Mikopo bila maarifa sahihi ya uwekezaji hatari kwa biashara

Taasisi mbalimbali za kifedha zina programu za utoaji mikopo, hususan kwa wajasiriamali wadogo ili kujikwamua na kukuza biashara zao.
Hata hivyo, kwa kuzingatia kwa umakini sifa mahususi za wanufaika wa programu hizo, kuna umuhimu mkubwa kuwepo mafunzo ya uwekezaji sambamba na utoaji mikopo hiyo ili kuweza kufikia tija iliyokusudiwa.
Wajasiriamali wadogo wengi wana mipango ya kibiashara ambayo haina mikakati mahususi, hawana uzoefu mkubwa wa mbinu za uwekezaji, au ufahamu katika mambo ya kifedha kama kuweka rekodi za hesabu na kuhudumia mikopo waliyochukua.
Tafiti zinaonyesha uwezeshaji wajasiriamali wadogo kwa njia ya mikopo umewasaidia kukuza biashara zao siyo kwa sababu ya kuwapa mitaji tu, ila ni kuwa makundi ya wajasiriamali hao waliofaidika walikuwa na uzoefu katika biashara wanazofanya, au waliwahi kupata ujuzi kuhusu uwekezaji na biashara kabla ya kuchukua mikopo.
Nchini Bangladesh ambapo ni chimbuko la dhana ya taasisi za utoaji huduma ndogo za kifedha (microfinance), benki ya Grameen ilipata mafanikio makubwa ya ukopeshaji mwaka 1976 kwa wajasiriamali wadogo wakulima.
Programu ilianza na wakazi wa vijijini ambao kwa muda tayari wanajishughulisha na kilimo kwa mtu mmoja mmoja au katika vikundi kwenye mashamba. Jambo zuri ni kuwa tayari wanufaika walikuwa wana ufahamu mzuri kuhusu mbinu za kilimo na wapi watapata masoko ya mazao yao.
Utoaji wa mikopo ulipoanza ilikuwa ni kama kutia petroli katika moto, uliwawezesha kwa haraka kukuza kilimo chao, kustawi kibiashara na kuweza kurejesha mikopo waliyochukua.
Kwa uhalisia huo wa Bangladesh, unakubaliana na dhana zilizobainishwa katika tafiti nyingine kuwa mikopo kwa wajasiriamali wadogo inatoa matokeo chanya kwa haraka ikiwa imetolewa kwa wanufaika ambao, tayari wapo katika biashara husika kwa muda usiopungua miaka mitatu.
Kwa upande wa Ethiopia, utafiti uliofanyika mwaka 2015 ulionyesha mikopo iliyotolewa na taasisi za huduma ndogo kifedha imefanikiwa kuwasaidia wajasiriamali wadogo, hususani waliowahi kupata mafunzo kama hayo. Jambo hilo pia limeonekana katika nchi za Philipines na Thailand.
Kinyume chake, ni kuwa utoaji mikopo ya ujasiriamali bila kuwa na namna yoyote maalumu kuwasaidia wanufaika hao kuhusu mbinu za kutunza mikopo na kuwekeza ni kuwaingiza katika mtego ambao, baada ya muda wakopaji watakuwa wamenasa kwa kushindwa kurejesha, kuzidiwa na madeni, ukopaji holela, na kwa sababu biashara zao ni ndogondogo, mwishowe ni rahisi kufa kabisa.
Utafiti uliofanywa nchini India mwaka 2018 umewahi kuonesha baadhi ya mbinu za ukopeshaji wa taasisi zinazotoa huduma ndogo za kifedha sio rafiki kwa ukuaji wa biashara ndogondogo, na inawaingiza wakopaji hao katika shimo la umasikini.
Taarifa za BoT Agosti 2023 zinaonyesha kuna jumla ya taasisi na wakopeshaji binafsi 1,352 walioidhinishwa kutoa huduma ndogo za kifedha, hususan kukopesha (hazipokei amana), ikiwa walengwa wakubwa wa taasisi hizo ni ambao wamekosa sifa za kukopa katika mabenki kama wajasiriamali wadogo au watu wa kawaida.
Mafanikio ya ukopeshaji huo yatategemea wanufaika wa programu hizo wana ufahamu kiasi gani kuhusu biashara, uwekezaji, mbinu za masoko na elimu ya fedha.
Tunahitaji kuliangalia kwa umakini kundi hili ambalo kwa kiasi kikubwa ndilo linachochea ukuaji wa uchumi, kwa kuwapa mbinu sahihi za kukuza biashara.