Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ONGEA NA AUNT BETTIE: Nalazimika kuzaa nje ya ndoa, mke wangu atanielewa?

Swali: Sina nia mbaya ila mazingira yananilazimisha kufikiria ninachotaka kukuambia Anti. Nimeoa huu mwaka wa nne, mke wangu kwa bahati mbaya tukiwa kwenye miezi sita ya ndoa alipata maradhi yaliyosababisha atolewe kizazi. Hilo siyo shida sana na nilikubaliana nalo ili kuokoa maisha yake. Changamoto ni kuwa wakati hilo linatokea hatukuwa na mtoto.

Sitaki kumuacha mke wangu wala sina nia ya kuoa, ila ninataka mtoto angalau mmoja, hivyo nalazimika kuzaa nje ya ndoa, wasiwasi wangu sijui kama mke wangu atanielewa. Naomba nisaidie namuambiaje ili asijisikie vibaya kwa sababu ili ndoa yetu iwe na amani na idumu lazima niwe na mtoto.

JIbu: Pole sana, huu ni mtihani unaozikabili ndoa nyingi, ila nakushauri jipe muda kabla hujaamua unachokifikiria, kwani kwa namna yoyote hilo suala litamuumiza.

Kwanza kitendo tu cha kutolewa kizazi na kujua hatokuzalia si jambo dogo, ukimuongezea na hilo utamuumiza zaidi.

Umesema utakuwa na amani ukipata mtoto nje, fikiria wewe ndiyo ungekuwa na tatizo kisha akakuambia anatamani kupata mtoto nje ungemuelewa, kabla hujaamua kutimiza azma yako fikiria na ufikirie tena.

Mkifunga ndoa mnakubaliana kwa shida na raha, nina imani mkeo angebeba dhima ya kuficha kilichotokea na kukubali kuonekana mgumba asiyezaa ili kuficha tatizo ulilonalo iwapo changamoto ya kiafya ingekupata wewe.

Heshimu hisia za mkeo na kumbuka haya ni maisha, changamoto aliyonayo inaweza kumpata yeyote, ukiwamo wewe wakati wowote maishani.

Ninachomaanisha hapa ni kuwa suala lenu linahitaji hekima zaidi kuliko mihemko na kauli kuwa wewe ni mwanamume lazima uwe na mtoto au watoto.

Hapa ndipo inapoingia umuhimu wa kuwa mkweli na kumheshimu mke wako. Hata kama unajiona unahitaji watoto katika maisha yako, ni lazima uzingatie na kuheshimu hisia za mkeo. Amini usiamini usipotulia kabla ya kufanya maamuzi mkeo anaweza kupata sonona na baadaye changamoto ya afya ya akili. Kwa sababu atakuwa anajiona asiyefaa, asiyependwa na asiye na thamani.

Kama mume, unapaswa kulitambua hilo na kumpa msaada wa kuwa karibu naye na kumhakikisha usalama wa ndoa yake, badala ya kuleta mambo mengine yatakayomuongezea wasiwasi na kutojiamini. Kibinadamu nakuelewa, kitu pekee ninachoweza kukushauri ni kuwa tafuta wakati wa utulivu na kwa busara nyingi mjadili kuhusu kuasili mtoto badala ya kuwaza kuzaa nje ya ndoa.

Anzisha mjadala huo taratibu, mwisho atakuelewa, lakini siyo kuzaa nje ya ndoa, kwani hata dini haziruhusu kuzini. Pia hata kama imani yako inakuruhusu kuoa mke zaidi ya mmoja, basi jitahidi mkeo kutokuwa na uwezo wa kuzaa isiwe ndiyo sababu ya kuoa.

Na ikiwa ni lazima mshirikishe mpaka akuelewe ili kupunguza joto moyoni mwake.

Fikiria pia huyo mwanamke utakayezaa naye huko nje atakuwa na moyo na heshima kwa mkeo ikizingatiwa kuwa atajua umezaa naye kwa sababu mkeo hana uwezo wa kuzaa. Usilete shida zisizo za lazima kwenye familia yako. Kama nilivyosema hapo awali mkeo hali hiyo ikimshinda anaweza kupata tatizo la afya ya akili shida ikawa kubwa zaidi.

Zungumzeni, jadilianeni kuhusu kuasili mtoto, wengi wenye changamoto inayofanana na yako walijaribu njia hii na wakawa na amani. Suala la kuasili mtoto lina nafuu kwenu nyote.

Usipande mbegu mbaya moyoni mwake ukaja kujuta baadaye, mtihani umeshatokea, tafuta namna bora ya kuushughulikia, badala ya kuongeza tatizo.