TAHARIRI: Tuyatafakari malengo ya Uhuru

Rais Samia Suluhu Hassani akikagua gwaride wakati wa sherehe za kutimiza miaka 60 ya Uhuru Tanganyika katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam zilizofanyika mwaka jana. Picha na Maktaba

Muktasari:

Leo ni Desemba 9, siku ambayo Watanzania tunaadhimisha Uhuru wa Tanganyika, nchi ambayo ilipoungana na Zanzibar ikaundwa Tanzania.

Leo ni Desemba 9, siku ambayo Watanzania tunaadhimisha Uhuru wa Tanganyika, nchi ambayo ilipoungana na Zanzibar ikaundwa Tanzania.

Imetimia miaka 61 tangu Taifa letu adhimu lilipoondokana na makucha ya mabeberu wa Kiingereza.

Ndio siku ambayo Watanzania tunaikumbuka kila mwaka kama siku kielelezo kwa Watanzania kufurahi kurudi kwa utu na uhuru wao kama Waafrika na binadamu.

Hata hivyo, mwaka huu kwa mujibu wa Serikali, maadhimisho hayo hayatakuwa yale ya shamrashamra, zikiwamo za gwaride maalumu la vikosi vya ulinzi na usalama, bali Serikali imeagiza bajeti ya Sh960 milioni iliyotengwa kwa ajili ya shughuli hiyo, ipelekwe katika ujenzi wa mabweni ya shule za wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Agizo hilo la Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene halikuishia hapo, limetaka Watanzania kuitumia siku hiyo kufanya midahalo na makongamano kuhusu maudhui mapana ya siku hiyo.

Bila shaka katika midahalo hiyo, tafakuri mojawapo ambayo tunadhani inaweza kuuweka mjadala wa uhuru katika mahala sahihi ni hoja kama malengo ya Uhuru wetu yamefikiwa.

Haya ni malengo ya kuwa na Tanzania huru ambayo Watanzania wenyewe kwa umoja wao watakuwa na fursa ya kujiletea maendeleo.

Hata hivyo, pengine tunaweza kuuliza swali; Je, Watanzania wako huru na kwa namna gani uhuru huo unajiakisi kwenye maendeleo na ustawi wa mwananchi mmojammoja na hata Taifa kwa jumla?

Tunalazimika kuuliza maswali haya hasa tunapoangalia mwenendo wa mambo ndani ya miaka 61 ya uhuru. Bado kuna malalamiko ya watu wengi kutwezwa utu na heshima zao, mipaka kwenye uhuru kama vile kuamua aina ya itikadi za siasa za kufuata na mambo mengineyo.

Lakini kubwa zaidi ni kuwapo kwa hoja kuwa hata kiwango cha maendeleo kilichofikiwa ndani ya kipindi hicho cha zaidi ya nusu karne, bado hakijawakosha wengi, hasa kutokana na rasilimali ambazo nchi yetu imejaaliwa.

Ndani ya miaka ya Uhuru na taifa kuruhusu siasa za ushindani wa vyama vingi kama chachu ya kuiletea nchi maendeleo, baadhi ya watu hawaamini kama wanaweza kutofautiana kwa itikadi zao za kisiasa, lakini bado wakabaki kuwa wamoja kama Watanzania.

Kinachoonekana ni kama kosa kubwa mtu kuwa upande fulani ambao unakinzana na wale walio upande wa mamlaka. Kipindi fulani katika miaka ya karibuni, ilikuwa ni kosa mtu kukosoa Serikali hata kwa nia njema.

Waliofanya hivyo walipewa majina mbalimbali mabaya na hata kushughulikiwa kama vile si Watanzania wanaopaswa nao kukusanya fito na kujenga nyumba yao Tanzania.

Miaka 61 ya uhuru, tunashuhudia hata sheria zikitungwa kwa ajili ya kukomoa kundi fulani la watu kisha baadaye tunakuja kutanabahi baada ya wengi kuathirika na kuanza kutumia gharama kubwa kuzifanyia mapitio sheria hizo.

Hata yale mambo ambayo kama Watanzania tunayaanzisha kwa mustakabali mwema wa Taifa hayafiki mwisho. Tuna mfano mzuri wa kukwama kwa mchakato wa Katiba Mpya ambao licha kuanza vizuri ulikuja kuharibika mwishoni kwa sababu za masilahi ya kisiasa.

Haya ni machache kati ya vilio, manung’uniko, lawama nyingi ambazo Watanzania wanayo ndani ya mioyo yao. Ni kero muhimu zinazopaswa kufanyiwa tafakuru tunduizi katika siku hii adhimu, ambayo tunaamini kila kona ya nchi kutakuwa na mijadala kuhusu maana ya uhuru wetu.