Tabia ya ‘kupasha viporo’ chanzo maambukizi ya VVU

Muktasari:

Ugonjwa wa Ukimwi bado ni tatizo kubwa katika jamii, hivyo ni muhimu kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na ugonjwa huo.

Ugonjwa wa Ukimwi bado ni tatizo kubwa katika jamii, hivyo ni muhimu kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na ugonjwa huo.

Ni muhimu kuhimiza watu kuchukua tahadhari kwa wale ambao hawajaambukizwa na wale waliokuwa na maambukizi kuzikubali hali zao na kufuata masharti yanayotolewa na wataalamu wa afya, ikiwamo kuwa wafuasi wazuri wa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARV’s).

Miongoni mwa elimu inayopaswa kuendelea kutolewa kwa wananchi ni kuepuka tabia hatarishi ambazo zitawasababishia kupata maambukizi ya ugonjwa huo. Moja ya tabia hizo ni ile inayoitwa ‘kupasha kiporo’. Kuna madhara mengi yanayoweza kusababishwa na tabia hii ya kumrudia mwenza ambaye mmeshaachana, na vijana wengi ndio wapo katika hatari ingawa pia makundi mengine yapo katika hatari hiyo.

Tabia hii imekithiri hasa kwa vijana, kwani unakuta ameshaanzisha uhusiano na mtu mwingine, lakini bado anataka kuendeleza wa yule aliyeachana naye au wakati mwingine hali hii hutokea pia kwa watu ambao walishakuwa kwenye ndoa na kuachana.

Wana lugha yao wanapenda kutumia ‘wanapasha viporo’, wakimaanisha kurudi kwa waliokuwa wapenzi wao na kushiriki tendo la ngono ambayo mara nyingi huwa ngono zembe.

Ni mara chache wapenzi wanaorudiana kukumbuka kwanza kupima afya zao kabla ya kuendeleza uhusiano wao, kwani katika kipindi ambacho hamkuwa pamoja huenda mmoja ameshapata magonjwa ya kuambukiza.

Hali hii kwa kiasi kikubwa inachangia kuenea kwa magonjwa ya zinaa, ukiwemo Ukimwi. Ukimwi ni ugonjwa hatari ambao bado unaendelea kuangamiza watu kila kukicha. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, vijana, hasa wa kike ndio waathirika wakubwa wa ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Juni, 2021 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kiwango cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi ni asilimia 4.9 (asilimia 6.3 ni wanawake na asilimia 3.4 ni wanaume).

Tangu Ukimwi ulipogundulika zaidi ya miaka 40 sasa, bado dunia inaendelea na vita ya kutafuta dawa na chanjo ya ugonjwa huo. Ingawa Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema dunia imepiga hatua kubwa katika mapambano hayo, bado ugonjwa huo ni tatizo kubwa duniani.

Tabia ya ‘kupasha kiporo’ ni hatari, kwa sababu muda ambao hukuwa pamoja na mwenza wako inawezekana kwa namna moja au nyingine kila mmoja alikuwa katika uhusiano mwingine, hivyo huwezi kujua kama bado yupo salama ama la.

Tofauti na Ukimwi, kuna magonjwa mengine ya zinaa kama gono na kaswende ambayo yanaweza kusababishwa na ngono isiyo salama.

Vijana acheni tabia hii, hasa unapojihusisha na mwenza wako bila kuchukua tahadhari yoyote. Ni muhimu kuzingatia matumizi ya kondomu na yanapaswa yawe endelevu ili kujiweka salama wakati wote.

Mbali na tabia hiyo hatarishi kumweka mtu katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza, pia inachangia ongezeko la kuzaliwa watoto wa nje ya ndoa ama kupatikana kwa mimba zisizotarajiwa.

Rai yangu kwa vijana na jamii kwa ujumla ni kujilinda na kujiepusha na tabia inayosababisha vitendo vya namna hiyo kwa sababu gharama ya malipo yake ni kubwa kuliko gharama ya kutenda, hakuna gharama ya kutibu Ukimwi.

Serikali na taasisi binafsi, za kidini na kijamii ziendelee kushirikiana kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza, ili kuwaongezea uelewa juu ya madhara yanayoweza kuletwa na tabia hiyo.

Kupitia utoaji wa elimu zaidi kwa vijana na jamii, nina imani kubwa tunaweza kupunguza tabia kama hizi kwa kiasi kikubwa katika jamii zetu, na kuhakikisha afya za watu katika jamii zinakuwa salama katika nyanja hii.

Jamii pia ina jukumu la kuhakikisha inakemea tabia kama hizi pale zinapoonekana na kuchukua hatua thabithi kuhakikisha mambo kama hayo hayatokei katika jamii husika.

Mwandishi ni mwanafunzi wa mawasiliano ya umma katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (kampasi kuu ya Mwanza). Anapatikana kwa mawasiliano 0672581593 na baruapepe: [email protected]