Ngorongoro Heroes, Futsal zifute historia mbaya AFCON

Siku chache zijazo, timu mbili za taifa za Tanzania za soka zitakuwa na kibarua cha kupeperusha bendera ya nchi katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa umri na jinsia tofauti.
Timu ya soka ya wanaume ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ itakuwa kibaruani huko Misri ambako itashiriki fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika kuanzia Aprili 27 hadi Mei 18 mwaka huu.
Katika fainali hizo, Ngorongoro Heroes imepangwa kundi A ambalo pia lina timu za Misri, Zambia, Sierra Leone na Afrika Kusini.
Kabla ya kibarua hicho cha Ngorongoro Heroes, timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania ya mchezo wa Futsal itakuwa huko Morocco kushiriki fainali za Afcon kwa mchezo huo ambazo zinaanza kesho na kumalizika Aprili 30 mwaka huu jijini Rabat.
Kwenye fainali hizo za AFCON kwa mchezo wa Futsal kwa wanawake, Tanzania imepangwa katika kundi C ikiwa na timu za Senegal na Madagascar.
Fainali zote hizo ni muhimu kwa vile zinatoa washindi ambao wataiwakilisha Afrika katika fainali za dunia ambazo zitafanyika baadaye mwaka huu.
Timu mbili ambazo zitatinga hatua ya fainali kwenye AFCON ya Futsal, zitajihakikishia tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia la mchezo huo zitakazofanyika Philippines kuanzia Novemba 21 hadi Disemba 7, 2025.
Katika fainali za AFCON U20, timu nne ambazo zitatinga hatua ya nusu fainali, zitafuzu moja kwa moja kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo ambazo zitafanyika Chile kuanzia Septemba 27 hadi Oktoba 19.
Ndoto kubwa ya wadau wa mpira wa miguu na Watanzania wengi ni kuona timu zetu za taifa zinashiriki Kombe la Dunia.
Ikumbukwe katika historia, ni timu moja tu ya soka ya taifa ya Tanzania ambayo imewahi kushiriki Kombe la Dunia ambayo ni timu ya taifa ya wanawake kwa umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Girls’ ambayo ilifanya hivyo katika fainali zilizofanyika India mwaka 2022 ambapo iliishia hatua ya robo fainali ilipofungwa mabao 3-0 na Colombia.
Hapana shaka mabenchi ya ufundi ya timu hizo mbili na wachezaji wanafahamu uzito na maana ya kushiriki Kombe la Dunia hivyo wamejiandaa na kujipanga vizuri kuhakikisha wanafanya vizuri ili waweze kushiriki katika fainali za dunia.
Lakini pia kufanya vizuri katika fainali hizo za AFCON mwaka huu kutafuta historia isiyovutia ya timu za taifa za Tanzania ziliposhiriki katika mashindano hayo kwa nyakati tofauti.
Timu yetu ya taifa ya wakubwa ya wanaume ‘Taifa Stars’ haijawahi kuvuka zaidi ya hatua ya makundi katika mara tatu ilizowahi kushiriki AFCON kama ilivyo kwa timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ katika mara moja ambayo ilishiriki.
Ngorongoro Heroes imeshiriki AFCON mara moja na ikaishia makundi kama ilivyo kwa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’.
Timu ya taifa ya wanawake ya Futsal na Ngorongoro Heroes zituondoe katika unyonge huu kwa kufanya vizuri katika mashindano yaliyo mbele yao.