Muhimu kuwa na mkataba wa ajira kabla ya kuanza kazi
Muktasari:
- Kwa mujibu wa sheria, mkataba ni makubaliano kati ya pande mbili zenye nguvu ya kisheria. Kwa lugha nyingine, ni makubaliano ambayo pande zote mbili zinawajibika kisheria.
Msemo kwamba kazi mbaya ukiwa nayo, unaonyesha uhalisia wa kufahamu aina ya mkataba wa ajira uliosainiwa kati ya mwajiri na mwajiriwa.
Kwa mujibu wa sheria, mkataba ni makubaliano kati ya pande mbili zenye nguvu ya kisheria. Kwa lugha nyingine, ni makubaliano ambayo pande zote mbili zinawajibika kisheria.
Mkataba ni moja ya mambo muhimu sana kati ya haki za mfanyakazi wakati mwingine kuliko hata kiasi cha fedha na marupurupu anayopaswa kulipwa.
Mkataba wa kazi hutoa mwelekeo wa ajira ya mfanyakazi, huonyesha usalama wa ajira, haki na wajibu wa mfanyakazi pamoja na haki na wajibu wa mwajiri, hueleza majukumu ya msingi ya mfanyakazi, muda na mahali pa kazi na masuala mengine muhimu kisheria.
Kukosekana kwa mkataba wa kazi huhatarisha usalama wa ajira yenyewe. Hivyo ni wajibu wa kila mwajiri na mwajiriwa kuhakikisha anapata mkataba wa ajira ikiwezekana hata kabla hajaanza kufanya kazi yenyewe na kulipwa mshahara wake wa kwanza.
Pamoja na uwapo wa kipindi cha matazamio hilo haliondoi umuhimu wa kuwapo kwa mkataba wa kazi. Baadhi ya waajiri wasio waaminifu hutumia kipindi cha matazamio kama kigezo cha kutompa mfanyakazi mkataba wa ajira bila kutambua kwamba inawezekana mtu akasaini mkataba unaoeleza kipindi cha matazamio kitakuwa cha muda gani japo kisheria hakipaswi kuzidi miezi sita.
Katika kipindi cha matazamio, mwajiri anayo haki ya kusitisha mkataba wa kazi endapo hataridhishwa na utendaji wa mfanyakazi au kwa sababu nyingine zozote zinazokubalika na ambazo ni halali kisheria.
Aina ya mkataba wa kazi huonyesha mustakabali wa ajira, humpa mfanyakazi na mwajiri fursa ya kufahamu haki na wajibu wa kila upande hivyo kujenga mazingira mazuri ya utekelezwaji wake kwa kulinda masilahi ya kila mmoja.
Mkataba wowote lazima uwe na vigezo vikuu vinavyojumuisha makubaliano ya pande mbili, malipo na lengo halali kisheria, uwezo wa kuingia mkataba na hiyari ya wahusika. Bila kujali ni aina ipi ya mkataba wa kazi mliosaini, kama kimojawapo kati ya vigezo hivyo kitakosekana, kinaufanya mkataba kuwa batili tangu mwanzo.
Kwa mujibu wa kifungu namba 14 cha Sheria ya Ajira na uhusiano Kazini ya mwaka 2004; kuna aina tatu za mikataba ya ajira ambayo ni usiokuwa na muda maalumu, wa muda maalumu kwa wataalam na kada ya uongozi pamoja na mkataba wa kazi maalumu.
Mkataba usiokuwa na muda maalumu unasainiwa kati ya mwajiri na mwajiriwa ambao unaweza kuonyesha tarehe uliyosainiwa lakini hauonyeshi au hauelezi utaisha lini. Mikataba ya namna hii mara nyingi huwa katika taasisi za umma na baadhi ya taasisi binafsi. Mkataba wa muda maalumu kwa kada ya uongozi huhusisha zaidi kada ya uongozi au mwajiriwa mwenye fani ya aina fulani ambaye huajiriwa kushika wadhifa fulani wa juu katika utekelezaji wa majukumu yake.
Hata hivyo aina nyingine za waajiriwa wanaweza pia kuwa na mkataba wa muda maalumu bila kujali kada anayotoka kulingana na mahitaji ya mwajiri.
Mkataba kwa kazi maalumu unaweza kupewa kipindi maalumu cha kuisha au mara nyingi kuisha kwake hutegemea kuisha kwa kazi husika ambazo mwajiri na mwajiriwa watakuwa wamekubaliana kutekeleza.
Hii yaweza kuhusu utekelezaji wa mradi fulani au shughuli maalumu ambayo kuisha kwake huashiria kufikia mwisho kwa mkataba wa ajira.
Jambo la muhimu na la kuzingatia ni kwamba kifungu namba 15 cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini kinamtaka kila mwajiri na mwajiriwa kuhakikisha kabla ya kuanza kazi, kuna mkataba wa maandishi uliosainiwa kati ya pande hizo mbili.
Pamoja na uwezekano wa kuwapo makubaliano kati ya mwajiri na mfanyakazi ya kuwa na mkataba ulio chini ya mwaka mmoja lakini makubaliano hayo yanapaswa yafanyike kwa sababu za msingi na si kwa lengo la kujaribu kumnyima mfanyakazi baadhi ya haki zake zilizopo kisheria.
Baadhi ya waajiri huingia kwenye makubaliano mapya ya mkataba na mfanyakazi kila baada ya miezi mitatu au sita ili kukwepa baadhi ya gharama zikiwemo kodi na malipo watakayowajibika kumlipa mfanyakazi kwa mujibu wa sheria jambo ambalo halikubaliki kisheria.
Mkataba ndio utakaoeleza aina ya shughuli utakazofanya, mipaka, unawajibika kwa nani, malipo yako, haki zako za msingi, namna ya kuvunja mkataba na masuala mengine muhimu ambayo hamuwezi kukubaliana tu kwa maneno.
Kukosekana kwa mkataba wa maandishi kunahatarisha ulinzi na usalama, haki na wajibu wa mwajiri na mwajiriwa. Usikubali kuanza kazi bila mkataba.
Mwandishi ni wakili, anapatikana kwa namba 0755 545 600.