Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mikoa hii isiachwe nyuma kiuchumi

Ripoti ya Utendaji wa Kiuchumi wa Kanda kwa Septemba 2024 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imebainisha changamoto kubwa za kiuchumi zinazozikumba mikoa ya Dodoma, Pwani, Singida, Kagera, na Simiyu.

Pamoja na kuwa na rasilimali nyingi, mikoa hii bado ina kiwango cha chini cha pato la mtu mmoja, hali inayochochea umaskini na kuzorotesha maendeleo ya wananchi.

Utafiti huo unaonyesha kuwa, bila mikakati madhubuti, tofauti ya kiuchumi kati ya mikoa ya Tanzania itaendelea kuongezeka, na hivyo kuhatarisha maendeleo shirikishi ya Taifa.

Mikoa hii ina umuhimu mkubwa katika uchumi wa nchi. Dodoma, kwa mfano, ikiwa ni makao makuu ya Serikali, inapaswa kuwa kitovu cha maendeleo. Hata hivyo, licha ya ongezeko la watu, mkoa huu bado uko nyuma kiuchumi.

Upungufu wa miundombinu bora ya kilimo, viwanda na biashara umezuia wakazi wake kunufaika na fursa zilizopo.

Hali kama hii inajitokeza pia Pwani, ambayo inashuhudia ongezeko la viwanda lakini bado wakazi wake wanakabiliwa na kiwango cha chini cha kipato. Kutokutumia rasilimali za bahari kwa ufanisi, pamoja na mbinu duni za uvuvi, ni moja ya sababu zinazotajwa kuchangia hali hiyo.

Kwa upande mwingine, Singida na Simiyu zinategemea kilimo kama nguzo ya uchumi wao. Hata hivyo, ukosefu wa mbinu za kisasa za kilimo na uhaba wa mifumo bora ya umwagiliaji umesababisha uzalishaji mdogo, hivyo kupunguza kipato cha wananchi.

Kagera, ingawa ni maarufu kwa kilimo cha kahawa, bado haijafaidika ipasavyo kutokana na ukosefu wa viwanda vya kuchakata mazao, hali inayosababisha wakulima kutegemea masoko yasiyo na uhakika.

Serikali inapaswa kuchukua hatua za makusudi kuinua mikoa hii kiuchumi. Kwanza, ni muhimu kuwekeza katika miundombinu ya msingi kama barabara, maji, na umeme ili kurahisisha shughuli za uzalishaji.

Pili, ni lazima kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa, mifumo bora ya umwagiliaji na uanzishwaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao.

Tatu, juhudi maalumu zinahitajika katika uendelezaji wa viwanda vidogo na vya kati ambavyo vitatoa ajira na kuongeza kipato cha wananchi. Hatua hizi zitasaidia kuongeza uzalishaji na kuimarisha uchumi wa mikoa hii.

Viongozi wa kisera wanapaswa kuhakikisha kuwa kunakuwa na sera shirikishi za kiuchumi zinazolenga kuleta usawa wa maendeleo kati ya mikoa.

Mfano mzuri ni mikoa kama Iringa na Mbeya, ambayo imefanikiwa kwa kutumia rasilimali zake ipasavyo kupitia kilimo cha kisasa, uchakataji wa mazao na uwekezaji wa viwanda.

Ikiwa mikoa yenye changamoto itapewa kipaumbele katika mikakati ya maendeleo, Tanzania itaweza kupunguza pengo la kiuchumi kati ya mikoa yake.

Ingawa mikoa inayotajwa kwenye orodha hiyo ni micheche – Dodoma, Pwani, Singida, Kagera, na Simiyu, hii itazamwe kwa ujumla pamoja na mingine, ili mikakati inayowekwa isaidie kuinua taifa zima kiuchumi.

Serikali, sekta binafsi, na wadau wa maendeleo wanapaswa kushirikiana kuhakikisha kuwa rasilimali zilizopo zinatumika kwa ufanisi. Kwa kufanya hivyo, si tu wananchi watanufaika, bali pia uchumi wa Taifa kwa ujumla utaimarika, na hatimaye Tanzania itapiga hatua kubwa katika maendeleo yake endelevu.