasibu pamoja na Teknolojia ya Mawasiliano, pia kimekuwa kikiendesha kozi za muda mfupi za lugha za kigeni.
Pia kipo kituo kinachojulikana kama ZOI Zanzibar kinachofundisha lugha za kigeni kama Kifaransa, Kijerumani, Kichina Kitaliano, Kihispania na Kiarabu, huku vijana wengi wakihamasika kujiunga na kozi hizo kwa malengo ya kupata ajira na kujiajiri.
Vijana hawa wamekuwa wakikimbilia kujifundisha lugha za kigeni kwa lengo wawe wakalimani kwa wageni katika maeneo mbalimbali ya kitalii yakiwemo majengo ya kale yaliyopo Mji Mkongwe Zanzibar pamoja na mbuga za wanyama Tanzania Bara.
Mbali ya utalii wa Zanzibar pia zipo mbuga za wanyama Tanzania Bara ikiwemo ya Ngorongoro, Mara, Serengeti, Mikumi na Saadan ambapo vijana ni fursa kwao kujiajiri ikiwa tu watajua kuzungumza lugha za kigeni.
Kwa muktadha huo, nashauri iwepo haja kwa Serikali kuongeza lugha za kigeni kama sehemu ya mtalaa ili zifundishwe kwa ngazi zote kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu.
Kwa mazingira ya sasa duniani, Watanzania hawana budi kuwa na umilisi wa lugha zaidi ya moja. Fursa zipo kwa watu wanaojua lugha mbalimbali.
Salim Mohammed ni mwandishi wa habari aliye safarini nchini Oman