Ndoa yoyote inahitaji maandalizi kisaikolojia

Kama ilivyo kwenye uanachama wa chama au taasisi yoyote, anayefanya hivyo lazima, kwanza ajielimishe aweze kujiunga na chama au taasisi inayomfaa kutokana na uchaguzi, malengo na matarajio yake.
Kufanya hivyo, mhusika anapaswa kumjua anayetaka au kutarajia kumuoa au kuolewa naye. Tofauti ipo hivi, mwanachama wa vyama vingine au makundi tofauti na ndoa, anaweza kuondoka wakati wowote na kujiunga na vingine. Kwenye ndoa ni tofauti.
Wengi huingia kwenye ndoa wakitarajia maisha yenye furaha na mafainiko hadi kifo kiwatenganishe. Lakini wapo ambao hushindwa na kuachana, hata hivyo mwanzo wa uhusiano wao hilo halikuwa lengo lao.
Hili linaweza kuepukika kama wahusika watafanya utafiti wa kutosha na kujielimisha kuhusu wenza, japo na majaliwa yana nafasi yake.
Lazima wahusika wajue ubora, udhaifu na hata ujinga wao kama binadamu kwenye safari hii yenye milima na mabonde na misukosuko lukuki yanaweza kuwakuta. Ukiyajua haya, ujue hutoa fursa kwa wahusika kujiandaa kisaikolojia na kuhiari kuishi pamoja wakifundishana na kuelimishana somo la maisha.
Nani anaajiriwa bila kutakiwa kuonyesha taaluma, akili, uzoefu na uwezo wa kufanya kazi anayoomba? Tusikubali kuingia au kuingizwa kwenye ndoa bila maandalizi na utayari.
Wahusika wasikilize roho na sauti zao za ndani bila kulazimishwa au kushawishiwa na yeyote kwa sababu ni wao watakaoyaishi maisha wanayoingia.
Tunasema hivi kutokana na kuzuka mtindo kwa baadhi ya wazazi kuwalazimisha watoto wao waolewe au kuoa watu fulani kwa kuangalia vitu kama mali na wadhifa wa familia watokazo, wasijue vinaweza kuwa chanzo cha maanguko kama wahusika hawakuchagua wenyewe.
Hili ni muhimu kwa sababu ndiyo wao watakaofurahia au kuumia mambo yakienda yalivyopangwa au ndivyo sivyo.
Kama tulivyosema hapo juu, tofauti na chama au taasisi nyingine ambako mhusika anaweza kuhama na kujiunga bila kuumia au kusababisha matatizo kwake binafsi na wengine, ndoa ni tofauti kabisa. Ikishindikana au kutofanikiwa, huleta hisia hafifu kuwa ndoa ni kifungo au ndoana.
Kwa Waafrika walio wengi, kabla ya kuoa au kolewa au kuoana kama wasemavyo siku hizi, kulikuwa na kipindi maalumu cha kujifunza taasisi hii, nini vinahitajika, havihitajiki, mbinu na miiko ya kuifanikisha na kuifaidi.
Pia, kulikuwa na kipindi cha mhusika na wanafamilia yake kumchunguza mtarajiwa ili kujiridhisha kama anakidhi matarajio na viwango vyao. Kwenye jamii nyingi, walichunguza vitu hatarishi vya kifamilia kama magonjwa ya kuambukiza, tabia mbaya kama uchawi, ulafi, kujinyonga na vingine kama hivyo kulingana na kabila au jamii wanamotoka wahusika.
Kwa Waswahili, kulikuwa na jando kwa wanaume na unyago kwa wanawake. Tunaposema Waswahili, hapa tumaanisha Watanzania ambao lugha yao ya taifa na kitambulisho ni Kiswahili au Waafrika kwa ujumla kwa vile tunafanana kisura na kimila, ukiachia mbali kuwa Kiswahili ndiyo lugha kubwa pekee ya Kiafrika inayoongelewa zaidi Afrika na ulimwenguni. Hivyo, dhana ya Waswahili inaweza kumaanisha Watanzania hata Waafrika kwa ujumla kulingana na anayeitumia na anavyokubaliana nayo.
Kitu kingine muhimu ni kujua historia, tabia, sura, umri na utayari wa anayetaka kufunga ndoa. Kisheria, kuna umri unaoruhusiwa kufanya maamuzi. Hivyo, wahusika wasifichane umri wala tabia zao.
Vitu hivi unaweza kuvificha kwa muda. Baadaye vitafichuka, hasa ikizingatiwa kuwa unaingia kwenye uhusiano wa kudumu. Kuna kisa cha mwanandoa mmoja aliyemdanganya mwenzie umri wake. Walifunga ndoa na wakaishi kwa furaha tele japo kitambo.
Tatizo katika kuficha umri, mhusika hakuwaambia au hakuwa na uwezo wa kuwaambia wote wanaomfahamu. Siku moja wanandoa hawa wakiwa hawana hili wala lile, mwanandoa aliyemficha mwenzie umri alipatikana. Mara nyingi, umri huwa tatizo kwa wanawake kuliko wanaume.
Mume wa mhusika akiwa kazini, aliajiriwa mwanamke mmoja akiwa mfanyakazi mwenzao mpya. Katika kujitambulisha kwa wafanyakazi wenzake, alisema kuwa anatokea sehemu fulani ambacho kilikuwa ni kijiji cha mke wa mwanandoa huyu. Baada ya kumaliza utambulisho wa kiofisi, mwanandoa huyu alimwendea yule mfanyakazi mpya. Walisabahiana kwa uchangamfu na akamuuliza moja kwa moja, “unamjua fulani?” Yule mfanyakazi mpya alijibu, “fulani, alimtaja jina. Namfahamu tumesoma wote. Na isitoshe tumetofautiana siku mbili kuzaliwa.
“Mwanandoa alimuuliza, “una maana ulizaliwa tarehe...” aliitaja. Yule mfanyakazi mpya aliyeonekana dhahiri kuwa mkubwa ikilinganishwa na mkewe alijibu:
“Ndiyo, wote tulizaliwa mwaka...” aliutaja. Yule jamaa alitabasamu ingawa aligundua kuwa mkewe alikuwa mkubwa miaka sita zaidi ya umri aliokuwa amemwambia. Alianza kujiuliza “je, amenificha mangapi na kwa nini?”
Kukatiza kisa kirefu, mwanandoa alimkabili mwenzie na kumuuliza. “Hivi, una cheti cha kuzaliwa?” Mwenzake aliuliza, “unataka cheti cha kuzaliwa cha nini?” Tumalizie.