Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TAHARIRI: Tusiyakubali matumizi haya ya dawa

Katika gazeti letu la jana, tuliandika tahadhari iliyotolewa na Serikali juu ya matumizi ya dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARVs) kunenepesha mifugo kama kuku na nguruwe na kuleta usugu wa dawa hiyo kwa binadamu.

Jambo hili halikubaliki hata kidogo hivyo tunatoa rai kwa wananchi wenye tabia hizo kuacha mara moja matumizi holela ya dawa au kutumia dawa za binadamu, kunenepesha mifugo bila kujali athari za matumizi hayo kwa binadamu.

Kulingana na taarifa ya watafiti na wanasayansi, ni kwamba kumekuwepo na matumizi holela ya ARV yanayochangia usugu wa dawa hizo, baada ya baadhi ya wafugaji kuzitumia vibaya hizo kwa lengo la kunenepesha mifugo yao.

Hii ndio imeifanya Serikali na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), kuonya kuwa kitendo wanachokifanya ni kinyume na sheria za nchi, kwani zinatakiwa zitumike tu kwa ajili ya kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi kwa binadamu.

Kulingana na TMDA na Serikali, matumizi ya ARV kwa mifugo kunafanya mazao ya mifugo hiyo kutofaa kwa matumizi ya binadamu kwani inaleta usugu za dawa hizo kutokana na wingi wa mabaki ya vimelea vya dawa hizo kwenye kitoweo.

Tunaungana na Serikali na TMDA kutahadharisha juu ya matumizi hayo kwani wakati wafugaji hao wakifurahi unene wa mifugo yao na kupata kipato kikubwa zaidi katika biashara, wanaleta madhara makubwa kwa afya ya binadamu.

Jambo hili halikubaliki kwa mtu yeyote anayefikiri sawasawa kwani inafifisha juhudi za Serikali na wadau za kupambana na virusi vya Ukimwi wakati nchi ikishuhudia kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Takwimu za Desemba 2023 zinaonyesha kiwango cha watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na wanaotumia ARV ni asilimia 97.9 kulinganisha na asilimia 93.6 mwaka 2016/17 na kiwango cha wanaotumia dawa na wamefubaza VVU ni asilimia 94.3 mwaka 2022/23 kulinganisha na asilimia 87 mwaka 2016/17.

Kwa hiyo tukiruhusu matumizi ya ARV kunenepesha mifugo, tutafifisha jitihada hizo za Serikali na wadau, lakini kibaya zaidi ni kuwa tunakwenda kuathiri afya za wanaotumia vitoweo hivyo.

Kwa upande mwingine, jamii inapaswa kupaza sauti si kwa matumizi holela tu ya ARV, bali matumizi mengine yoyote holela ya dawa kwani husababisha usugu wa dawa hizo.

Tunasema hivyo kwa sababu hivi sasa kuna matumizi holela ya antibiotiki aina ya Azuma na dawa aina ya Aspirin Junior ambayo sasa inatumiwa na vijana kwa hisia ya kuongeza nguvu za kiume.

Tufuate ushauri wa madaktari wanapo tuandikia na kutushauri dawa gani tunapaswa kutumia na kwa wakati gani ili kuepuka usugu wa dawa dhidi ya vimelea, badala ya kwenda kwenye maduka ya dawa bila kuandikiwa na daktari.

Wataalamu wa afya wanathibitisha kwamba, mazoea ya kumeza dawa pasipo maelekezo wala vipimo sahihi, ni kujimaliza kwani wapo watu imewagharimu maisha baada ya kuwasababishia maradhi ya ini na figo au usugu wa dawa.

Matumizi haya holela ya dawa za binadamu kwa wanyama hayakubaliki kwani tunaweka rehani maisha yetu na maisha ya wengine.

Jamii iamke sasa kufichua wanaotumia ARV kwa Wanyama, isikae kimya.